Saturday, June 3, 2017

Nguvu ya Kuvumilia

Uwezo wetu wa kuvumilia hadi mwisho katika wema utakuwa unalingana moja kwa moja na nguvu ya ushuhuda wetu na kina cha uongofu wetu.
Kila asubuhi tunapoamka, tunakumbana na siku mpya iliyojaa changamoto za maisha. Changamoto hizi huja kwa aina nyingi: changamoto za kimwili, pingamizi za kifedha, matatizo na mahusiano, majaribio ya kihisia, na hata mapambano na imani ya mtu.

Nyingi za changamoto tunazokabiliana nazo maishani zinaweza kutatuliwa na kushindwa, hata hivyo, nyengine huenda zikawa ngumu kuelewa na kutowezekana kushindwa na zitakuwa nasi mpaka tutakapoaga duniani. Tunapovumilia kwa muda changamoto tunazoweza kutatua na tunapoendelea kuvumilia changamoto ambazo hatuwezi kutatua, ni muhimu kukumbuka kwamba nguvu ya kiroho tunayokuza zitatusaidia kuvumilia vyema changamoto zote tunazokabiliana nazo maishani.

Ndugu na dada, tunaye Baba wa Mbinguni, anayetupenda, ambaye amesanifu kuwepo kwetu duniani ili tuweze kibinafsi kujifunza masomo tunayohitaji kujifunza ili kufuzu kwa ajili ya uzima wa milele katika uwepo wake.

Kipindi katika maisha ya Nabii Joseph Smith kinaeleza kanuni hii. Nabii na wenzi kadhaa walikuwa wamekuwa wafungwa kule Liberty, Missouri, kwa miezi. Wakiteseka gerazani, Nabii Joseph alimsihi Bwana katika maombi ya unyenyekevu kwamba Watakatifu wangeweza kufarijiwa kutokana na mateso yao ya sasa. Bwana alijibu kwa kumfundisha Nabii Joseph, na sisi sote, kwamba changamoto tunazokumbana nazo, zikivumiliwa vyema, zitatusaidia mwishowe. Hili ndilo jibu la Bwana kwa dua ya Joseph:

“Mwanangu, amani iwe katika nafsi yako, taabu yako na mateso yako yatakuwa kwa muda mfupi;

“Na halafu, kama utastahimili vyema, Mungu atakuinua juu.”1

Baba wa Mbinguni amepanga safari yetu maishani kuwa mtihani wa silka zetu. Tunaachwa tushawishiwe na mema na mabaya na kisha kupewa wakala wa kimaadili kujichagulia wenyewe njia tutakayochukua. Kama vile nabii Samweli wa Kitabu cha Mormoni wa kale alivyofundisha, “Mko huru, mmekubaliwa kujichagulia, kwani tazama, Mungu amewapatia elimu na amewafanya huru.”2

Baba wa Mbinguni pia alielewa kwamba kutokana na hali yetu ya kidunia hatungefanya chaguo sahihi au la haki kila wakati. Kwa sababu sisi si wakamilifu na kwa sababu sisi hufanya makosa, tunahitaji usaidizi ili kurudi kwa uwepo Wake. Msaada unaohitajika hutolewa kupitia mafundisho, mfano, na dhabihu ya upatanisho wa Yesu Kristo. Dhabihu ya upatanisho wa Mwokozi huwezesha wokovu wetu wa baadaye na utukufu kupitia kanuni ya toba. Tukitubu kwa uaminifu na dhati, Upatanisho unaweza kutusaidia kuwa wasafi, kubadilisha asili yetu, na kuvumilia vyema changamoto zetu.

Uvumilivu ni kanuni muhimu inayopatikana katika mafundisho ya Yesu Kristo. Ni muhimu kwa sababu uzuri wa maisha yetu ya baadaye ya milele unalingana na uwezo wetu wa kuvumilia katika wema.

Katika 2 Nefi 31 nabii Nefi anatufundisha kwamba baada ya kupokea agizo lile lile la wokovu la ubatizo ambalo Yesu Kristo alipokea na kisha tupokee karama ya Roho Mtakatifu, lazima “tusonge mbele tukila na kusheherekea neno la Kristo, na tuvumilie hadi mwisho, tazama, [na basi] hivyo ndivyo asema Baba: [Sisi] tutapokea uzima wa milele.”3

Hivyo basi, ili kupokea baraka kuu ya zote za Baba yetu wa Mbinguni, ambayo ni uzima wa milele, lazima tukamilishe kazi ya agano inayostahili na kisha tuendelee kutii maagano yanayohusika. Yaani, lazima tuvumilie vyema.

Uwezo wetu wa kuvumilia hadi mwisho katika wema utakuwa unalingana moja kwa moja na nguvu ya ushuhuda wetu na kina cha uongofu wetu. Wakati shuhuda zetu ziko imara na tumeongoka kwa kweli kwa injili ya Yesu Kristo, chaguo zetu zitasawishiwa na Roho Mtakatifu, zitakuwa na msingi katika Kristo, na zitahimili hamu yetu ya kuvumilia katika wema. Ikiwa shuhuda zetu ni dhaifu na uongofu wetu ovyo, hatari ni zaidi kwamba tutashawishiwa na tamaduni za uongo za dunia ili kufanya chaguo mbaya.

Ningependa kushiriki tukio linaloonyesha juhudi inayohitajika kuvumilia kimwili na kisha kulilinganisha kwa juhudi inayohitajika kuvumilia kiroho. Baada ya kurudi kutoka misheni yangu, nilikuwa na nafasi ya kucheza mpira wa vikapu na kocha mwenye ushawishi mkubwa na mwandishi katika chuo kule California. Kocha huyu alikuwa makini sana kuhusu wachezaji wake kuwa katika hali nzuri ya kimwili kabla ya kuanza kwa msimu wa mpira wa vikapu. Moja ya mahitaji yake ya zoezi kabla ya yeyote kati yetu kuweza kugusa mpira wa kikapa kwenye kiwanja cha mazoezi ilikuwa ni kukimbia mzunguko wa mbio za nyika katika milima karibu na shule kwa wakati maalum na ngumu sana. Ninakumbuka jaribio langu la kwanza kabisa katika kukimbia kozi hii ya mbio za nyika punde baada ya kurejea kwangu kutoka misheni: Nilifikiria ningekufa.

Ilichukua wiki nyingi za mafunzo makali ili hatimaye kuvunja rekodi ya wakati ambao kocha alikuwa ameweka kama lengo. Ilikuwa ni hisia nzuri si ​​tu kuweza kukimbia mzunguko lakini pia kuharakisha hadi kwenye uhondo wa mwisho hadi kwenye laini ya kumaliza.

Ili kucheza mpira wa vikapu vyema, unahitaji kuwa katika hali nzuri ya kimwili. Kuwa katika hali nzuri ya kimwili huja kwa gharama, na gharama hiyo ni kujitolea, uvumilivu, na nidhamu ya kibinafsi. Uvumilivu wa kiroho pia huja kwa gharama. Ni gharama ile ile: kujitolea, uvumilivu, na nidhamu ya kibinafsi.

Ushuhuda, kama mwili wako, unahitaji kuwa katika hali nzuri kama unautaka hudumu. Hivyo basi ni jinsi gani tunaweka ushuhuda wetu katika hali nzuri? Hatuwezi kufanya miili yetu kuwa katika hali nzuri ya kucheza mpira wa vikapu kwa kutazama tu mpira wa vikapu kwenye televisheni. Vile vile, hatutaweza kuweka shuhuda zetu katika hali nzuri kwa kutazama tu mkutano mkuu kwenye televisheni. Tunahitaji kusoma na kujifunza kanuni za msingi za injili ya Yesu Kristo, na kisha ni lazima tufanye tuwezavyo kuizitumia maishani. Hivyo ndivyo tunavyokuwa wafuasi wa Yesu Kristo, na hivyo ndivyo tunavyojenga ushuhuda wa kudumu.

Tunapokabiliwa na shida maishani na hamu yetu ni kuiga sifa za Yesu Kristo, ni muhimu kuwa tayari kiroho. Kuwa tayari kiroho kunamaanisha tumekuza sulubu na nguvu ya kiroho---tutakuwa katika hali nzuri ya kiroho. Tutakuwa katika hali nzuri kiroho hata kwamba tutachagua wema kila mara. Tutakuwa hatuhamashiki katika hamu na uwezo wetu wa kuishi injili. Kama vile mwandishi mmoja asiyejulikana aliwahi kusema, “Ni lazima uwe mwamba ambao mto hauwezi kuondoa.”

Kwa sababu sisi tunakabiliwa na changamoto kila siku, ni muhimu kwamba tufanye kazi juu ya ushupavu wetu wa kiroho kila siku. Sisi  tunapokuza ushupavu wa kiroho, tamaduni za uongo za dunia, pamoja na changamoto zetu za kibinafsi za kila siku, zitakuwa na athari ndogo kwa uwezo wetu wa kuvumilia katika wema.

Mifano mizuri ya ushupavu wa kiroho huja kutoka historia za familia zetu wenyewe. Miongoni mwa hadithi nyingi kutoka kwa mababu zetu, tutaweza kupata mifano ambayo inaonyesha tabia chanya ya uvumilivu.

Hadithi kutoka kwa historia ya familia yangu mwenyewe inaeleza kanuni hii. Baba ya babu yangu mkuu Joseph Maynes Watson alizaliwa mnamo 1856 kule Hull, Yorkshire, Uingereza. Familia yake ilijiunga na Kanisa kule Uingereza na kisha kwenda Jijini Salt Lake. Alimuoa Emily Keep mnamo 1883, na wakawa wazazi wa watoto wanane. Joseph aliitwa kuhudumu misheni ya muda mnamo Juni 1910, alipokuwa na umri wa miaka 53. Na kwa usaidizi wa mke wake na watoto wanane, alirudi nchi yake ya asili Uingereza kuhudumu misheni yake.

Baada ya kuhudumu kwa uaminifu kwa takriban miaka miwili, alikuwa akiendesha baiskeli yake pamoja na mwenziwe kwenda misa ya Shule ya Jumapili kule Gloucester, Uingereza, ambapo tairi yake ikapasuka. Alishuka kutoka wa baiskeli yake ili kutathmini uharibifu. Alipoona ya kuwa ilikuwa imeharibika sana na ingechukua muda kurekebisha, alimwaambia mwenziwe amtangulie na kuanza ibada ya Jumapili na angefika pale baada ya muda mfupi. Punde tu alipomaliza kusema hayo, alianguka chini. Alikufa ghafula kutokana na mshtuko wa moyo.

Joseph Watson Maynes kamwe hakumwona mke wake na watoto wanane tena katika maisha haya. Waliweza kusafirisha mwili wake kurudi katika Jiji la Salt Lake na kuwa na huduma ya mazishi yake katika ukumbi mzee wa Waterloo Assembly Hall. Kauli iliyotolewa katika mazishi yake na Mzee Anthony W. Ivins wa Jamii ya Mitume Kumi na Wawili inatufundisha somo muhimu kuhusu maisha, kifo, na uvumilivu: “Hii ndiyo injili inatupa---si kinga kutokana na kifo, lakini ushindi juu yake kupitia matumaini ambayo tunayo katika ufufuo mtukufu. … Unamgusia [Joseph Maynes] . …Ni furaha, na jambo la kuridhisha na shangwe kujua kwamba wanadamu hujitolea maisha yao kwa haki, kwa imani, wakiwa wakweli kwa imani.”4

Hadithi hii ya familia yangu inanishawishi kujaribu niwezavyo kufuata mfano wa uvumilivu na sulubu ya kiroho iliyoonyeshwa na baba ya babu yangu. Ninavutiwa pia na imani ya mke wake, Emily, ambaye maisha yake baada ya kifo cha Joseph hakika yalikuwa mzigo mzito kubeba. Ushuhuda wake ulikuwa imara na uongofu wake kamili akiishi maisha yake yote baadaye akiwa mwaminifu kwa imani akiwasaidia watoto wake wanane pekee yake.

Mtume Paulo alisema, “Na tuweke kando kila mzigo mzito, na dhambi ile ituzingayo kwa upesi, na tupige mbio kwa subira katika yale mashinidano yaliyowekwa mbele yetu.”5 Mashindano yaliyowekwa mbele yetu katika dunia hii ni mbio ya uvumilivu, iliyojaa vizuwizi. Vizuwizi katika mashindano haya ni changamoto tunazoamka nazo kila asubuhi. Tuko hapa duniani ili kukimbia mbio, kutumia wakala wetu wa kimaadili, na kuchagua kati ya mema na mabaya. Ili kukamilisha mbio kwa heshima na mafanikio na kurudi kwa Baba yetu wa Mbinguni, tutalazimika kulipa gharama ya kujitolea, uvumilivu na nidhamu ya kibinafsi. Tunahitaji kuwa katika hali nzuri ya kiroho. Tunahitaji kukuza sulubu ya kiroho. Tunahitaji shuhuda imara zitakazoelekeza kwa uongofu wa kweli, na kwa matokeo tupate ndani yetu amani ya ndani na nguvu inayohitajika kuvumilia changamoto zozote huenda tukakabilina nazo.

Hivyo basi bila kujali changamoto unazoamkia kila asubuhi, kumbuka---na nguvu ya kiroho unayokuza, pamoja na msaada wa Bwana, mwishoni mwa mashindano utaweza kufurahia hakikisho ambalo Mtume Paulo alionyesha aliposema:

“Kwa maana, mimi sasa namiminwa, na wakati wa kufariki kwangu umefika.

“Nimevipiga vita vilivyo vizuri, mwendo nimeumaliza, Imani nimeilinda:

“Baada ya hayo nimewekewa taji ya haki, ambayo Bwana, mhukumu mwenye haki, atanipa siku ile.”6

Nawatolea ushuhuda na ushahidi wangu wa uhalisi wa Baba wa Mbinguni mwenye upendo na mpango wake wa furaha mkuu na wa milele, ambao umetuleta kwenye dunia hii wakati huu. Roho wa Bwana awavutie kukuza ndani yenu nguvu ya kuvumilia. Katika jina la Yesu Kristo, amina.
Share:

USCF-SJUT NEWS

Designed by Joel Elphas @ 2015. Powered by Blogger.

Recent Posts