Monday, January 4, 2016

TAFAKARI UJUMBE WA MWAKA MPYA 2016


JE UMEJIANDAAJE KUKABILI MWAKA 2016?

Nakusalimu katika Jina la Yesu Kristo. Heri ya Mwaka mpya 2016!

Ni kawaida kwa watu wengi kila ifikapo mwanzo mwa mwaka mpya kufanya maandalizi mbalimbali eidha binafsi, familia, ukoo, taasisi na hata nchi. Wengine huanza maandalizi mwishoni mwa mwaka uliokwisha na wengine hufanya mwanzoni mwa mwaka mpya. Ni jambo jema kufanya maandalizi ya kukabili mwaka kwani hukuandaa kuishi sawasawa na ulivyokusudia.

Lakini Je kama Mkristo umejiandaaje kukabili mwaka 2016? Biblia inasemaje kuhusu majira, nyakati na mwaka aliotupa Bwana?

Biblia inatuambia katika kitabu cha Mhubiri 3:1-8  kwa kila jambo kuna majira yake, na wakati wa kila kusudi chini ya mbingu; Wakati wa kuzaliwa, na wakati wa kufa; Wakati wa kupanda, na wakati wa kung'oa yaliyopandwa; Wakati wa kuua, na wakati wa kupoza; Wakati wa kubomoa, na wakati wa kujenga; Wakati wa kulia, na wakati wa kucheka; Wakati wa kuomboleza, na wakati wa kucheza; Wakati wa kutupa mawe, na wakati wa kukusanya mawe; Wakati wa kukumbatia, na wakati wa kutokumbatia; Wakati wa kutafuta, na wakati wa kupoteza; Wakati wa kuweka, na wakati wa kutupa; Wakati wa kurarua, na wakati wa kushona; Wakati wa kunyamaza, na wakati wa kunena;Wakati wa kupenda, na wakati wa kuchukia; Wakati wa vita, na wakati wa amani.



Katika mistari hiyo tunaona Biblia ikielezea vitu vingi ambavyo Mungu ameviumba na kuviweka chini ya mbingu LAKINI vyote vimewekwa katika WAKATI (TIME) yake ndani ya kusudi maalumu la Mungu. Maana yake ni kwamba kila kitu ambacho Mungu amekiweka chini ya mbingu kipo/kimefungwa ndani ya muda/wakati wake maalumu na haiwezekani kukatokea muingiliano, kwani wakati ndio UFUNGUO au ndio unao amuru kitu gani kiwepo au kisiwepo. Huu ndio utaratibu wa Mungu aliouweka.



Kwanini Mungu ameweka utaratibu huo? Ipo siri ya Mungu na muda, Muda na Mungu ni marafiki tena wana mahusiano mazuri sana. Muda anaongoza maamuzi ya Mungu na Mungu anaongoza matumizi ya muda kwa kuiweka mipango yake ndani ya mtu au kuachilia majira Fulani katika mwaka na kumwagiza mwanadamu atekeleze hiyo mipango/majira ndani muda sahihi aliokusudia.



 Kwahiyo hata katika mwaka 2016, ipo mipango na yapo majira, na nyakati Mungu aliyoamuru Kuwepo na vyote hivyo vimefungwa katika muda ili viweze kutimia sawasawa na mpango wa Mungu, na Mwanadamu ndiyo amepewa hiyo mamlaka ya kufahamu na kuyatimiza yote lakini ndani ya wakati wa Mungu pekee. KWAHIYO Mwanadamu kamwe hana wakati wakwake peke yake bali kila jambo ndani ya wakati (Time) pamoja na Mungu aliye hai. Ms. 11 Kila kitu amekifanya kizuri kwa wakati wake; tena ameiweka hiyo milele ndani ya mioyo yao…’



Unaweza jiuliza KUSUDI la Mungu hapa ni nini? Ukiendelea Ms. 14 utapata jibu ‘Najua ya kwamba kila kazi aifanyayo Mungu itadumu milele; haiwezekani kuizidisha kitu, wala kuipunguza kitu; nayo Mungu ameifanya ili watu wamche Yeye’. Mungu ameyafanya hayo yote ili tu Mwanadamu amche yeye pekee na si vinginevyo.



Je tunawezaje kuyafahamu majira na nyakati Mungu alizoamuru kwa Mwaka 2016 ili tuweze kuishi sawa sawa na Mungu anavyotaka? Kama anayosema katika neno lake Zaburi 32:8Nitakufundisha na kukuonyesha njia utakayoiendea; Nitakushauri, jicho langu likikutazama’.



Ukisoma 1 Wakorinto 2:9 -10 ‘Lakini, kama ilivyoandikwa, mambo ambayo jicho halikuyaona wala sikio halikuyasikia, (wala hayakuingia katika moyo wa mwanadamu,) mambo ambayo Mungu aliwaandalia wampendao. Lakini Mungu ametufunulia sisi kwa Roho. Maana Roho huchungza yote, hata mafumbo ya Mungu’. Kwahiyo njia peke ni kumuliza Roho wa Mungu peke yake ndiye aliye na uwezo wa kutufunulia yote ili tuweze kujua.



Maelezo ya Mtume Paulo yanatufanya tujue kwamba katika mwaka 2016 kuna mambo mazuri ambayo Mungu amewandalia watoto wake na kwa njia ya Roho Mtakatifu tunao uwezo wa kutambua nini kinakuja kwenye kila eneo la maisha yetu hata kabla hatujauingia mwaka husika.



Tambua kwamba katika mwaka 2016 kila ufalme yaani ufalme wa Mungu (Nuru) na ule wa Shetani (Giza) kuna mambo umeyaandaa/kusudia kwa ajili yako kifamilia, ndoa, kazi, huduma, masomo, biashara, kanisa lako, taifa lako n.k. LAKINI Ni dhahiri kwamba Mungu amekusudia mema kwa ajili yako kama Neno lake linavyosema katika Yeremia 29:11a Maana nayajua mawazo ninayowawazia ninyi, asema Bwana, ni mawazo ya amani wala si ya mabaya, kuwapa ninyi tumaini siku zenu za mwisho’. Shetani kama ilivyo asili yake amekusudia mabaya juu yako.



Je, unakumbuka matukio ya mwaka 2015 kwako binafsi, kifamilia, kikanisa, Kitaifa na dunia kwa ujumla?   Je, unajua katika ulimwengu wa roho matukio hayo yameacha au kuzaa kitu gani? Naam chukua muda yatafakari kibiblia na kisha jiulize laiti ungejua kabla hujaingia mwaka 2015, kwamba hayo yaliyotokea yatatokea ungechukua hatua gani? 

Kumbuka lolote unaloliona katika ulimwengu wa mwili linatokea ujue, lilishatokea kwenye ulimwengu wa roho kwanza. Naam kwenye ulimwengu wa roho, ndipo una fursa ya kuona mambo yanayoenda kutokea duniani, kabla hayajatokea. Ni katika ulimwengu wa roho ndipo unaweza:-

(I)           kupambana ili kuhaikisha jambo jema ambalo Mungu amekusudia linatimia. Pia,

(II)         kuzuia lolote baya ambalo Shetani amekusudia juu yako, famila n.k katika ulimwengu huu wa mwili lisitokee. 

Kutokana na umuhimu wa kuwa na ufahamu wa nini kinakuja siku za usoni yaani mwaka 2016, imenilazimu kuandaa ujumbe huu ili ukusaidie kujua angalau kwa sehemu 2016 ni mwaka wa namna gani na ndani yake kuna nini? Hii itakusaidia sana kujua ufanye nini ili kufanya maandalizi mazuri tushirikiana na kuyakabili yale yanayokuja. 

Kila mwaka, ndani yake kuna mambo ambayo ni LAZIMA yafanyike au yatime kulingana na nyakati ambazo zimeamriwa juu yako na Taifa pia (Rejea Mhubiri 3:1). Kwa mwaka 2016 yafuatayo ni baadhi ya mambo muhimu ambayo ambayo Roho wa Mungu amenifunulia tujue Mungu alivyokusudia kwa ajili yetu watoto wake:-



1.   Ni mwaka wa kuwekeza na kukusanya (kuweka akiba) Zaidi kwa kuwa kuna mabadiliko ya kiuchumi yanakuja.

Biblia katika kitabu cha Mwanzo 41:35-36 inasema ‘Na wakusanye chakula chote cha miaka hii myema ijayo, wakaweke akiba ya nafaka mikononi mwa Farao wakakilinde kuwa chakula katika miji. Na hicho chakula kitakuwa akiba ya nchi kwa ajili ya miaka hiyo saba ya njaa, itakayokuwa katika nchi ya Misri, nchi isiharibike kwa njaa’. Maelezo haya ya Yusufu ni matokeo ya fasili ya ndoto ya Farao kiongozi wa Misri.  Baada ya kupata tafsiri yake ilibidi Taifa la Misri watumie miaka saba ya mwanzo kukusanya chakula kwa ajili ya miaka mingine saba ya njaa iliyokuwa inakuja mbele yao.

Usiogope, binafsi, sikuelezi kwamba pia katika Taifa letu kuna miaka saba ya njaa inakuja La hasha!. Hata hivyo jambo ambalo nina uhakika linaenda kutokea ni mabadiliko muhimu ya kiuchumi si tu wa nchi yetu bali Dunia nzima kuanzia mwaka 2016 ambayo yataleta athari si tu kwa uchumi wa Taifa bali mpaka mtu mmoja mmoja. Mabadiliko hayo kama yatakukuta haujajipanga vizuri kwa kuwekeza katika sekta na nyanja mbalimbali za kiuchumi itakugharimu sana. Naam! mabadiliko haya yaliyoanza kwa sehemu mwaka 2015 na kuendele kwa kasi mwaka 2016 yatakuwa mazuri kwa wale waliojiandaa kuyakabili, na si vinginevyo (asomaye na afahamu).

Hivyo nakushauri mpedwa katika mwaka 2016 fanya kila jitihada kuwekeza fedha, muda na nguvu katika kuimarisha biashara zako, kazi zako, mifugo na zaidi kuongeza vyanzo vingine vya mapato. Naam tia bidii sana katika kila utakalofanya kwa mwaka 2016 ukimtanguliza Mungu. Katika Kumbukumbu la Torati 8:18 imeandikwa ‘Bali utamkumbuka BWANA, Mungu wako, mana ndiye akupaye nguvu za kupata utajiri; ili alifanye imara agano lake hata hivi leo’. Hivyo tarajia kupata mawazo mapya na yaliyo bora zaidi yatakayokusaidia kupata utajiri katika mwaka 2016 kutoka kwa BWANA Yesu, naam tegemea akili zako kutakaswa na hivyo kuwa na mawazo ya ubunifu na ufumbuzi zaidi katika mwaka 2016 yatakayopelekea kukubalika na kuinuliwa kwako zaidi kushinda wengine kazini kwako.

Kama una mradi wako yaani duka au biashara yoyote usiridhike nayo ipanue zaidi au kuongeza nyingine mpya, naam chukua hata mkopo upanue wigo wako ni muhimu sana kwa kule tunakokwenda.  Sambamba na hayo anza sasa kuweka akiba ya fedha (endapo hufanyi hivyo) ambayo ni muhimu sana kwa huko tunakokwenda, ni muhimu sana ukaweka akiba yako kwenye mifuko mbalimbali ya kutunza akiba ya kijamii au ukawa na akaunti maalum kwa ajili ya akiba.

N: B KUMBUKA Tunza na zingatia sana Muda katika kila jambo, usipoteze muda kwenye mambo yasiyo ya msingi kama kuangalia Tv, Sinema masaa 24. Tunza muda na tumia vizuri muda wako, muda ni mali kwani muda ukipita hauridi tena na mafanikio yako yote yamefungwa katika Muda kama Biblia inavyosema. Kufanikiwa au kutokufanikiwa kwako kunategemea kwa kiasi gani umetumia muda wako vizuri.

2.   Ni mwaka wa kucheka kwa kuwa BWANA anaenda kuwafurahisha watu wake wale wanaomtegemea.

Ayubu 42:10 ‘Kisha BWANA akageuza uteka wa Ayubu, hapo alipowaombea rafiki zake; BWANA naye akampa Ayubu mara mbili kuliko hayo aliyokuwa nayo kwanza’.  Ukisoma kitabu cha Ayubu sura 1-2 utaona habari za Ayubu na jinsi Shetani alivyoharibu maisha yake kwa ujumla. Kilikuwa ni kipindi kigumu sana kwa Ayubu, hata hivyo hizo ndio nyakati zilizokuwa zimeruhusiwa juu yake. Maandiko yanaonyesha kuwa baada ya Ayubu kusimama vizuri na Mungu wake katika kipindi hicho kigumu, BWANA alimrejeshea Ayubu maradufu kila kilichokuwa kimeharibiwa na Shetani yaani furaha, afya, watoto na mali zake zote. 

Vivyo hivyo katika mwaka 2016 BWANA amekusudia kutimiza ahadi nyingi kwa watu wake wanaomtegema, kile kilichoharibiwa kitarejeshwa, haki zilizopotea zinaenda kurejeshwa, BWANA anaenda kurejesha uzima katika mwili wako nk. Kama ni familia yako, ndoa yako, huduma yako, kazi yako nk Shetani aliharibu na kuteka, uwe na uhakika BWANA Yesu anaenda kuponya na kurejesha uhai tena.

3.   Ni mwaka wa amani utakaokupa fursa ya kujijenga na kutimiza mapenzi ya Mungu kwa mwaka husika

1 Waflme 5: 3-5, Umemjua Daudi baba yangu jinsi asivyoweza kujenga nyumba kwa jina la Bwana, Mungu wake, kwa sababu ya vita vilivyomzunguka pande zote, hata Bwana alipowatia watu chini ya nyayo zake. Ila leo Bwana, Mungu wangu, amenipa amani kila upande; hakuna adui, wala tukio baya. Nami, tazama, nakusudia kujenga nyumba kwa jina la Bwana, Mungu wangu, kama Bwana alivyomwambia Daudi baba yangu, akisema, Mwana wako, nitakayemweka katika kiti chake cha enzi mahali pako, ndiye atakayeijenga nyumba kwa jina langu’.

Maneno haya yalisemwa na Sulemani baada ya kutawazwa kuwa mfalme kufuatia kifo cha baba yake Daudi. Ukisoma Biblia yako vema utagundua kwamba utawala wa Daudi ulikuwa na vita sana, na kwa sababu ya vita na damu nyingi iliyomwagika katika kipindi chake BWANA alimzuia Daudi asimjengee Hakalu. Hekalu lilijengwa kipindi cha mwanawe Sulemani.  Naam ili Sulemani aweze kujenga hekalu vema, BWANA akampa amani pande zote na kazuia baya lolote lisitokee.

Vivyo hivyo Mungu anaenda kuleta amani juu yako kila upande katika mwaka 2016 ili utumie fursa si kujijenga wewe binafsi bali kuujenga ufalme wake kwa mwaka husika kwa kutimiza yale anayotaka kufanya juu ya Taifa, Kanisa, familia, ndoa kupitia wewe. Hii haina maana kwamba Shetani hajapanga mabaya, tunafahamu kwamba yeye ni baba wa uongo, lengo lake kubwa ni kuiba, kuchinja na kuharibu.

Amini kwamba kabla Shetani hajatekeleza mipango yake BWANA ataizuia na kupigana kwa ajili yako ili kutoathiri kusudi lake kupitia wewe kama alivyofanya  siku za Mfalme Yehoshafati, aliposema “Hamtahitaji kupigana vita, jipangeni, simameni, mkauone wokovu wa BWANA ulio pamoja nanyi, enyi Yuda na Yerusalemu; msiogope wala msifadhaike; kesho tokeni juu yao, kwakua BWANA yu pamoja nanyi” (2Nyakati 20:125), naam hivi ndivyo BWANA anavyoenda kuwashindia watoto wake katika mwaka huu.

Hakika huu ni mwaka wako wa kujijenga kiuchumi, kibiashara, kifamilia, kikazi, kwa kilimo nk. Ndio BWANA anaenda kuruhusu majira mazuri juu ya nchi yetu na kuzuia kila uharibifu uliokusudiwa juu yetu. 

Kwa uchache na kadri Mungu alivyonifunulia siri hizi kwa habari ya mambo yanayokuja siku za usoni katika mwaka huu. Hayo ni mawazo ya Mungu kuhusu watu wake na kanisa kwa ujumla kwa mwaka 2016, na daima mawazo ya Mungu ni mawazo ya amani (Yeremia 29:11), haya ambayo amesema nawe kuhusu 2016 unapaswa kuhakikisha unayafuatilia mpaka yatimie juu yako na Taifa letu pia. Namna mojawapo ya kuhakikisha haya yanatimia ni kujiwekea malengo ambayo yatatoa fursa kwa imani yako kuwa na mahali pa rejea kadri unavyozidi kuukabili mwaka 2016. 

TAMBAUA; Biblia katika kitabu cha Waebrania 12:1 inasema ‘Basi imani ni kuwa na hakika ya mambo yatarajiwayo, ni bayana ya mambo yasiyoonekana’. Ni muhimu sana ukajiwekea utaratibu wa kuwa na malengo ili yakusaidie kujua hatua zilizoko mbele yako ambazo unapaswa kuzifikia. Naam si suala tu la kuweka malengo bali kuyaweka kwa kuzingatia kile kinachokuja katika mwaka 2016. Natambua liko kundi kubwa la watu ambao wanaweza kuwa walishaweka malengo yao hata hivyo bado una fursa ya kuyaboresha (adjust) kwa kuzingatia hiki ambacho umejifunza katika ujumbe huu.

Malengo yako yatakusaidia kujua hatua unazopiga endapo zinakufikisha kule ambako Mungu anataka ufike katika mwaka 2016.

Maandiko yanasema katika Isaya 60: 1 ‘Ondoka, uangaze; kwa kuwa nuru yako imekuja, Na utukufu wa BWANA umekuzukia’. Ukisoma msatri huu katika toleo la kiingereza la ESV unasema ‘Arise, shine, for your light has come, and the glory of the LORD has risen upon you’ (Isaiah 60:1). Neno ondoka ambalo kwa kiingereza ni ‘arise’ kwa fasiri ya kamusi ya kiebrania na kigiriki lina maana ya timiliza (accomplish), maliza (complete), fikia lengo (achieve) au fanikiwa (succeed). 
Kwa tafsiri hii ina maana kwamba, Mungu anayo mambo (mipango) ambayo katika mwaka 2016 anataka ufanikiwe katika kuyatimiliza na kukamilisha.

Naam na ili uweze kuyafikia yeye anaenda kukulinda kwa kufanyika ukuta wa moto utakaokuzunguka pande zote sawasawa na Zekaria 2:5 ‘Kwa maana mimi, asema BWANA, nitakuwa ukuta wa moto kuuzunguka pande zote, nami nitakuwa huo utukufu ndani yake’.  

Zaidi katika Mitahli 8:17 imeandikwa ‘Nawapenda wale wanipendao, Na wale wanitafutao kwa bidii wataniona’. Ni imani yangu kama:-

(i)           Ukidumu katika kumpenda Mungu kwa kuzishika amri zake

(ii)          Ukadumu katika kumtafuta

(iii)        Ukasimama vema kwenye nafasi yako kama mlinzi basi uwe na uhakika haya ambayo leo Mungu ameyafunua kwako kuhusu mwaka 2016 yatakuwa dhahiri na mwaka huu utakuwa wa baraka za pekee kuliko yote iliyotangulia. 

Mungu akubariki kwa kusoma na kuelewa maneno yake katika msisitizo huu, Biblia inasema ‘wakati wasemapo kuna amani ndipo uharibifu uwajiapo’.  Hivyo ni muhimu sana ukazingatia kumpenda Mungu na kuwa makini na maisha yako kwa kila hatua kwa mwaka huu mpya 2016. Amen!!

*************************************************************************************
Share:

USCF-SJUT NEWS

Designed by Joel Elphas @ 2015. Powered by Blogger.

Recent Posts