FAHAMU NAMNA
YA KUSIKIA NA KUIELEWA SAUTI YA MUNGU ILI IKUSAIDE KATIKA KUFANYA MAAMUZI.
Lengo kuu la somo hili ni kumsaidia Mwanadamu yeyote yule aliyeumbwa kwa
mfano wa Mungu kujua namna anavyoweza kusikia Sauti ya Mungu na Kuielewa Sauti
ya Mungu. Kwanini? Kwasababu ni wachache sana wanao sikia na kuilewa sauti ya
Mungu pamoja na kuwa Mungu huzungumza nao mara kwa mara. Wengine hujiuliza
swali hili; Je ni kweli
Mungu anazungumza na mwanadamu hata sasa? Hili ni moja ya swali ambalo watu wengi
wamekuwa wakijiuliza na kukosa majibu muafaka kwani baadhi yao hawaamini kwamba
ni kawaida ya Mungu kuzungumza na wanadamu. Kama ilivyokuwa katika agano la
kale, agano jipya, naam hata sasa, Mungu ni yeye yule jana na leo na hata
milele.
Maandiko
yanadhibitisha wazi kuwa ni kweli Mungu anazungumza na mwanadamu hata hivi leo
na si Mitume na Manabii tu tunaowasoma katika Biblia, lakini hata mimi na wewe katika
ukawaida wetu Mungu husema nasi.
Mungu
anasema “Enyi watu, nawaita ninyi; Na
sauti yangu ni kwa wanadamu” (Mithali 8:4). Hivyo ni kusudio la somo hili kuongeza
ufahamu wako ili uweze kujua ni kwa namna gani Mungu huzungumza na mwanadamu na
kisha nini ufanye ili kumuelewa Mungu anapozungumza na wewe. Ni muhimu kwanza
tujiulize swali hili muhimu tunapotafakari somo hili, Kwa nini Mungu azungumze/aseme
na mwanadamu? Jibu la swali hili,
linalenga kutaka kujua sababu za Mungu kuzungumza na mwanadamu au mwanadamu
anahitaji kuisikia sauti ya Mungu ili:-
I.
Aishi sawasawa na kusudi au mapenzi ya Mungu awapo hapa duniani. Nitakufundisha na kukuonyesha njia
utakayoiendea; Nitakushauri, jicho langu likikutazama. (Zaburi
32:8)
II.
kujenga na kudumisha mahusiano/mawasiliano mazuri kati yake na
Mungu. Kutoka 33:11
“Naye
Bwana akasema na Musa uso kwa uso, kama vile mtu asemavyo na rafiki yake. Kisha akageuka akarejea
hata maragoni; bali mtumishi wake Yoshua, mwana wa Nuni, naye ni kijana,
hakutoka mle hemani”
III.
kuona kama Mungu aonavyo na hivyo kutafsiri mambo ya rohoni kwa
maneno ya rohoni. Yeremia 1:11-12 “Tena
neno la Bwana likanijia, kusema, Yeremia, waona nini? Nikasema, Naona ufito wa
mlozi. Ndipo Bwana akaniambia, Umeona vema, kwa maana ninaliangalia neno langu,
ili nilitimize.
MAMBO MHUMU
YA KUJUA KUHUSU SAUTI YA MUNGU
Yafuatayo ni
baadhi ya mambo muhimu ya kukusaidia kuijua, kuisikia na kuielewa sauti ya
Mungu, nawe hunabudi kuyafahamu na kuyatenda:-
1. Jenga na
kudumisha mahusiano mazuri na Roho Mtakatifu – Ni vizuri ukafahamu kwamba Roho Mtakatifu
yupo duniani sasa akiliongoza kanisa katika kuyatenda mapenzi ya Mungu. Hivyo uwepo wa mahusiano mazuri kati yako na Roho
Mtakatifu ndio ufunguo wa mawasilaino mazuri kati yako na Mungu. Biblia
inasema wazi kabisa katika 1Wakorinto
2:10
“Lakini Mungu ametufunulia sisi kwa Roho.
Maana Roho huchunguza yote, hata mafumbo ya Mungu… vivyo hivyo na mambo ya
Mungu hakuna ayafahamuye ila Roho wa Mungu”. Andiko hili linatuonyesha umuhimu na nafasi ya Roho Mtakatifu
katika kutusaidia kuisikia sauti ya Mungu. Hivyo jenga na kudumisha uhusiano
wako na yeye, itakusaidia sana katika kiujua na kuisikia sauti ya Mungu.
2. Ongeza
ufahamu wa viashiria (signal) vya mawasiliano kati yako na Mungu Ufahamu wa
viashiria (signal) za mawasiliano kati yako na Mungu ni wa lazima ili kusikia
na kuielewa sauti ya Mungu. Zipo alama mbalimbali kwa kila mwamini ambazo Mungu
hutumia katika kusema naye. Biblia katika 1Samweli
3:9 inasema “… Enenda, kalale, itakauwa AKIKUITA, utasema, Nena, BWANA; kwa kuwa
mtumishi wako anasikia…” Kwahiyo kiashiria kimojawapo ambacho Mungu
anakitumia kusema na Mwanadamu ni KUITA, naam anaweza kukuita kwa sauti itokayo
kinywani pake au KWA NJIA KUKULETEA ALAMA/VIASHIRIA VYENYE KUKUFANYA UJUE MUNGU
ANANIITA.
Kama ilivyo
kwa jinsi ya kibinadamu anayekuita si lazima aongee, anaweza kutumia alama za
mikono au hata maandishi nk, kukuita. Katika kukuita kwa njia ya
viashiria/alama Mungu anaweza kuleta
nguvu/msisimuko/ubaridi/maumivu fulani kwenye sehemu ya mwili wako au
huzuni moyoni mwako kama ishara/kiashiria cha uwepo wake juu yako na hivyo
KUTAFUTA/KUTAKA USIKIVU WAKO ILI ASEME NAWE. Hivyo ni lazima uwe na ufahamu na
utafute kujua kuhusu alama/namna ya kwako ambayo Mungu hutumia kutafuta usikivu
wako.
N: B Tambua
kuwa Ipo namna ya kwako ambayo Mungu hupenda kusema na wewe ambayo inaweza
kabisa ikawa tofauti na anavyosema na rafiki yako, Mke, Mume au ndugu yako. Ni
jukumu lako kujua viashiria hivyo kwa upande wako kwa kumuuliza Roho Mtakatifu
pekee ambae hutufunulia siri za Mungu. Usijefanya vitu kwa Mkumbo au kuiga
kutoka kwa rafiki yako na ikakugharimu.
3. Ni lazima
ujue kutofautisha sauti ya Mungu na sauti nyingine. Hapa ndipo penye mtihani mkubwa sana kwa watu wengi mno, kama ilivyokua
kwangu kabla sijajifunza kuhusu jambo hili. Ni muhimu sana kwako kulielewa ili usije
ukaipuuza sauti ya Mungu kwa kudhani ni mawazo yako au ni ya Shetani au usije
ukatekeleza jambo ukiamini kwamba Mungu amesema nawe kumbe Shetani ndiye
alisema nawe. Shida ya namna hii aliipata Samweli wakati huo akiwa mtoto na
Mungu alikusudia kumuita kwaajili ya Taifa la Israeli. Mungu alimuita kwa sauti
yake lakini hakuitambua, badala yake alifananisha na sauti ya Babu yake Mzee
Eli. Maandiko yanasema “Ikawa wakati huo, Eli alipokuwa amelala
mahali pake (tena macho yake yalikuwa yameanza kupofuka, hata asiweze kuona),
na taa ya Mungu ilikuwa haijazimika bado, na Samweli alikuwa amelala katika
hekalu la Bwana, palipokuwa na sanduku la Mungu; basi, wakati huo Bwana
akamwita Samweli; naye akasema, Mimi hapa. Akamwendea Eli kwa haraka, akasema,
Mimi hapa; kwa maana uliniita. Akasema, Sikukuita; kalale tena. Naye akaenda,
akalala tena. Bwana akaita mara ya pili, Samweli! Samweli! Akaondoka akamwendea
Eli, akasema, Mimi hapa; kwa maana uliniita. Akajibu, Sikukuita, mwanangu;
kalale tena. Basi Samweli alikuwa hamjui Bwana bado, na neno la Bwana lilikuwa
bado halijafunuliwa kwake. Bwana akamwita Samweli mara ya tatu. Naye akaondoka
akamwendea Eli, akasema, Mimi hapa; kwa maana uliniita. Ndipo Eli akatambua ya
kuwa Bwana ndiye aliyemwita yule mtoto. Kwa hivyo Eli akamwambia Samweli,
Enenda, kalale; itakuwa, akikuita, utasema, Nena, Bwana; kwa kuwa mtumishi wako
anasikia. Basi Samweli akaenda akalala mahali pake. Bwana akaja, akasimama, akaita
vile vile kama kwanza, Samweli! Samweli! Ndipo Samweli akasema, Nena, Bwana;
kwa kuwa mtumishi wako anasikia” (1Samweli 3:2-10). Ni muhimu ukaelewa kwamba Mungu anaweza
kusema na wewe hata kama uko katikati ya mkutano wa watu wenye kelele nyingi
sana. Hii ni kwa sababu Mungu hatumii mdomo kusema nasi bali anatumia moyo
wako kuzungumza. Moyo ndio kiungo muhimu cha mawasiliano kati ya mtu na Mungu.
Ukisoma
katika Matendo ya Mitume 12:22
Biblia inasema “Watu wakapiga kelele,
wakasema, Ni sauti ya Mungu, si sauti ya Mwanadamu. Mara
malaika wa Bwana akampiga, kwa sababu hakumpa Mungu utukufu; akaliwa na chango,
akatokwa na roho”. Kauli hii ya
watu ilikuja baada ya Mfalme Herode kuhutubia watu na kutoa maneno makuu. Watu
waliamini kwamba ile ilikuwa sauti ya Mungu, kumbe sivyo na matokeo yake Herode
alipigwa na Mungu akafa.
Katika hili
nataka nikupe Tahadhari ndugu
mpendwa, kuna wakati mtu/watu au watumishi wanaweza kunena mambo makubwa na
watu wakadhani Mungu wa kweli anasema ndani yao, kumbe ni mungu wa dunia hii.
Na ndio maana ni muhimu sana wewe binafsi uongeze ufahamu wako katika kuijua,
kuisikia na kuielewa sauti ya Mungu, ili hata mwanadamu akinena unajua kwamba
hili limetoka kwa Mungu wa kweli au vinginevyo.
Naam!
mpendwa zipo sauti mbalimbali ambazo zote zinalenga kupambana/kuharibu kusudi
la Mungu ndani ya mtu, zipo sauti za wanadamu (wazazi, walezi, mwenza wa ndoa,
viongozi wa kiroho), ipo sauti ya Shetani kupitia majeshi ya pepo wabaya nk. Ni
lazima mwanadamu amjue sana Mungu kiasi cha kutosha ili kuweza kutofautisha
sauti hizi. Njia au namna pekee ya kutofautisha sauti hizi na ile ya Mungu ni
kuwa na uelewa au ufahamu mkubwa wa Neno la Mungu pekee, kwasababu Mungu hawezi
hata siku moja kukuagiza jambo lililo kinyume na Neno lake.
FAHAMU
VIKWAZO VINAVYOWEZA KUPELEKEA KUTOKUSIKIA SAUTI YA MUNGU.
Biblia
imeainisha vikwazo kadhaa vyenye kupelekea mtu kutokuisika sauti ya Mungu. Nitakuonyesha
vikwazo 2 vikubwa na nikupe changamoto ya kuingia ndani Kiimandiko ili kujua
vikwazo vyengine:-
I.
Dhambi au
kuishi maisha ya dhambi. Mungu hapendezwi na Mtu anayeishi katika mazingira au maisha ya
dhambi, (1Yohana 3:4) “Kila
atendaye dhambi, afanya uasi; kwa kuwa dhambi ni uasi”. Maana yake ni
kuwa atendaye dhambi anakua amemuasi Mungu, kwahiyo amekwenda kinyume na sheria
iliyowekwa na Mungu. Matokeo yake mtu huyo na Mungu wanakua mbali kila mmoja
akiacha kujishughulisha na mwenzie. Isaya
59: 1-2 “Tazama, mkono wa Bwana
haukupunguka, hata usiweze kuokoa wala sikio lake si zito, hata lisiweze
kusikia; lakini maovu yenu yamewafarikisha ninyi na Mungu wenu, na dhambi zenu
zimeuficha uso wake msiuone, hata hataki kusikia”. Angalia lilee neno ‘HATA HATAKI KUSIKIA’.
II.
Kukosa
uaminifu.
(Hesabu 12:7-8,). Mungu hupendezwa sana na Mtu aliye mwaminifu kwake siku zote
za maisha yake. Kwa mtu huyo Mungu hujenga mahusiano ya karibu kwa haraka mno
na hata kusemezana nae Zaidi. Maandiko yanalidhibitisha hili pale Mungu
aliposema mwenyewe akiwaambia Haruni na Miriamu “Bwana akashuka katika nguzo ya wingu akasimama pale
mlangoni pa Hema, akawaita Haruni na Miriamu, nao wakatoka nje wote wawili.
Kisha akawaambia,Sikizeni basi maneno yangu;Akiwapo nabii kati
yenu,Mimi,Bwana,nitajifunua kwake katika maono,Nitasema naye katika ndoto.
Sivyo ilivyo kwa mtumishi wangu, Musa; Yeye ni mwaminifu katika nyumba yangu
yote; Kwake nitanena mdomo kwa mdomo, Maana, waziwazi wala si kwa mafumbo; Na
umbo la Bwana yeye ataliona. Mbona basi ninyi hamkuogopa Kumnenea mtumishi
wangu, huyo Musa? (Hesabu 12:5-
8). Uhusiano wa karibu sana aliokua nao Musa na
Mungu ulitokana na UAMINIFU aliokua nao Musa mbele za Mungu. Mungu alimpenda na
kuamua kuingilia kati kwa yeyote yule aliyejaribu kufuatilia au kugusa maisha
ya Musa, hakika ni kama alikua akigusa maisha ya Mungu kwasababu haukunyamaza
hata kidogo. Cheki kilichomtokea Miriamu baada ya kumsemasema Musa kwa habari
ya Mke wake “Hasira za Bwana zikawaka juu yao; naye akaenda zake. Kisha hilo wingu
likaondoka kutoka pale juu ya hema; na tazama, Miriamu akawa mwenye ukoma,
mweupe kama theluji; Haruni akamwangalia Miriamu, na tazama, yu mwenye ukoma.
Kisha Haruni akamwambia Musa, Ee bwana wangu nakusihi sana usituwekee dhambi
juu yetu, kwa kuwa tumefanya ya upumbavu, na kufanya dhambi. (Hesabu
12:9-10). Kwa muda wako unaweza soma habari za Samweli katika ile 1Samweli 2:26-35 utajifunza kitu kuhusu uaminifu kupitia wito wa Samweli.
Ipo mifano
ya wanamapinduzi wengi amabo walifanya mambo makubwa wakiongozwa na sauti ya
Mungu katika kila jambo; akina Daniel, Paulo, Samweli, Yoshua na wengine wengi.
Maisha ya uaminifu mbele za Mungu ndiyo ilikua silaha kubwa ya mafanikio na
ushindi wao dhidi ya wengine.
MAMBO YATAKAYOWEZA KUKUSAIDIA KUJUA NA KUISIKIA SAUTI YA MUNGU
KATIKA MAISHA YAKO.
I.
Unahitaji kufahamu umuhimu wa Mungu kuzungumza/kusema nawe. Zipo sababu
nyingi za Mungu kuzungumza na wanadamu laikini kubwa yenye kuzibeba zote ni ile
iliyoandikwa katika Zaburi 32:8
kwamba “Nitakufundisha na kukuonyesha
njia utakayoiendea; Nitakushauri, jicho langu likikutazama”. Kwanini? Kwasababu mwanadamu haishi duniani
kwa muda ambao Mungu amemuweka kwa kusudi lake mwenyewe, bali ni kwa kusudi la
Mungu pekee.
Ndivyo maandiko yanavyotueleza ukisoma kitabu cha (Warumi 8:28) “Nasi twajua
ya kuwa katika mambo yote Mungu hufanya kazi pamoja na wale wampendao katika
kuwapatia mema, yaani, wale walioitwa kwa kusudi lake. Kwahiyo ili uweze kulitumikia vizuri kusudi la Mungu katika
maisha yako sharti ni kwamba; lazima uongozwe nay eye katika njia sahihi. Na
njia mojawapo ni ya Mungu kusema na wewe. Lengo lake katika kusema na wewe ni
kukuongoza katika njia sahihi kwa kukuondoa kwenye makusudi ambayo yapo nje na
mapenzi yake kwenye maisha yako maana imeandikwa “Kwa kuwa Mungu hunena mara moja,
Naam, hata mara ya pili, ajapokuwa mtu hajali. Katika ndoto, katika maono ya
usiku, Usingizi mzito uwajiliapo watu, Katika usingizi kitandani; Ndipo
huyafunua masikio ya watu, Na kuyatia muhuri mafundisho yao,Ili amwondoe mtu
katika makusudio yake, Na kumfichia mtu kiburi; Yeye huizuia nafsi yake isiende
shimoni, Na uhai wake usiangamie kwa upanga” (Ayubu 33:14-18)
II. Ongeza ufahamu wako kuhusu ulimwengu wa roho. Mambo yote
yanayotokea katika ulimwengu wa mwili yameanzia katika uilimwengu wa roho, naam
maamuzi ya kile ambacho hutokea katika ulimwengu wa mwili hufanyika katika
ulimwengu wa roho. Zaidi hata mapambano (vita vya kiroho) yote aliyoanayo
mwanadamu katika kulitumikia kusudi la Mungu hufanyika katika ulimwengu wa
roho.
Hivyo kuwa
na ufahamu wa ulimwengu wa roho hususani namna ya kuishi na kuwasiliana katika
ulimwengu huo ni muhimu sana kwa mwamini mwenye kutafuta kujua na kuisikia
sauti/mawazo ya Mungu katika maisha yake. Kwa kuwa Mungu ni roho kama alivyo na
Shetani pia. Hebu tusome habari ya Elisha na Mtumishi wake, 2 Wafalme 6:8-17. Maandiko yanatueleza
kwamba Shetani nae ni roho ukisoma Waefeso
6:10-12.
Ndugu
mpendwa usiruhusu yale unayoyapitia au yale ambayo watu /mazingira yanasema juu
yako yabadilishe au kuongoza maisha yako, bali tafuta kuijua na kuielewa sauti
ya Mungu kwenye maisha yako. Na ndiyo maana somo hili limekuja ili kukusaidia
kufika mahala ambapo utaweza kuyatenda mapenzi kamili ya Mungu kwenye maisha
yako.