Monday, August 10, 2015



MAOMBI YENYE UWEZO WA KUPASUA ANGA

NA: DR. GODWIN GUNEWE

MAOMBI NA JINSI YANAVYOZUILIWA
NA WAKUU WA ANGA

      Moja kati ya silaha kuu, ambayo inamwezesha mtoto wa Mungu kushinda vita dhidi ya majeshi ya giza, ni maombi. Hofu kubwa kwa shetani na majeshi yake, ni pale anapokuwapo mtu mwenye nguvu ya kuzalisha maombi yaletayo moto, na hatimaye kuleta athari kubwa sana katika ufalme wa giza.
      Ni ukweli usiopingika kwamba, watoto wa Mungu katika kanisa la leo, wanakosa ufahamu sahihi wa namna gani wanaweza kuzalisha maombi yanayoweza kutishia usalama wa shetani na majeshi yake, kama vile ilivyokuwa katika kanisa la kwanza. Wengi wanaomba, lakini hawapokei majibu ya maombi yao, kwa kuwa wanaomba vibaya (Yakobo 4:3). Wengi wanaomba, lakini hawaombi kwa imani, hivyo kusababisha maombi yao kutokuwa na nguvu ya kupenya katika anga.
      Ni kwa sababu hii basi, tutachukua muda mrefu, katika kuchimbua siri kuu iliyo katika maombi, na kufahamu kwa mapana na marefu, sababu inayomfanya shetani kuogopa sana maombi.
      Kabla hatujaingia kwa undani sana, ni vema kwanza tukifahamu kwa nini tunatakiwa kufanya maombi. Hatuwezi kusababisha maombi yanayoweza kupasua anga kama hatujui kwa kina, kwa nini tunapaswa kuomba. Zifuatazo ni sababu kuu zinazopelekea watoto wa Mungu kufanya maombi;

1.      Maombi ni uchaguzi wa Mungu wa kuzuia nguvu na kazi za shetani (Mathayo 6:13; Waefeso 6:12, 18).

2.      Maombi hutupatia msaada wa Mungu katika kila hali (Zaburi 3:3-4; Zaburi 34:4, 6).

3.      Maombi yanaondoa vikwazo au vipingamizi vyote (Marko 11:23-24).

4.      Maombi ni njia ya kupata amani tunapokabiliwa na hali ya kutisha na kukatisha tama (Wafilipi 4:4-7).

5.      Maombi hugeuza mioyo na tabia ya watu wengine (Nehemia 2:4-8).

6.      Maombi ni njia ya uponyaji wa kimwili na kiroho (Yakobo 5:14-15).

7.      Maombi huleta msukumo wa kiroho na kumtia mtu nguvu wakati mtu fulani anapokabiliwa na hali ya kushindwa (Wakolosai 1:9-11).

     Kwa ujumla, maombi ni njia ya kuita nguvu ya Kimungu ili ikatende kazi katika eneo kusudiwa.

SABABU KUU ZINAZOPELEKEA KUZUILIWA AU KUCHELEWESHWA KWA MAJIBU YA MAOMBI YETU
      Asilimia kubwa ya watoto wa Mungu, katika kanisa la leo, wamekata tamaa kabisa katika kuomba. Na sababu kuu ni kucheleweshwa au kutopokea kabisa kwa majibu ya maombi yao. Zipo sababu kuu nne zinazopelekea majibu ya maombi kucheleweshwa au kuzuiliwa kabisa, ingawa katika kitabu hiki nitaizungumzia kwa undani sana sababu ya pili, yaani ushindani wa wakuu wa giza katika anga (Danieli 10:12-13).

1. DHAMBI/ UOVU (Isaya 59:2; Mithali 28:9)
     Dhambi ni kikwazo kikubwa kinachosababisha muombaji asipokee majibu ya maombi yake. Katika Isaya 59:2 tunasoma, “Lakini maovu yenu yamewafarikisha ninyi na Mungu wenu, na dhambi zenu zimeuficha uso wake msiuone, hata hataki kusikia.” Mtu yeyote asiyekwenda na maagizo yote ya Mungu, huyo ni mtenda dhambi, na maombi yake hayawezi kumfikia Mungu, maana maombi yake ni chukizo mbele za Mungu, kama maandiko yanavyotuambia katika Mithali 28:9, “Yeye aligeuzaye sikio lake asiisikie sheria, hata sala yake ni chukizo.”

2. USHINDANI WA WAKUU WA GIZA (Danieli 10:12-13)
     Wakuu wa giza katika anga, huchukua nafasi kubwa sana katika kuzuia au kuchelewesha majibu ya maombi yetu. Yapo majeshi ya ufalme wa giza maelfu na maelfu katika kila anga la eneo fulani, na moja ya kazi yao ni kuzuia maombi ya watoto wa Mungu. Zama za Danieli mkuu wa anga aliye katika eneo la Uajemi, aliweza kuchelewesha majibu ya Danieli (Danieli 10:12-13).

3. KUPIMWA JINSI TUNAVYOMTUMAINIA MUNGU PEKEE (Zaburi 78:7; 26:1-2)
     Sababu hii ya kucheleweshwa kwa majibu ya maombi yetu, hutokana na Mungu mwenyewe na siyo majeshi ya giza. Mungu huchelewesha majibu ya maombi yetu yeye mwenyewe, ili kupima imani yetu na kuona namna gani tunaweza kumtumainia yeye kwa asilima zote.


4. KULINDWA KWA MAISHA YETU YA KIROHO (2 Wakorintho 12:7-9).
     Mungu anatujua vema hali zetu za kiroho tulizo nazo, na anajua nani akipewa hiki anamwacha Mungu, na nani akipata hiki ataendelea kuwa na Mungu. Hivyo katika kulinda usalama wetu wa kiroho, kuna vitu ambavyo tukimwomba, huwa hatupi kwa wakati huo au kutotupa kabisa, kwa kuwa anajua tukipata kitu fulani tutamwacha Mungu. Hufanya hivi, kwa upendo wake mkuu kwetu ili tusije kuingia jehanamu ya moto. Kuna watu wanakuwa wanyenyekevu mbele za Mungu wakiwa hawana fedha, na mara wakipata fedha wanachanganyikiwa na kumwacha Mungu na hatimaye kurudi dhambini.

MUONEKANO WA MAOMBI KATIKA ULIMWENGU
WA ROHO
      Watoto wa Mungu wanapoomba duniani, maombi yao, katika ulimwengu wa roho huonekana kwa mfumo wa moshi. Katika kitabu cha Ufunuo 8:4Biblia inasema, “Na moshi wa ule uvumba ukapanda mbele za Mungu, pamoja na maombi ya watakatifu, kutoka mkononi mwa malaika.” Athari za maombi ya Wakristo dhidi ya ufalme wa shetani, zinatofautiana kati ya muombaji na muombaji, kulingana na sifa alizonazo muombaji huyo, zinazomwezesha kusababisha maombi yenye nguvu, ya kutawanya ukungu wa kipepo katika anga.
      Sababisho la uharibifu katika ufalme wa anga, linategemea sana na uhusiano wa muombaji na Roho Mtakatifu, kiwango cha imani alicho nacho, pia utakatifu alio nao, kadhalika maarifa aliyo nayo katika Neno la Mungu, pamoja na maarifa ya kupeleka maombi hayo.
     Vitu hivyo, ndiyo vinavyofanya muombaji azalishe aina fulani ya maombi katika anga. Kimsingi, maombi ya Wakristo katika anga, huonekana katika mfumo wa namna tatu;

A.  MAOMBI YALIYO DHAIFU SANA
      Maombi haya, huitwa dhaifu sana, kwa sababu hayana uwezo wa kuwafikia au kuleta Athari kwa majeshi ya giza yanayozuia maombi ya Wakristo katika anga. Maombi haya huwa katika mfumo wa moshi usio na muelekeo mmoja, huzagaa katika anga na hatimaye kupotea katika hewa bila kusababisha madhara yoyote katika ukuta wa kipepo, yanakuwa hayana nguvu ya kupenya utando wa kipepo. Maombi ya namna hii hutoka kwa watu wanaoomba huku wakiwa na dhambi (Isaya 59:2). Na mara nyingi, wakuu wa anga, huwa hawashughuliki na maombi ya namna hii, kwa kuwa hayana madhara yoyote kwao.

B.   MAOMBI YALIYO VUGUVUGU.
     Maombi ya namna hii, huonekana kama moshi unaopanda juu na hata kufika kwenye ukungu au utando wa kipepo, lakini moshi huu, unakuwa hauna uwezo wa kuyeyusha utando huo ili kupenya na kufika mbinguni, kwa kuwa ni moshi usio na moto. Maombi haya yanakuwa hayazalishi moto wa kuyeyusha utando huo mzito ulio na mfano wa kama nta. Huu utando ndiyo kizuizi kikubwa.
     Hivyo ni wazi kabisa, maombi ya namna hii huwa hayawezi kupasua anga, ingawa yanaweza kuleta shida kwa majeshi ya wakuu wa anga. Haya ni maombi ya watu walio watakatifu, lakini mioyoni mwao hawana imani na kile wanachoomba, kwa kuwa wanakuwa na mashaka fulani. Katika kitabu chaWaebrania 10:38 Biblia inasema, “Lakini mwenye haki wangu ataishi kwa imani; naye akisita-sita, roho yangu haina furaha naye.”

C.   MAOMBI YALIYO NA MOTO
     Aina hii ya tatu ya maombi, huonekana kama moshi ambao umejaa moto. Na moshi huu unapopanda juu, ni wa moto sana kiasi kwamba, huyeyusha utando wa kipepo katika anga na kuyeyuka kama nta, na kupasua anga lililozuiliwa na wakuu wa giza, na hatimaye hupenya na kufika mbinguni.
     Mara zote, wakati Wakristo walio wakamilifu na wenye imani, wanapoanza kuomba, maombi yao huwa kama ya aina ya kwanza, lakini wanapoendelea kuomba, maombi yao hubadilika na kuwa kama ya aina ya pili. Na mara wakiendelea kuomba, ghafla huanza kulipuka na kugeuka kuwa moto. Na maombi yao huwa na nguvu sana, na hata kusababisha kupasua kizuizi kilichowekwa na wakuu wa giza, na hatimaye maombi hayo kufika kwa Mungu.

JINSI WAKUU WA GIZA WANAVYOZUIA MAOMBI
YA WATOTO WA MUNGU
Watoto wa Mungu wanapoomba, maombi yao huweza kuzuiliwa kwa namna mbili;
1. Maombi huzuiliwa wakati yanakwenda mbinguni ili yasimfikie Mungu mbinguni.
     Aina hii ya kizuizi hufanywa na majeshi ya giza yaliyo katika anga kwa ushirikiano wa majeshi ya giza yaliyo katika ardhi. Mtoto wa Mungu anapoomba, maombi huanza kupaa kwa mfumo wa moshi, na kwenda juu mbinguni, hivyo majeshi ya wakuu wa giza wanapoyaona maombi hayo, hufanya jitihada kuyazuia ili yasifike mbingu ya tatu yaani mbinguni alipo Mungu (2 Wakorintho 12:2).
     Ni vema ifahamike kwamba, katika anga yaani mbingu ya kwanza na ya pili, kuna majeshi ya wakuu wa giza, ambayo yamejipanga kikamilifu ili kupambana na watoto wa Mungu, ikiwemo kuzuia maombi yao yasimfikie Mungu. Katika kitabu cha Waefeso 6:12 Biblia inasema, “Kwa maana kushindana kwetu sisi si juu ya damu na nyama; bali ni juu ya falme na mamlaka, juu ya wakuu wa giza hili, juu ya majeshi ya pepo wabaya katika ulimwengu wa roho.” Katika 1 Petro 3:7 tunasoma, “………kusudi kuomba kwenu kusizuiliwe.”

2. Majibu ya maombi kutoka kwa Mungu mbinguni huzuiliwa ili yasimfikie muombaji duniani.
     Aina hii ya kizuizi hufanywa na majeshi ya wakuu wa giza yaliyo katika anga pia kwa ushirikiano na majeshi yaliyo katika ardhi na maji. Muombaji anapofanikiwa kufanya maombi ya nguvu na hatimaye maombi yake yakapasua anga na kumfikia Mungu, majeshi ya wakuu wa giza, huchukua nafasi tena kuzuia mara ya pili ili majibu yaliyotoka kwa Mungu yasimfikie muombaji aliye duniani. Katika kitabu cha Danieli 10:12-13 Biblia inasema, “Ndipo akaniambia, usiogope, Danieli; kwa maana tangu siku ile ya kwanza ulipotia moyo wako ufahamu, na kujinyenyekeza mbele za Mungu wako, maneno yako yalisikiwa; name nimekuja kwa ajili ya maneno yako. Lakini mkuu wa ufalme wa uajemi alinipinga siku ishirini na moja; bali tazama, huyo, Mikaeli, mmoja wa hao wakuu wa mbele, akaja kunisaidia; nami nikamwacha huko pamoja na wafalme wa Uajemi.” Kwa kawaida maombi yanapojibiwa na Mungu mbinguni, maombi hayo huletwa duniani kwa mkono wa malaika kwa mfumo wa kifurushi, maana malaika ni roho watumikao kwetu (Waebrania 1:14).
     Katika aina hii ya pili ya kuzuiliwa kwa maombi ya watoto wa Mungu, vita huwa kali sana kuliko ile ya kwanza. Majeshi ya wakuu wa giza hupambana na malaika aliyebeba kifurushi cha majibu ya maombi ya muombaji, kwa lengo la kupora kile kilichobebwa, ili kisimfikie mlengwa. Katika eneo hili, ushindi wa malaika huyo katika vita hiyo, hutegemea sana na hali ya kiroho, aliyo nayo muombaji husika. Kama mtu anayeomba anazo silaha zote za Mungu zinazotajwa katika kitabu cha Waefeso 6:13-18, ni wazi kabisa malaika yule aliyebeba majibu ya maombi ya muombaji huyo, atashinda vita katika anga, na kumfikishia muombaji majibu yake.
     Kama muombaji anakuwa hajavaa silaha zote za Mungu, na malaika atakayetumwa kuleta majibu ya maombi, anakuwa hana hizo silaha, kama alivyo muombaji. Hiyo humfanya malaika yule, kuporwa majibu ya muombaji husika. Silaha za kiroho hazitulindi katika ulimwengu wa kimwili, bali zinatulinda katika ulimwengu wa kiroho.
    Malaika anaponyang’anywa majibu ya maombi na majeshi ya giza, siyo kwamba malaika huyo anakuwa ameshindwa vita, la hasha; anayekuwa ameshindwa vita ni muombaji na wala siyo malaika wala Mungu.
    Kwa kawaida majeshi ya giza hata yakikusanyika yote, hayana uwezo wa kumshinda malaika wa Mungu mmoja. Kinachofanyika ni kwamba, uaminifu wa muombaji kwa Mungu, ndiyo unaomfanya Mungu ahakikishe usalama wa kile anachomletea; lakini pia, uzembe wa kiroho wa muombaji, ndiyo unaomfanya Mungu kuruhusu majeshi ya giza yatimize makusudi yao dhidi ya majibu ya muombaji husika.
     Ni sawa tu na Mkristo aliyemwamini Bwana Yesu, anapoenda kwenye mateso ya jehanamu ya moto; siyo kwamba, Bwana Yesu kashindwa, bali aliyeshindwa ni Mkristo mwenyewe. Mungu ameweka kanuni na miongozo ya kuifuata ili mtu afike mbinguni, kwa hiyo anaposhindwa kufuata miongozo hiyo ni wazi hataiona mbingu. Kadhalika, katika maombi, Mungu ameweka kanuni zitakazomwezesha mtoto wa Mungu kupokea majibu ya maombi yake, hivyo mtu anapokosa kuzifuata kanuni hizo, ni wazi atakosa kile ambacho amekiomba.
      Majeshi ya wakuu wa giza yanafahamu wazi kwamba, muombaji anapokuwa na silaha zote za Mungu, na malaika atakaye tumwa kuleta majibu ya maombi huwa na silaha zote za Mungu. Wakishagundua malaika huyo ana silaha zote za Mungu, huogopa kumshambulia; na hata kama wakimshambulia, hawataweza kushinda, hivyo malaika huyo hufikisha majibu ya maombi kwa muombaji.
     Malaika anapotumwa kutoka mbinguni kuleta majibu ya muombaji, majeshi ya wakuu wa giza, watamchunguza malaika huyo ni silaha gani ambayo hana, na wanapogundua hana silaha fulani, humshambulia katika maeneo hayo. Baada ya kumshambulia, humpora majibu ya maombi aliyobeba. Kimsingi, majeshi ya giza hayana uwezo wa kumharibu malaika huyo, bali wana uwezo wa kupora kile alichobeba. Na baada ya hapo yule malaika hurudi mbinguni, hivyo muombaji anakuwa amekosa kupokea kile alichoomba na pia kuwa chini ya mamlaka ya nguvu za giza.
    Unaweza kujiuliza ni kwanini inakuwa hivi? Sababu kuu ni kwamba, Mungu mwenyewe ameruhusu iwe hivyo; hiyo ni kanuni katika ulimwengu wa roho. Ni lazima watu wafahamu kwamba, kila kitu katika ulimwengu wa kiroho kinaenda kwa kanuni. Na Mungu wetu anaheshimu sana kanuni alizoweka.
  
MUUNDO WA FALME ZA WAKUU WA ANGA
NA UTENDA KAZI WAO

     Ufalme wa giza katika anga, ngazi ya kimataifa, umegawanyika sehemu kuu nne; sehemu ya kwanza ya ufalme wa anga katika falme na mamlaka za wakuu wa giza inaitwa ufalme wa nyota. Sehemu hii ina kanda 900,000,000 na pepo linalotawala kila kanda huitwa Deva, na mkuu wao katika ufalme huu niSagna.
     Sehemu ya pili ya ufalme wa anga una miungu 33,000,000. Pepo linalotawala hapo huitwa Bavara. Sehemu ya tatu ya ufalme wa anga huitwaUzura, ufalme huu hutawaliwa na Sat Kumara.
     Na ufalme wa nne wa anga huitwa Kalami, ufalme huu ndiyo makao makuu ya falme za giza, maana ndipo alipo mkuu wao, kiongozi mkuu katika eneo hili ni shetani mwenyewe.
    Wakuu wa anga, wamegawanyika katika ngazi mbalimbali; wapo wakuu wa anga wa mtaa/kijiji, wakuu wa anga wa wilaya au majimbo, wakuu wa anga wa mikoa, wakuu wa anga wa nchi, na wakuu wa anga wa kimataifa. Mgawanyo wa wakuu wa anga unategemeana na nchi na nchi, na kila ngazi kuna mkuu wao na majeshi yao.
   Hata hivyo kwa kawaida, inasemekana kwamba, kila mkuu wa anga wa mtaa/kijiji huwa na mabodigadi 99, na kila bodigadi huwa na watumishi 1000wa kumsaidia kazi bodigadi huyo. Na jumla ya idadi ya majeshi ya giza yanayohusika na ulinzi katika kila anga la mtaa au kijiji ni askari wa kipepo36,270,600. Uongozi huu wa ufalme wa anga katika mtaa, huakikisha kwamba maombi ya watoto wa Mungu hayamfikii Mungu. Na wakiona nguvu ya uombaji imepamba moto katika mtaa, hushirikiana na majeshi ya falme za giza katika ardhi na maji ili kuwadhoofisha waombaji hao.
    Nguvu ya wakuu wa anga na majeshi yao, hutofautiana kati ya mtaa na mtaa, wilaya na wilaya, mkoa na mkoa, nchi na nchi. Mkuu wa anga wa eneo fulani na majeshi yake anaweza kuwa na nguvu kubwa kuzidi eneo lingine. Na mara nyingi hii inatokana na asili ya eneo husika. Kwa mfano, eneo ambalo kuna asili ya uchawi, matambiko na mambo ya kitamaduni, katika eneo hili, mkuu wa anga na majeshi yake huwa na nguvu sana ya kuzuia maombi kuliko eneo lingine. Mtu anapofanya maombi katika eneo kama hilo, huwa ni ngumu sana kupata mpenyo wa kimaombi.
    Pia maeneo ambayo, kulikuwa au kuna utawala mkubwa wa dini nyingine kama uislamu n.k. mara nyingi anga la eneo hilo huwa zito sana kimaombi. Na ndiyo maana, muombaji anaweza kutililika vizuri katika maombi katika eneo fulani, lakini pindi akihamia eneo lingine nguvu ya kutililika kimaombi hupotea kabisa, na hii, husababishwa na uhodari wa majeshi ya giza katika eneo mpya aliloamia muombaji huyo.
     Uzito wa anga na upinzani katika maombi, pia hutegemea na unyeti wa eneo hilo kwa ufalme wa giza. Kwa mfano, kama eneo hilo ndiyo makao ya mkuu wa giza au ni lango la kuzimu, eneo hilo huwa na ulinzi mkubwa sana wa mapepo, hivyo kusababisha ugumu usio wa kawaida katika kuomba.
     Kadhalika, kiongozi wa ufalme za giza, anaweza akawa anapita katika anga la eneo fulani kwa kipindi fulani, ni wazi waombaji waliopo chini ya eneo hilo, watapata shida sana, kutokana na nguvu ya kipepo inayomlinda kiongozi huyo anayepita, lakini mara akishapita katika anga hilo, hali ya eneo hilo hurudi na kuwa kawaida.

UTENDA KAZI WA WAKUU WA ANGA DHIDI YA MAOMBI YA WATOTO WA MUNGU
      Laiti kama watoto wa Mungu wangefunuliwa na kuona upinzani uliopo katika ulimwengu wa roho, kamwe wasingeomba kilegevu kama ilivyo sasa. Watu wanachukulia maombi kama raha fulani.
     Maombi ni kazi zaidi hata ya kazi ya zege, maombi ni vita kali sana, kuizidi vita yoyote iliyowahi kupiganwa kimwili hapa duniani. Na ndiyo maana kiongozi mkuu wa wokovu wetu, Bwana wetu Yesu Kristo alitumia muda mwingi sana katika kuomba, aliomba usiku na mchana (Luka 6:12). Kuna wakati aliomba mpaka jasho la damu likatoka (Luka 22:44).
     Upinzani wa maombi ya watoto wa Mungu ni mkubwa sana, tofauti kabisa, na wanavyofikiria watu. Muombaji anapoomba, maombi yake huanza kupata upinzani katika ngazi ya mtaa. Na kama nilivyokwisha kufafanua hapo awali kwamba, mkuu wa anga wa mtaa, huwa na mabodigadi 99 wa kumsaidia kazi, na katika mabodigadi hao, kila mmoja ana walinzi 1000. Na katika mtaa, majeshi ya giza yanayotenda kazi ni 36,270,600. Jaribu kuwaza! Je ni muombaji gani legelege anaweza kufanikiwa katika upinzani wa namna hii? Ni kweli Mungu anatushindia, lakini, kuna sehemu na sisi ya kuchukua hatua kama watoto wa Mungu. Na ndiyo maana Bwana Yesu alitupa kielelezo kwa kufanya maombi yasiyo ya kawaida, Bwana Yesu alitumia muda mwingi sana katika kuomba.
     Kwa hiyo, muombaji anapofanikiwa kupenya kimaombi katika anga la mtaa au kijiji, maombi yake yanaweza kupata upinzani tena na mkuu wa anga wa wilaya na majeshi yake. Kama maombi hayo yatapata neema ya kupenya tena katika anga la wilaya, maombi ya muombaji yanaweza kupata upinzani tena kwa mkuu wa anga wa mkoa na majeshi yake. Na kama yakipata mpenyo katika anga la mkoa, maombi hayo yanaweza kupata upinzani katika anga la kimataifa.
    Katika anga la kimataifa kuna mapepo yaliyo na nguvu isiyo ya kawaida. Hivyo, ni maombi yenye moto wa Roho Mtakatifu, ndiyo yanayoweza kupasua anga na kumfikia Mungu mbinguni.
     Si hivyo tu, lakini maombi, yakifika mbinguni, Mungu huyatolea majibu. Baada ya kutolewa majibu, malaika hupewa majibu hayo, ili kupeleka duniani kwa muombaji husika. Katika hatua zote za kupeleka majibu, malaika pia hukutana na upinzani wa wakuu wa anga katika ngazi zote, ili majibu hayo, yasimfikie mtoto wa Mungu.
     Muombaji anaweza akawa na silaha zote za Mungu, pindi anapoomba, hivyo kusababisha maombi yake kufika mbinguni. Lakini, wakati akisubiri majibu, akiyumba kiroho na kupoteza baadhi ya silaha za Mungu, kama ngao ya imani n.k, ni wazi kabisa, majibu yake hayatamfikia. Sababu kuu ni kwamba, malaika atakayetumwa kuleta majibu, naye atakuwa hana ngao; hivyo kupelekea majeshi ya giza katika anga, kumvamia kirahisi na kupora majibu ya maombi.
     Ni kwa sababu hii basi, Bwana Yesu, katika kitabu cha Luka 21:36anasema, “Basi, kesheni ninyi kila wakati, mkiomba, ili mpate kuokoka katika hayo yote yatakayotokea, na kusimama mbele za mwana wa Adamu.” Katika Luka 18:1 Bwana Yesu anatuagiza, “Akawaambia mfano, ya kwamba imewapasa kumwomba Mungu siku zote, wala wasikate tamaa.” Katika Wakolosai 4:2 Biblia inasema, “Dumuni sana katika kuomba, mkikesha katika kuomba huku na shukrani.

JINSI YA KUFANYA ILI MAOMBI YETU
YAPATE KUPASUA ANGA
     Ili maombi yaweze kupasua anga na kumfikia Mungu, inategemea sana kiwango cha kiroho cha muombaji husika na maarifa sahihi katika kuomba. Siyo kila muombaji anaweza kupata mpenyo katika anga. Ebu jaribu kujiuliza kwamba, ni Wakristo wangapi katika nyakati za leo ambao wana hali ngumu sana ya kiuchumi, kiroho, kifamilia, kimahusiano n.k? Na ukichunguza kwa makini, ni dhahiri kabisa kwamba, Wakristo hao wanaomba kwa bidii sana. Swali lingine ni kwamba, kama wanaomba kikamilifu, kwa nini hawapokei majibu yao?

SIFA ZA MUOMBAJI MWENYE UWEZO
WA KUPASUA ANGA KIMAOMBI
    Zipo sifa nyingi sana, zitakazomwezesha muombaji kupata kibali cha kufanya maombi yake yasambaratishe upinzani wa wakuu wa anga, lakini zifuatazo, ni sifa kuu na za msingi sana, na sifa zote zimebebwa ndani ya sifa hizi;

1.   MUOMBAJI NI LAZIMA AWE MTAKATIFU ALIYEKAMILIKA.
     Ukamilifu wa muombaji, unamfanya shetani na majeshi yake kukosa sababu ya kumshitaki muombaji kwa lolote. Katika kitabu cha 1Petro 5:8 Biblia inasema, “Mwe na kiasi na kukesha; kwa kuwa mshitaki wenu Ibilisi, kama simba angurumaye, huzunguka-zunguka, akitafuta mtu ammeze.” Pia Ufunuo 12:10 Maandiko yanasema, “Nikasikia sauti kuu mbinguni, ikisema, sasa kumekuwa wokovu, na nguvu, na ufalme wa Mungu wetu, na mamlaka ya Kristo wake; kwa maana ametupwa chini mshitaki wa ndugu zetu, yeye awashitakiaye mbele za Mungu wetu, mchana na usiku.”
     Ni kwa sababu hii basi, Bwana Yesu anatutaka tuwe wakamilifu kama Baba yetu wa mbinguni alivyo mkamilifu; Mathayo 5:48, “Basi ninyi mtakuwa wakamilifu, kama Baba yenu wa mbinguni alivyo mkamilifu.” Katika Walawi 19:2 tunasoma, “Nena na mkutano wote wa wana wa Israeli, uwaambie, mtakuwa watakatifu; kwa kuwa mimi Bwana, Mungu wenu ni mtakatifu.” Katika 1 Petro 1:16tunasoma, “Kwa maana imeandikwa, mtakuwa watakatifu kwa kuwa mimi ni mtakatifu.” Waefeso 1:4, “Kama vile alivyotuchagua katika yeye kabla ya kuwekwa misingi ya ulimwengu, ili tuwe watakatifu, watu wasio na hatia mbele zake katika pendo.”
    Kwa ujumla, maombi ya mtakatifu, huwa ni manukano mbele za Mungu, hivyo, Baba yetu wa mbinguni, huakikisha, majibu ya maombi hayo yanamfikia muombaji husika kama ilivyokuwa kwa Danieli (Danieli 10:12-13). Maombi yanayoweza kupanda mbele za Mungu ni maombi ya mtu mtakatifu tu kama Neno la Mungu linavyosema katika kitabu cha Ufunuo 8:4, “Na moshi wa ule uvumba ukapanda mbele za Mungu, pamoja na maombi ya watakatifu, kutoka mkononi mwa malaika.

2.   MUOMBAJI NI LAZIMA AVAE SILAHA ZOTE ZA MUNGU.
    Kitabu cha Waefeso 6:11 Biblia inasema, “Vaeni silaha zote za Mungu, mpate kuweza kuzipinga hila za Shetani.” Kadhalika katikaWaefeso 6:13, Maandiko yanasema, “Kwa sababu hiyo twaeni silaha zote za Mungu, mpate kuweza kushindana siku ya uovu, na mkiisha kuyatimiza yote, kusimama.” Silaha hizo za Mungu ni kama ifuatavyo;

(i) Kujifunga Kweli (Waefeso 6:14)-
   Mtoto wa Mungu ni lazima akae na kujifunza kweli yote, amfuate Mungu katika kweli na siyo kufuata mapokeo ya wanadamu. Kweli ni maagizo yote ya Mungu (Yohana 17:17). Kweli ya Neno la Mungu, inamfanya muombaji awe mkamilifu mbele za Mungu. Wakristo katika kanisa la leo hawafundishwi kweli yote na wachungaji wao, na hii imepelekea kanisa la leo kupoa sana kimaombi.

(ii) Kuvaa Dirii ya haki (Waefeso 6:14)
   Mtoto wa Mungu ni lazima atembee katika haki, ukamilifu, utaua, unyoofu ili asipate kushitakiwa na mshitaki na hatimaye maombi yake kuzuiliwa (1Petro 5:8; Ufunuo 12:10).

(iii)  Kuwa na utayari kwa ajili ya Injili ya amani (Waefeso 6:15)-
   Maandiko katika 1 Wakorintho 9:16 yanasema, “Maana, ijapokuwa naihubiri Injili, sina la kujisifia; maana nimewekewa sharti; tena ole wangu nisipohubiri Injili.” Kutokuhubiri Injili, aidha kwa kualika, kushuhudia, kugawa tracts n.k. ni kufanya dhambi ya kutotimiza wajibu, hii inatufanya tuwe na hatia, na ni ole wetu tusipofanya hivyo. Nguvu ya Mungu katika maisha yetu ya kiroho, inadhihirishwa, pale tunapokuwa tayari na kuchukua hatua ya kuhubiri habari za Yesu, na amani ya Mungu, kwa watu wote.

(iv)  Kubeba ngao ya Imani (Waefeso 6:16).
   Imani kwa mtoto wa Mungu ni ngao ya kuweza kuizima mishare ya moto ya shetani. Ni lazima tufahamu kwamba pasipo Imani haiwezekani kumpendeza Mungu (Waebrania 11:6). Pia Mungu wetu anataka mwenye haki wake aishi kwa imani (Waebrania 10:38; Wagalatia 3:11). Tunalindwa na nguvu ya Mungu kwa imani (1 Petro 1:5). Imani yetu katika maombi ndiyo inayotufanya tupokee kile tunachokiomba.

(v)  Chapeo ya wokovu (Waefeso 6:17).
   Kuuishi wokovu ni jambo la msingi sana kwa watoto wa Mungu. Wokovu wetu ni wa thamani sana, kwa kuwa Mungu mwenyewe amegharamika kwa mateso kwa ajili ya kuwakomboa wanadamu (Waebrania 2:3). Nguvu yetu ya maombi, inasababishwa na jinsi tunavyoweza kuutunza wokovu tulioupokea.

(vi)  Upanga wa roho ambao ni Neno la Mungu (Waefeso 6:17).
   Kwa kawaida Shetani anamuogopa sana muombaji aliyejaa Neno la Mungu. Neno la Mungu ni zaidi ya upanga wowote ukatao kuwili, na pia ni nyundo, kadhalika Neno la Mungu ni moto (Waebrania 4:12; Yeremia 23:29).
    Muombaji anapoomba, kwa kulitaja Neno la Mungu yaani ahadi za Mungu, shetani na majeshi yake hutetemeka na kuogopa sana. Mungu analiangalia Neno lake apate kulitimiza (Yeremia 1:12, hivyo muombaji anapoomba kwa kulitaja Neno la Mungu yaani ahadi za Mungu, Mungu hushuka kupitia Neno lake na kufanya kile kilichoombwa.
     Muombaji asiyejaa Neno la Mungu, maombi yake ni dhaifu, na ni rahisi maombi yake kupingwa na wakuu wa anga. Katika kitabu chaYohana 15:7 Biblia inasema, “Ninyi mkikaa ndani yangu, namaneno yangu yakikaa ndani yenu, ombeni mtakalo lote nanyi mtatendewa.”

3.   MUOMBAJI NI LAZIMA AWE NA UHUSIANO WA KARIBU SANA NA ROHO MTAKATIFU WAKATI WOTE.
   Biblia inasema kwamba, wanaoongozwa na Roho wa Mungu, hao ndiyo wana wa Mungu (Warumi 8:14). Kadhalika, Roho Mtakatifu hutusaidia udhaifu wetu katika kuomba, maana sisi hatujui kuomba ipasavyo, na Yeye pia hutuombea (Warumi 8:26). Tunapokuwa na uhusiano wa karibu sana na Roho Mtakatifu, Yeye hutufunulia wakati mzuri wa kuomba, si hivyo tu, lakini hutufundisha namna nzuri ya kuomba ili maombi yetu yasizuiliwe (Yohana 14:26) kwa kuwa Yeye ni msaidizi ambaye Baba amemleta kwa ajili yetu (Yohana 14:16; 14:26; 15:26; 16:7). Tukiwa na Roho Mtakatifu atatuwezesha kufanya yafuatayo;

1.      Atatufundisha kuomba sawasawa na mapenzi ya Mungu (1Yohana 5:14).

2.      Atatufundisha kuomba ipasavyo (Yohana 14:26; Yakobo 4:3).

3.      Atakufanya tuzae matunda, hivyo kufanya maombi yetu yasizuiliwe(Yohana 15: 9-17).

4.      Atatupa nguvu ya kusamehe wengine, hivyo kufanya maombi yetu yasizuiliwe (Marko 11:25-26).

5.      Atatuwezesha kuomba kwa kutumia Neno la Mungu, hivyo kufanya maombi yetu yawe na nguvu ya kupasua anga (Yohana 15:7).

6.      Atatuwezesha kuwa na mahusiano mazuri na familia zetu, maana uhusiano mbaya na wake au waume zetu, hufanya maombi yetu kuzuiliwa (I Petro 3:7).

7.      Atatuwezesha tusiombe kwa unafiki, kwa kuwa kuomba kwa unafiki kunasababisha muombaji asipokee chochote kutoka kwa Mungu (Mathayo 6:5-6)

8.      Atatuwezesha kuwajali wahitaji, kwani mtu asiyejali maskini, maombi yake hayawezi kusikiwa (Mithali 21: 13).

9.      Atatuwezesha tuwe na imani katika kuomba (Marko 11:23-24).

10. Atatuwezesha kukaa katika hali ya utakatifu wakati wote, kwani dhambi hufanya majeshi ya wakuu wa giza kuzuia maombi yetu (Isaya 59:1-2).

11. Hutufanya tusiwe na kiburi bali tuwe wanyenyekevu; mtu mwenye kiburi maombi yake huzuiliwa na wakuu wa anga (Ayubu 35:12-13).

4.   MUOMBAJI NI LAZIMA AWE NA SIFA YA KUWA NA BIDII KATIKA KUOMBA, NA KWA MUDA MREFU NA KILA WAKATI.
   Katika kitabu cha Waefeso 6:18 Maandiko yanasema, “Kwa sala zote na maombi mkisali kila wakati katika Roho, mkikesha kwa jambo hilo na kudumu katika kuwaombea watakatifu wote.” KatikaWakolosai 4:2 Biblia inasema, “Dumuni sana katika kuomba, mkikesha katika kuomba huku na shukrani” Muombaji mwenye sifa ya kuomba kila wakati, ndiye anayeweza kupasua anga kimaombi.

JINSI YA KUFANYA MAOMBI YA KUPASUA ANGA
     Kuna hatua za msingi ambazo, Mkristo mwenye sifa za hapo juu, akizifuata, atafanya maombi yake yawe na uwezo wa kupasua anga. Hatua hizi ni kama ifuatavyo;

HATUA YA KWANZA
    Kabla hatujaanza kuombea jambo lolote lile, ni vema kwanza tukatafakari, na kumuuliza Roho Mtakatifu, juu ya jambo tunalokwenda kuombea kama ni mapenzi ya yake au la. Tutajichunguza wenyewe kwamba, hilo jambo tunalokwenda kumuomba Mungu, je! Tunastahili kuliomba kwa wakati huo au la? au je! Hilo tunalotaka kumwomba Mungu ni hoja yenye nguvu kwake? (Isaya 41:21; 43:26). Hapa ndipo Wakristo wengi tunapofanya makosa kwenye uombaji. Kuwa na hoja yenye nguvu, ni kitu cha msingi sana mbele za Mungu ili tupokee kile tunachoomba.
    Maombi ya Wakristo wengi yanapata upinzani kwa kuwa yanakuwa si hoja zenye nguvu mbele za Mungu. Kumuuliza Roho Mtakatifu, kunaleta muongozo wa jinsi ya kuliombea jambo fulani. Lolote tunaloliomba kwa Mungu sawasawa na mapenzi yake, Yeye atusikia. Katika kitabu cha 1 Yohana 5:14 Biblia inasema, “Na huu ndiyo ujasiri tulio nao kwake, ya kuwa, tukiomba kitu sawasawa na mapenzi yake, atusikia.” Kwa hiyo ni wazi kabisa kwamba, tukiomba kinyume na mapenzi yake Yeye hawezi kusikia.
      Makundi mengi ya wanamaombi, huchukua hatua ya kuombea jambo fulani kama walivyopokea maelekezo ya kuliombea kutoka kwa wahitaji, bila kuuliza kwa Roho Mtakatifu kama ni sahihi kuliombea kwa namna hiyo au siyo sahihi. Kupata muongozo wa kuliombea jambo fulani kutoka kwa Roho Mtakatifu, ni jambo la msingi sana, kuliko kuliombea jambo moja kwa moja kama apendavyo aliyeleta jambo hilo.
    Wengine wanaweza wakafunga na kuomba, kumuombea mtu fulani afanikiwe katika biashara zake, wakati waombaji hao hawajui kama mtu huyu analipa fungu la kumi na sadaka kwa uaminifu. Kumuombea mtu wa namna hii ni kupoteza muda.
    Amani inapochafuka katika nchi, watumishi wa Mungu wasikimbilie kuwaambia watu waombee amani tu ya nchi hiyo bila kujua kwanza, chanzo cha uvunjifu wa amani hiyo nini. Watumishi wa Mungu, ni lazima waanze kwa kumuuliza Mungu chanzo cha uvunjifu wa amani hiyo. Hatupaswi kuliombea jambo lolote, bila kwanza kulitafutia usahihi wa jambo lenyewe kutoka kwa Roho Mtakatifu.
     Baada ya kupata majibu kutoka kwa Mungu, ndiyo Wakristo wapewe muongozo wa nini cha kuombea. Wakristo wanaweza kuombea amani, lakini kumbe, swala si kuombea amani tu, bali taifa limemkosea Mungu, hivyo linapaswa kufanya maombi ya toba ili taifa lipone (2 Nyakati 7:14). Taifa la Israeli lilipopigwa na watu wa mji wa Ai, baada ya kuuliza kwa Bwana, Bwana alimfunulia Joshua kuwa tatizo lilisababishwa na Akani mwana wa Zera, ambaye alikuwa ameiba hazina ya Mungu (Yoshua 7:1-26). Baada ya kugundua chanzo cha tatizo, wakapata muelekeo wa nini waombee na kipi wanapaswa kufanya.
    Swala kama hili, lilitokea kule Burudi miaka ya nyuma. Mwaka 1989, mwezi wa kumi, saa kumi na mbili asubuhi, Mtumishi wa Mungu Emmanueli Lazalo, alipewa ujumbe na Mungu juu ya kuharibiwa kwa Burundi na Tanzania kwa sababu ya uovu mkubwa. Ujumbe huo ulisema, “TANZANIA HAITAWEZA KUSIMAMA KATIKA SIKU YA KUPIMWA KWAKE, WALA BURUNDI NAYO.”
    Watu walipuuza na kuusahau ujumbe huu. Unabii huu ulikuja kutimia kwa Burundi, vurugu zilipokaribia kuanza katika nchi hiyo, watumishi wa Mungu walianza kuombea amani, badala ya kutangaza maombi ya toba kwa nchi nzima. Maombi ya kuombea amani kwa nchi ya Rwanda na Burundi, hayakuleta majibu, kwa kuwa waliomba kinyume na Mungu alivyotaka. Mungu alimtumia Mtumishi wake Emmanueli Lazalo ili watu watubu, lakini hao wakafanya kinyume.
     Moja ya vitu vya msingi ambavyo muombaji anatakiwa kufanya ni kumuuliza Roho Mtakatifu kabla ya kuanza kuombea jambo lolote ambalo anaona haliko wazi kwake au hajui chanzo chake. Lengo la kumuuliza Roho Mtakatifu, ni kuhakiki nini kimpendezacho Mungu ili aombee jambo hilo kwa usahihi. Katika kitabu cha Waefeso 5:10 Biblia inasema, “Mkihakiki nini impendezayo Bwana
     Kumuuliza Roho Mtakatifu ni maombi ya kutafuta taarifa kamili au muongozo, ili muombaji aweze kupata ushirikiano mzuri na Roho wa Mungu. Wachungaji wengi hawakufanikiwa kwa sababu hawakuuliza kwa Bwana kama Biblia inavyosema katika Yeremia 10:21, “Kwa sababu wachungaji wamekuwa kama wanyama, wala hawakuuliza kwa Bwana; basi hawakufanikiwa, na makundi yao yote yametawanyika.” Kama watoto wa Mungu tunapaswa kumwita Mungu ili atuonyeshe mambo makubwa na magumu tusiyoyajua kama maandiko yanavyosema katika Yeremia 33:3, “Niite, nami nitakuitikia, nami nitakuonyesha mambo makubwa, magumu usiyoyajua.”
   Baada ya waombaji kuhakikisha kwamba, maombi wanayokwenda kuomba ni mapenzi ya Mungu, na wana muongozo katika kuliombea jambo hilo, basi hawana budi kufuata hatua ya pili.

HATUA YA PILI
    Kabla hatujaingia kwenye kipindi cha maombi maalum, aidha ya muda mfupi au muda mrefu, ni lazima tuchukue hatua ya kufanya maandalizi binafsi ya kiroho siku au masaa au dakika kadhaa kabla ya kuingia kwenye maombi hayo. Kusudi kuu la maandalizi haya, ni kututengenezea mazingira ya kutufanya tuwe rohoni sana, maana vita vyetu ni katika ulimwengu wa roho (Waefeso 6:12).
    Mtu anapoingia kwenye maombi, yawe ya muda mfupi au ya muda mrefu bila maandalizi, muombaji huyo atachoka na kukata tamaa, atakosa matumaini, na anaweza akaishia njiani bila kukamilisha maombi hayo, kwani atapata uzito na upinzani mkubwa sana katika ulimwengu wa roho.
    Maandalizi haya yanajumuisha toba ya kumaanisha katika maeneo ambayo tumemkosea Mungu bila kukusudia, kwa kuwa Mkristo wa kweli hafanyi dhambi kwa kukusudia.
    Maandalizi haya, pia yanajumuisha, utengenezaji wa mahusiano yetu na Roho Mtakatifu, maana bila Yeye, hatuwezi kufanikiwa katika maombi (Warumi 8:26). Katika kipindi hiki cha maandalizi, tunapaswa kutumia muda wetu wote, kujinyenyekeza mbele za Roho Mtakatifu, tukijieleza mbele zake kwa unyenyekevu na upole, tukimbembeleza awe pamoja nasi, huku tukimwomba msamaha kwa machozi maeneo ambayo tumemuhuzunisha, na kumsihi atusaidie tusimuhuzunishe tena, tukimwomba atutie nguvu na kutufundisha kuomba ipasavyo.  Tutamwambia Roho Mtakatifu kuwa bila Yeye sisi hatuwezi kufanya chochote. Roho Mtakatifu siyo nguvu fulani kama wanavyodhani wengi, bali ni nafsi hai ya Mungu (Soma kitabu changu kinachoitwa ‘Roho Mtakatifu na utenda kazi wake’).
   Kutenda kazi na Roho Mtakatifu kunahitaji ufahamu wa ziada, asilimia 99.9 ya Wakristo bado hawajajua namna ya kwenda na Roho Mtakatifu. Baada ya Bwana Yesu kuondoka kwenda mbinguni, akatuachia Mungu Roho Mtakatifu akae pamoja nasi hapa duniani, bila Yeye kamwe hatutaweza kufanya chochote (Yohana 14:16; 14:26; 15:26; 16:7).
   Kadhalika, katika kipindi hiki cha maandalizi, muombaji anapaswa kutumia muda mwingi peke yake, ili apate kuwa na muda mwingi wa kuzungumza na Roho Mtakatifu. Muombaji anapaswa kuepuka mazingira yoyote yatakayomfanya ufahamu wake kurudi mwilini au kumuhuzunisha Roho Mtakatifu.
  Kwa maombi ya muda mfupi, muombaji anapaswa kufanya maandalizi, masaa au dakika kadhaa, kabla ya kuingia kwenye maombi hayo. Maandalizi hayo yatamfanya muombaji apate utayari wa kuomba. Maandalizi kwa muombaji, yatamfanya apate muunganiko katika ulimwengu wa roho.
   Baada ya maandalizi haya, muombaji; kwanza, atajisikia amani ya ajabu moyoni mwake; pili, atasikia furaha ya namna ya kipekee; tatu, atasikia uwepo wa Mungu usio wa kawaida; nne, atasikia hamu kubwa ya kuomba; tano, atasikia uamsho wa nguvu kubwa sana ya maombi.

ANGALIZO
   Kwa kuliombea tatizo la ghafla, hatuna budi kujitakasa wakati huo huo na kuingia moja kwa moja kwenye maombi, hapa hatuhitaji maandalizi ya siku au masaa kadhaa. Mara nyingi tatizo lolote la ghafla, kwa asili hutufanya tuende mbele za Mungu kwa unyenyekevu, hivyo kutufanya tuingie kwenye ulimwengu wa roho kwa wepesi sana, kulingana na uchungu tunaoupata kutokana na tatizo hilo.

HATUA YA TATU
    Baada ya kufuata hatua ya kwanza na ya pili kwa uaminifu, muombaji hana budi sasa kuingia kwenye maombi, akiwa na imani timilifu ya kupokea kile anachokwenda kuomba, huku akifuata vipengele vifuatavyo;

1.   KUFANYA TOBA KAMILIFU.
     Kabla ya kuanza kipindi cha maombi, muombaji atafanya maombi ya toba. Ni vema ikumbukwe kwamba, toba inayofanywa hapa ni kwa dhambi ambazo tumezifanya bila sisi kujua au kukusudia. Sisi kama watoto wa Mungu, hatupaswi kufanya dhambi kwa makusudi ili tutubu, dhambi za namna hii huwa hazisamehewi. Maandiko katika Waebrania 10:26 yanasema, “Maana, kama tukifanya dhambi kusudi baada ya kupokea ujuzi wa ile kweli, haibaki tena dhabihu kwa ajili ya dhambi; bali kuna kuitazamia hukumu yenye kutisha, na ukali wa moto ulio tayari kuwala wao wapingao.”


2.   KUMSHUKURU MUNGU KWA YOTE ALIYOTENDA.
     Hatuwezi kuwa watu wa kuomba tu, bila kuwa watu wa shukrani kwa yale mambo kadhaa ambayo Mungu ametenda kwetu. Na ndiyo maana Neno la Mungu katika Wakolosai 3:15 linasema, “.........tena iweni watu wa shukrani.” Ni jambo linalompendeza Mungu wakati wote, pale tunapoanza kumshukuru, kabla ya kuanza kuomba mambo mengine mapya. Mtume Paulo katika nyaraka zake zote, kwanza kabisa, anaanza na kumshukuru Mungu (Filemoni 1:4; 2 Timotheo 1:3; 1 Timotheo 1:12; 2 Wathesalonike 1:2; 1:13; 5:18; Wakolosai 1:3; 1:12 ; 3:17; Wafilipi 1:3; 4:6; Waefeso 5:4; 5:20; 1 Wakorintho 1:4; 1:14; Warumi 1:8). Kwa hiyo, kabla hatujaanza kuyaombea yale yaliyokusudiwa kuombewa katika siku hiyo, ni vema kwanza, tukitumia dakika kadhaa, katika kumshukuru Mungu kwa yale ambayo amefanya.
    Kitendo cha mimi na wewe kuwa wazima na afya njema kwa wakati huo wa maombi, hiyo ni neema, hatuna budi kumshukuru Mungu. Kitendo cha kupata neema ya kukusanyika katika maombi kwa wakati huo, hiyo ni neema, hivyo hatuna budi kumshukuru Mungu. Kitendo cha mimi na wewe kuwapo kwenye nchi ya amani na hata kupata nafasi ya kuomba kwa amani bila vurugu, hiyo ni neema, ni lazima tumshukuru Mungu. Kwa ujumla, yapo mambo mengi ambayo tunaweza kumshukuru Mungu na kumwinua kwa ajili ya hayo aliyotenda. Na baada ya kumshukuru Mungu na kumwinua kwa yake aliyotutendea, hatuna budi, kwenda kwenye kipengele kifuatacho.


3.   KUOMBA KUMWAGIWA ROHO WA NEEMA NA KUOMBA.
     Baada ya kumshukuru Mungu, kabla hatujaanza kupeleka hoja zetu mbele za Mungu (Isaya 41:21), kwanza, tutamwomba Bwana atumwagie Roho wa Neema na Kuomba kama maandiko yanavyosema katika Zekaria 12:10, “Nami nitawamwagia watu wa nyumba ya Daudi, na wenyeji wa Yerusalemu, roho ya neema na kuomba; nao watamtazama yeye ambaye walimchoma……..” Roho wa Neema na Kuomba ndiye Roho Mtakatifu anayetusaidia udhaifu wetu katika kuomba, kwa kuwa sisi hatujui kuomba jinsi ipasavyo (Warumi 8:26).


4.   KUANZA KUOMBA HUKU TUKITUMIA JINA LA YESU NA KUZITAJA AHADI ZA MUNGU (NENO).
    Baada ya kumwalika Roho Mtakatifu, muombaji anaweza kuendelea kuomba yale ambayo amepanga kuyaomba katika kipindi hicho cha maombi. Muombaji ni lazima aombe kwa Baba kwa Jina la Yesu. Wengi wanafanya maombi bila kutumia Jina la Yesu. Baba wa mbinguni hawezi kutufanyia jambo lolote tunapomwomba, kama hatutatumia jina la Yesu katika maombi yetu. Bwana Yesu katika kitabu cha Yohana 16:23 anasema, “Tena siku ile hamtaniuliza neno lolote. Amin, amini, nawaambia, mkimwomba Baba neno lolote atawapa kwa jina langu.” Pia katika Yohana 14:14 Bwana Yesu anasema, “Nanyi mkiniomba lolote, kwa jina langu, hilo nitalifanya, ili Baba atukuzwe ndani ya mwana. Mkiniomba neno lolote kwa jina langu, nitalifanya.”
   Maombi yoyote, yasiyoenda na muhuri wa jina la Yesu, ni rahisi kuzuiliwa na majeshi ya giza, na mara zote maombi haya huwa hayana majibu. Kwa ujumla sala, maombi au dua yoyote isiyohusisha jina la Yesu, hiyo siyo sala na haina faida yoyote.
  Pia wakati wa maombi, muombaji anapaswa kutumia Neno la Mungu yaani kuzitaja ahadi za Mungu kulingana na hitaji husika. Kwa kawaida Mungu analiangalia Neno lake ili apate kulitimiza (Yeremia 1:12), hivyo muombaji anapotaja ahadi alizotoa Mungu katika Neno lake kulingana na jambo analoombea, jambo hilo hufanyika kwa haraka, na majeshi ya wakuu wa giza, huwa hawawezi kuzuia, maana Neno la Mungu ni moto (Waebrania 4:12; Yeremia 23:29).


5.   KUSHINDANA NA WAKUU WA GIZA.
   Baada ya muombaji kumaliza kupeleka hoja zake zote mbele za Mungu, hatua inayo fuata ni kufanya maombi ya kushindana na wakuu wa giza katika anga. Muombaji anapofanya maombi ya kushindana na wakuu wa anga, ni lazima awe amesimama. Maombi haya, yana makusudi ya kupiga majeshi ya wakuu wa giza ili kuwafanya wasizuie maombi yako (Waefeso 6:12).
   Haya ni maombi ya vita ili kuwatawanya na kuwasambaratisha majeshi ya wakuu wa giza. Silaha yoyote itakayotamkwa na muombaji ili kupiga majeshi ya wakuu wa anga ni lazima itumwe kwa jina la Yesu. Kwa mfano, unapotuma moto wa Roho Mtakatifu, ni lazima utume kwa muhuri wa jina la Yesu. Muombaji anapofanya maombi haya, ni lazima ufahamu wake utulie katika mapambano hayo. Kumaanisha kwa muombaji anapotuma makombora, ndiko kunakomfanya ayashinde majeshi hayo. Ni lazima tukumbuke kwamba, chochote tunachotamka na kufanya wakati huu katika ulimwengu wa mwili, katika ulimwengu wa roho, hufanyika hivyo hivyo.
  Shetani hutumia muda huu, kuwateka ufahamu waombaji wanaoshindana. Muombaji anaweza kujikuta anashindana kwa mdomo tu, lakini mawazo yake yakawa kwenye kitu kingine. Tunapokuwa katika maombi haya, tuhakikishe tunakuwa katika mazingira, yenye kutufanya, tusihame kiufahamu. Tukizingatia haya, tunashinda na zaidi ya kushinda (Warumi 8:37).

6.   KUJIFUNIKA KWA ULINZI WA MUNGU.
     Muombaji akifanya maombi haya ya kushindana na wakuu wa giza kikamilifu, ufalme wa shetani unakuwa umeharibiwa sana. Hivyo, shetani mara zote hupanga mipango ya kuja kulipiza kisasi kwa muombaji husika. Ni lazima ifahamike kwamba kuna mapepo ya kisasi (Spirits of vengeance), kazi ya mapepo haya, ni kulipiza kisasi kwa yoyote ambaye ameharibu ufalme wa giza. Mapepo haya, yana silaha nyingi, na mbinu mbalimbali za kulipiza kisasi kwa maadui zao.  Hivyo ni jukumu la kila muombaji, kujifunika kwa ulinzi wa Mungu baada ya kufanya maombi haya.
    Mapepo hawa huweza kumvamia muombaji, na kumpiga kwa homa kali, kuwashwa mwili, kuharisha, kizunguzungu na mengine mengi. Muombaji asipokuwa makini, anaweza asirudi tena kwenye maombi. Kwa hiyo unaposikia hali yoyote tofauti baada ya kutoka katika maombi haya, usiogope, endelea kukemea kwa jina la Yesu, huku ukiamini kwamba unalindwa na nguvu ya Mungu kwa imani (1 Petro 1:5). Pia unaweza ukashangaa kuona wale waliokuwa wanakudai siku nyingi ambao walitulia kukusumbua, siku hiyo ndiyo wanakuja kwa kasi au kukupigia simu ili kukudai pesa. Yanapotokea haya, usiyaogope, ujue wazi kabisa, umeuharibu sana ufalme wa giza.
    Mapepo hawa wanaposindwa kumpiga muombaji husika, huvamia watoto au mume/mke au ndugu wa karibu wa muombaji, unaweza ukarudi nyumbani na ukashangaa kuona mafarakano yasiyo ya kawaida na familia yako au majirani. Pia majeshi haya huweza kuvamia hata biashara na miradi mbalimbali na kuharibu.
    Ni kwa sababu hii basi, muombaji anapomaliza kufanya maombi ya kushindana, anapaswa kujifunika yeye mwenyewe, familia yake, miradi yake, huduma yake, mahusiano yake, vyakula, vinywaji, hewa unayovuta, pamoja na vyote alivyo navyo kwa damu ya Bwana wetu Yesu Kristo. Mapepo wanaogopa damu ya Yesu Kristo, hivyo unapojifunika kwa imani, unakuwa salama.
    Pia ni lazima uombe ulinzi kwa jina la Yesu huku ukitaja ahadi za Mungu kuhusu ulinzi; baadhi ya ahadi hizo ni kama ifuatavyo; Isaya 54:17 Mungu ameahidi kwamba, “Kila silaha itakayofanyika juu yako haitafanikiwa, na kila ulimi utakaoinuka juu yako katika hukumu utauhukumu kuwa mkosa. Huu ndiyo urithi wa watumishi wa Bwana, na haki yao inayotoka kwangu mimi, asema Bwana.” Zaburi 34:7 Neno la Mungu linasema, “Malaika wa Bwana hufanya kituo, akiwazunguka wamchao na kuwaokoa.” Zekaria 2:8Neno la Mungu linasema, “Kwa maana Bwana wa majeshi asema hivi, ili nitafute utukufu amenituma kwa mataifa wale waliowateka ninyi; maana yeye awagusaye ninyi aigusa mboni ya jicho lake.” Walawi 26:7 Mungu ameahidi kwamba, “Nanyi mtawafukuza adui zenu, nao wataanguka mbele zenu kwa upanga.”

7.   KUMSHUKURU ROHO WA NEEMA NA KUOMBA (ZEKARAI 12:10).
     Roho wa Neema na Kuomba ndiye Mungu Roho Mtakatifu (Zekaria 12:10). Hivyo kama tulianza naye, hatuna budi kumaliza naye kwa kumshukuru kwa neema ya kipekee aliyotupa katika kuomba (Zaburi 109:30). Baada ya kumshukuru Roho Mtakatifu, pia ni vema kumwomba, atupe neema ya kuwepo tena siku inayofuata kwa ajili ya maombi, na kumsihi awe pamoja nasi katika kila hatua tunayokwenda kupiga.
    Baada ya kufanya hayo yote kwa ukamilifu na kwa unyenyekevu, ni wazi kabisa maombi yako yatakuwa  na nguvu kubwa ya kusambaratisha majeshi ya wakuu wa giza na kupasu anga, hatimaye kumfikia Mungu.

MUDA UNAOTAKIWA KATIKA KUFANYA MAOMBI
YA KUPASUA ANGA
     Ili maombi yetu yapate kutikisa majeshi ya wakuu wa anga, muda wa kufanya maombi hayo, ni kitu cha kuangaliwa sana. Biblia haitupi muda maalum wa kuomba, ingawa tukiwaangalia waombaji mashuhuri katika Biblia, inaonesha wazi kwamba, walitumia muda mrefu sana katika kuomba. Katika 1 Samweli 15:10-11 tunaona Samweli aliomba usiku kucha. Katika Luka 6:12tunaona pia Bwana Yesu aliomba usiku kucha. Danieli aliomba mara tatu kila siku (Danieli 6:10). Daudi naye vivyo hivyo aliomba kwa machozi asubuhi, mchana na jioni (Zaburi 55:17). Tukimwangalia Nabii mke Ana binti Fanueli, yeye siku zote alikuwa hekaluni akiomba usiku na mchana (Luka 2:36-37). Yakobo alimng’ang’ania malaika usiku kucha ili kupata Baraka (Mwanzo 32:24-30). Ili kurudisha mvua inyeshe, Eliya aliomba mara saba (1 Wafalme 18:41-45). Paulo aliomba mchana na usiku (2 Timotheo 1:3; 1 Wathesalonike 3:10). Kwa hiyo, tukiwaangalia waombaji hawa na wengine waliotumiwa sana na Mungu katika zama za Biblia, inadhihirisha wazi kwamba kwa siku, walitumia masaa mengi katika kuomba.
     Hata hivyo, tukichunguza kwa makini, juu ya muda wa kuomba, ambao umesisitizwa katika maandiko, tunagundua kwamba, ni sehemu nyingi katika Biblia, maandiko yanatuambia juu ya kukesha katika kuomba (Luka 21:36; Wakolosai 4:2; Waefeso 6:18; 1 Wakorintho 16:13; Marko 13:37; 2 Wakorintho 6:5; Marko 13:35; Marko 13:33; Mathayo 26:41; Mathayo 26:38; Mathayo 25:13; Mathayo 24:42; Marko 14:38; Marko 14:38; Ufunuo 3:2; Ufunuo 16:15; 1 Petro 5:8; 1 Wathesalonike 5:6). Na neno kukesha katika kuomba maana yake, ni kitendo cha kukaa macho usiku wote huku mtu akiwa anaomba. Sasa tujiulize, Je! Usiku una masaa mangapi? Usiku una masaa tisa (9). Muombaji mwenye uwezo wa kuomba masaa tisa kwa siku, ni wazi kabisa Mkristo huyo atakuwa si wa kawaida katika ulimwengu wa roho. Maombi ya mtu wa namna hii, majeshi ya giza hayawezi kuhimili kuyazuia.
   Hata hivyo, Bwana Yesu katika Mathayo 26:40 aliwaambia wanafunzi wake,“…...Je! Hamkuweza kukesha pamoja nami hata saa moja?” Kwa kusema ‘hata saa moja’ Bwana Yesu hapa, alimaanisha kuwa, saa moja, ndicho kiwango cha chini cha muda wa kuomba. Hivyo kwa muombaji mchanga aombe muda usiopungua saa moja kwa siku. Lakini kwa muombaji mwenye karama ya uombaji, kipimo cha chini cha uombaji ni karibu wastani wa masaa 4 kwa kila siku.
   Huduma ya Campus Crusade for Christ, yenye makao makuu huko Arrowhead Springs, Califonia nchini Marekani ina watendakazi wanane (8) ambao maisha yao yote, ni maombi, hawana kazi nyingine ya kufanya. Watendakazi hawa, hukutanika kila asubuhi kanisani na kuomba kwa masaa nane (8) mfululizo bila kupumzika kila siku. Pia kuna muombaji mwingine aitwaye Mrs Bernice Watne wa Eagle Grove, Iowa, Marekani, muombaji huyu ni kilema anayetembelea wheelchair, lakini huomba masaa 4 kwa siku, na anasema anaifurahia hali hiyo ya ulemavu kwani inampa nafasi kubwa ya kuomba.

KWA NINI MUOMBAJI ANAPASWA KUOMBA MASAA MENGI KWA SIKU ILI KUPASUA ANGA?

   Tulijifunza hapo nyuma kwamba, mara zote, wakati Wakristo walio wakamilifu na wenye imani, wanapoanza kuomba, maombi yao huwa kama moshi na unapanda juu taratibu, lakini wanapoendelea kuomba, maombi yao hubadilika na kuwa kama moshi unaokwenda kwa kasi juu na ulionyooka. Na mara wakiendelea kuomba, ghafla huanza kulipuka na kugeuka kuwa moto. Moto huu, ndiyo unaounguza utando wa kipepo katika anga unaozuia maombi ya Wakristo yasimfikie Mungu. Na maombi yao huwa na nguvu sana, na hata kusababisha kupasua kizuizi kilichowekwa na wakuu wa giza, na hatimaye maombi hayo kufika kwa Mungu.
  Sasa hatua zote hizi, mpaka maombi kugeuka kuwa moto, muombaji anapaswa kutumia masaa mengi katika kuomba, ili maombi yapate kupasua anga la mtaa, anga la wilaya, anga la mkoa, anga la Taifa na anga la kimataifa, hatimaye kumfikia Mungu. Maombi ya muombaji yakigeuka kuwa moto, muombaji anapaswa kuendelea kuomba, ili kuhakikisha moto huo hauzimiki. Mara akikatiza maombi tu, moto huzimika na kufanya maombi yake kuzuiliwa na wakuu wa anga.


NI WAKATI UPI MZURI WA KUFANYA MAOMBI?
   Wakati wote ni wakati mzuri wa kuomba, cha msingi ni kwamba, pale unaposikia haja ya kuomba ni vema ukaanza kuomba. Zaburi 32:6 Maandiko yanasema, “Kwa hiyo kila mtu mtaua akuombe wakati unapopatikana.” Maandiko katika kitabu cha Waefeso 6:18 yanasema, “Kwa sala zote na maombi mkisali kila wakati katika Roho, mkikesha kwa jambo hilo na kudumu katika kuwaombea watakatifu wote.” Lakini hata hivyo, tutapata ushindi zaidi kama tutakuwa na utaratibu wa kuomba kila siku, usiku na mchana. Kitabu cha Luka 18:7 Biblia inasema, “Na Mungu, je! Hatawapatia haki wateule wake wanaomlilia mchana na usiku naye ni mvumilivu kwao?

UMUHIMU WA MAOMBI YA USIKU NA ALFAJIRI
     Sisi kama watoto wa Mungu, hatuna budi kufahamu kwamba, Shetani ni mfalme wa GIZA. Wasaidizi wake wanaitwa wakuu wa giza (Waefeso 6:11-12). Nguvu za Shetani zinaitwa NGUVU ZA GIZA (Wakolosai 1:13). Kwa hiyo, ni muhimu kufahamu kwamba Shetani hufanya kazi zaidi usiku kuliko mchana.
    Dhambi nzito na uharibufu mkubwa hufanywa zaidi usiku. Uzinzi, uasherati, wizi, uchawi, ulevi, kucheza dansi, ujambazi, unyang’anyi na mambo mengi machafu hufanywa usiku.
    Mipango yote ya shetani hufanywa USIKU. Kazi za shetani zinazodhihirika mchana wote, hutokana na mipango ya shetani iliyopangwa usiku uliotangulia. Ukiona mtu amegongwa na gari mchana, huo mpango ulipangwa usiku uliotangulia. Mipango ya kumsaliti Bwana Yesu, ilipangwa usiku na kutekelezwa mapema alfajiri. Mipango ya kumshambulia Daudi ilikuwa usiku pia (2 Samweli 17:1-2).
   Wakuu wa giza hufanya mipango yao ya uharibifu usiku, hivyo nasi kama tutakuwa macho usiku na kuvunja mipango hiyo, au kuamka alfajiri na mapema na kubomoa mipango yao yote kwa maombi, ushindi hupatikana siku mzima. Licha ya kuomba kabla ya kulala, lakini ni muhimu sana kuomba usiku au alfajiri na mapema. Kutokuomba usiku au alfajiri na mapema ni kuruhusu mipango ya shetani, siku hiyo itekelezwe kwetu binafsi na kwa kanisa lote.
  Shetani anaogopa sana maombi ya usiku na alfajiri, hivyo hufanya kila jinsi kuyazuia yasifanyike. Kama Wakristo, hatuna budi kumpinga mpaka akimbie (Yakobo 4:7). ALFAJIRI ni wakati wowote baada ya saa kumi usiku, mpaka wakati ule ambao bado kuna giza na haijawa hata asubuhi.
   Kumpinga kwetu shetani ili asituzuie kufanya maombi ya usiku na alfajiri, hakuna budi kuambatane na jitihada zetu binafsi za kimwili. Tukishiba kupita kiasi, ni wazi hatutaweza kuamka usiku au alfajiri na mapema kwa ajili ya maombi. Usiku tule kwa kiasi na tunywe maji mengi sana, hii kwa kiasi inaweza kutusaidia kuamka. Hata hivyo, yupo Roho Mtakatifu, msaidizi wetu (Yohana 14:16; 14:26; 15:26; 16:7), kama tutakuwa waaminifu kwake, yeye atatusaidia kutuamsha usiku katika wakati unaofaa zaidi. Kuomba usiku na alfajiri, kunahitaji kujitia nidhamu na kusema ‘Lazima niamke kwa jina la Yesu’ na kuyakatalia matakwa ya mwili unaosaidiana na Shetani kuzipinga roho zetu (Wagalatia 5:16-17).

ANGALIZO: ALFAJIRI ni wakati wowote baada ya saa kumi usiku, mpaka wakati ule ambao bado kuna giza na haijawa hata asubuhi.

MIFANO YA WATAKATIFU WALIOFANYA
MAOMBI YA USIKU NA ALFAJIRI
1.   YAKOBO-Yakobo hatimaye aliitwa Israeli kwa sababu alishindana na Mungu na watu na kuwa mshindi (Mwanzo 32:28). Hata hivyo ushindi wake ulianzia katika maombi ya alfajiri alipokuwa akiomba na kuweka nadhiri zake (Mwanzo 28:18-22).

2.   SAMWELI-Samweli aliomba na kumlilia Mungu usiku kucha yaani usiku na alfajiri (1 Samweli 15:10-11).

3.   BWANA YESU-Bwana Yesu mara nyingi aliomba usiku kucha yaani usiku na alfajiri (Luka 6:12; Mathayo 4:2; Marko 1:35).

4.   WAZAZI WA SAMWELI-Wazazi wa Samweli, waliweza kufanikiwa kumzaa mtoto Samweli aliyekuwa nabii wa kipekee, kutokana na wao kuzingatia maombi ya alfajiri (1 Samweli 1:19). Sisi nasi tukizingatia maombi ya alfajiri au uziku, tutaona mambo makuu katika maisha yetu.

5.   HEZEKIA-Hezekia naye aliomba maombi ya alfajiri (2 Nyakati 29:20). Hezekia aliongezewa maisha alipokuwa katika kufa, na Mungu alimjua kama Hezekia alikuwa mwaminifu kwake kutokana na kujikana na kufanya maombi ya alfajiri. Maombi yake ya alfajiri yalimpa ushindi dhidi ya mkono wa mfalme wa Ashuru (2 Wafalme 20:1-6).

6.   DAUDI-Daudi pia alifanya maombi ya alfajiri (Zaburi 57:8; 119:147). Ushindi mkubwa wa mfalme Daudi ulitokana na kuzingatia maombi ya alfajiri na usiku.

7.   PAULO-Maombi ya usiku yalimfanya Paulo kutumiwa na Mungu kipekee kuliko mitume wengine. Siri kuu ni maomba ya usiku (2 Timotheo 1:3; 1 Wathesalonike 3:10).

NGUVU YA MAOMBI YA KUFUNGA
    Katika kitabu cha Mathayo 17:14-21 Maandiko yanasema, “.........Lakini namna hii haitoki ila kwa kusali na KUFUNGA.” Katika mistari hii, Bwana Yesu anatufundisha kwamba, yako mambo ambayo hayawezekani kama mtu ataomba tu bila ya kufunga.
    Mkristo anaweza akaomba kwa ajili ya jambo fulani kwa muda mrefu, lakini bado upo uwezekano wa Mkristo huyo, kutopokea chochote, endapo kama maombi yake yatakuwa hayaambatani na kufunga. Kwa hiyo, ni jambo la msingi kwa kila mtoto wa Mungu kujifunza, jinsi ya kufunga ipasavyo.

MAANA YA KUFUNGA
     Neno “Kufunga” linatokana na neno la Kiyunani linaloitwa “Nestevo.” Kadhalika neno ‘Nestevo’ nalo linatokana na maneno mawili ya Kiyunani ambayo ni “Ne” na “Esthio” Neno “Ne” maana yake ni “Bila” au “Hapana”, Kwa kiingereza ni “No” au “Without’. Neno “Esthio” maana yake “Kula chakula au kinywaji”, kwa Kiingereza ni “To eat solid or liquid food.”  Neno “Nestevo” likiunga hayo maneno mawili ya Kiyunani “Ne” na “Esthio”, inaleta maana ya “Bila kula chakula au kinyajia chochote.” Kwa hiyo maana ya kufunga ni kutokula chakula wala kinywaji chochote.
    Kufunga siyo kuacha kusoma vitabu, kuacha kuchana nywele au kuacha n.k. Bali kufunga ni kuacha kula na kunywa kinywaji chochote. Maana hii ya kufunga inathibitishwa na maandiko yafuatayo; Ezra 10:6; Yona 3:7; 2 Samweli 3:35; Esta 4:16; Kumbukumbu; 9:9; Matendo 9:9.
    Kufunga siyo kuacha kula vyakula kama wali, ugali au mihogo halafu tukawa tunakunywa maji, soda, juisi, maziwa, uji au kula matunda n.k. Kufunga siyo kula vyakula laini na kuacha vyakula vigumu, bali kufunga ni kuacha kula chakula na kunywa kabisa.
    Wapo Wakristo ambao wanahalalisha kwamba kufunga unaweza kula vyakula laini au kunywa tu na ukaacha vyakula vigumu, hiyo siyo sahihi kabisa. Wakristo hao hutumia andiko la Danieli 10:2-3 linalosema, “Katika siku zile mimi, Danieli, nalikuwa nikiomboleza muda wa majuma matatu kamili. Sikula chakula kitamu, wala nyama wala divai haikuingia kinywani mwangu, wala sikujipaka mafuta kabisa, hata majuma matatu kamili yalipotimia.” Katika andiko hili “Sikula chakula kitamu” kwa tafsiri ya Biblia ya kiingereza (The living Bible) chakula kitamu ni “Desserts” au “Pudding”. Neno la Kiingereza “Desserts” au “Pudding’ lina maana ya chakula kitamu kinacholiwa baada ya mlo (matunda), chakula hicho ni kama maembe, ndizi, nanasi, papai, machungwa n.k. Katika mistari hiyo Danieli anasema kwamba, siyo tu kwamba hakula chakula, bali hata matunda, yaani hakula chakula wala kunywa chochote kwa muda wote wa wiki tatu.

UMUHIMU WA KUFUNGA
    Bwana wetu Yesu Kristo, anamtazamia kila mtu aliyeookoka kuwa na maisha ya kufunga pale anapotuambia, “Tena mfungapo,” “Bali wewe ufungapo” (Mathayo 6:16-18). Maombi ya kufunga, yanampa nguvu ya kiroho kila aliyeokoka, na kumfanya imani yake ipande kwa viwango vya juu sana. Wanafunzi wa Yesu, hawakuweza kumtoa pepo kwa sababu ya upungufu wa imani yao iliyotokana na kukosa kusali na kufunga. Na ndiyo maana Bwana Yesu akawapa maelekezo kwamba, hawana budi kusali na kufunga ili wawe na imani hiyo; Mathayo 17:21 Biblia inasema, “Lakini namna hii haitoki ila kwa kusali na kufunga.” Mtu anapofunga, mwili huwa na nidhamu kwa sababu ya kutiishwa, hivyo kumfanya mtu huyo kuwa rohoni sana na hatimaye kumpa nafasi nzuri ya kuzungumza na Mungu.

MIFANO YA KIBIBLIA YA WATAKATIFU
WALIOKUWA WAKIFUNGA
1.         Yesu Kristo- Bwana wetu Yesu Kristo baada ya kujaa Roho Mtakatifu, alifunga siku arobaini na baada ya mfungo huo alirudi kwa Nguvu ya Roho Mtakatifu (Luka 4:1, 14).
2.         Musa (Kutoka 34:28).
3.         Ezra (Ezra 10:6).
4.         Eliya (1 Wafalme 19:8).
5.         Daudi (Zaburi 109:24).
6.         Yoshua (Kutoka 24:12-15).
7.         Danieli (Danieli 10:1-3).
8.         Anna binti Fanueli (Luka 2:36-37).
9.         Paulo (Matendo 9:8-9; 2 Wakorintho 11:27).
10.    Paulo na Barnaba (Matendo 14:23).
11.    Kanisa la kwanza (Matendo 13:1-3).

   Ikiwa watakatifu wengi zama za Biblia walifunga na kupata ushindi mkubwa katika maisha yao, sisi nasi hatuna budi kuchukua hatua ya kufunga. Tunapopuuza kufunga, tutakuwa dhaifu sana kiimani na hatimaye kukosa ushindi.

NGUVU YA KUFUNGA
    Sehemu nyingi katika Biblia, tunaona jinsi mambo yalivyobadilika baada ya kufunga na kuomba. Kufunga kunaweza kutokana na mbiu ya kufunga, yaani kufunga kunakotokana na kiongozi kutangaza watu wafunge (2 Nyakati 20:3-4; Yona 3:7-8; Ezra 8:21). Pia kufunga kunaweza kutokana na uamuzi wa mtu binafsi (Nehemia 1:4). Mifano ifuatayo, inatufundisha juu ya nguvu ya kufunga;
1.      Wana wa Israeli walipigwa mfululizo katika vita na wana wa Benyamini. Baada ya kushindwa mfululizo, wakaamua kufunga na kuomba (Waamuzi 20:20-26). Baada ya kufunga na kuomba matokeo yakabadilika, Benyamini wakapigwa sana, na wana wa Israeli wakashinda vita kwa kuiteketeza miji ya maadui zao kwa moto (Waamuzi 20:34-48).
2.      Ezra hakumtegemea mfalme, bali alifunga, na matokeo ya kufunga yakawa kwamba mkono wa Mungu ulikuwa pamoja naye, yeye na wenzake wakaokolewa kwa mkono wa adui (Ezra 8:31-32). Ikiwa kanisa linahitaji kuokolewa kutoka katika mkono wa adui, ni lazima liwe na wafungaji.
3.      Yehoshafati alipata taarifa za majeshi kombaini ya maadui waliotaka kumpiga. Akatangaza kufunga na kuomba (2 Mambo ya Nyakati 20:1-4), matokeo yake wakashinda vita kirahisi mno kwa sifa tu (2 Mambo ya nyakati 20:22-25).
4.      Nehemia alivyopata taarifa za kubomolewa kwa ukuta wa Yerusalemu na malango yaliyoteketezwa kwa moto, alifunga na kuomba (Nehemia 1:3-4), na matokeo yake ukuta ulijengwa tena kwa muujiza mkubwa (Nehemia 6:15-16).
5.      Hasira ya Bwana kwa kanisa, au Taifa, inayotokana na uovu wa watu, inaweza utoweshwa endapo watu hao watakuwa tayari kufunga na kuomba (1 Wafalme 21:27-29; Yona 3:7-10; Ezra 10:6).

MUDA WA KUFUNGA
    Biblia haijaweka sheria juu ya muda maalum wa kufunga. Hata hivyo tukichunguza vipindi ambavyo watakatifu zama za Biblia walifunga, tunaweza kupata mwanga juu ya muda wa kufunga katika kuombea jambo husika.  Hata hivyo mifungo mingi katika Biblia haitaji idadi ya siku zilizotumika katika mifungo hiyo, lakini katika jedwali lifuatalo, tutaangalia mifungo ambayo imetaja siku pamoja na sababu za kufanya mifungo hiyo;


MFUNGAJI
KIPINDI CHA KUFUNGA
SABABU ZA KUFUNGA
ANDIKO
1.
Daudi
Asubuhi hadi jioni
Kumuombolezea aliyekufa
2 Samweli 3:35
2.
Israeli
Asubuhi hadi jioni
Kumuuliza Bwana juu ya kushindwa kwao.
Waamuzi 20:24-27
3.
Daudi
Asubuhi hadi jioni
Kumlilia aliyekufa
2 Samweli 1:12
4.
Yuda
Siku moja
Kuutafuta uso wa Mungu.
Nehemia 9:1-4






5.
Yuda
Siku moja
Kuutafuta uso wa Mungu.
Yeremia 36:6
6.
Mafarisayo
Siku moja mara mbili kwa juma.

Luka 18:9-12
7.
Wana wa Israeli
Siku moja
Kumlilia Bwana waokolewe na mkono wa Wafilisti.
1 Samweli 7:6-14
8.
Esta na wana wa Israeli
Siku tatu
Kumwomba Mungu watoke katika hatari ya kuuawa.
Esta 4:13-16
9.
Kundi la watu
Siku tatu
Kumsikiliza Bwana Yesu akifundisha
Mathayo 15:32
10.
Paulo
Siku tatu
Wokovu na wito wa Paulo.
Matendo 9:9
11.
Daudi
Siku saba
Kumwomba Mungu kwa ajili ya mtoto.
2 Samweli 12:16-18
12.
Wana wa Israeli
Siku saba
Kuomboleza kifo cha Sauli na wanawe.
1 Samweli 31:13
13.
Paulo na watu 276
Siku 14 nzima
Safari iliyojaa misukosuko
Matendo 27:33-37.
14.
Danieli
Siku 21 nzima
Kumwomba Mungu ili kufunuliwa jambo.
Danieli 10:1-3
15.
Musa
Siku 40 nzima
Kuwaombea wana wa Israeli na kuketi mbele za Bwana.
Kumbukumbu 9:9, 18, 25-29; 10:10
16.
Yoshua
Siku 40 nzima
Kuketi mlimani mbele za Mungu.
Kutoka 24:12-15





17.
Eliya
Siku 40 nzima
Safari ndefu.
1 Wafalme 19:5-8
18.
Bwana Yesu
Siku 40 nzima
Kujaribiwa nyikani kutokana na kuongozwa na Roho.
Mathayo 4:1-2

  Kutokana na vipindi hivi vya ufungaji wa watakatifu mbalimbali kama tulivyoona hapo juu, tunajifunza mambo yafuatayo;
1.      Kipindi cha kufunga katika kumtafuta Bwana kwa maombi, kinabidi kiwe siyo chini ya siku moja (masaa 24).
2.      Kipindi cha kawaida cha mfungo kinaweza kufikia siku tatu nzima yaani masaa 72 yote. Ni katika uzito usio wa kawaida tunazidisha hapo kwa maongozi ya Roho Mtakatifu, hata hivyo siku hazizidi saba.
3.      Kufunga zaidi ya siku saba nzima, lazima kuambatane na kufunuliwa neno. Mtu hawezi kufunga siku 40 bila kula wala kunywa mpaka kuwe na maongozi dhahiri ya Mungu, uwepo wake na msaada wake maalum (1 Wafalme 19:8).

   Mwanafunzi halisi wa Kristo, atajipangia muda wa kufunga angalau siku tatu kwa kila mwezi. Inaweza kuwa siku moja katika wiki mara tatu na siyo mfululizo.

VIZUIZI VYA NGUVU ZA KUFUNGA
1.      Nia ya kufunga (Warumi 12:2).
Nia ya kufunga, ikiwa kinyume na Neno la Mungu, huzuia kupatikana kwa nguvu ya kufunga.
2.      Kufunga huku tukiwa na dhambi (Yeremia 14:10-12; Isaya 58:3-5).
3.      Kufunga bila kuomba
Kufunga ni lazima kuambatane kumtafuta Bwana kwa maombi (2 Nyakati 20:3-4; Ezra 8:21; Mathayo 17:21). Kufunga bila kuomba ni kushinda njaa kusiko na faida.
4.      Kufunga hakupaswi kuchukua nafasi ya imani.
Hatupaswi kuwaza kila jambo haliwezekani mpaka tufunge kwanza. Pasipo imani haiwezekani kumpendeza Mungu (Waebrania 11:6; Yakobo 1:6). Ni lazima ifahamike kwamba kufunga kunachochea tu imani.


 NA: DR. GODWIN GUNEWE

Share:

USCF-SJUT NEWS

Designed by Joel Elphas @ 2015. Powered by Blogger.

Recent Posts