ADHARI NA MATOKEO YA DHAMBI YA UZINZI/UASHERATI KWA MTU ALIYEOKOKA.
Katika Mithali 6:32 Biblia inasema “Mtu
aziniye na mwanamke hana akili kabisa; afanya jambo litakalomwangamiza nafsi
yake” na pia katika Mithali 6:26 inasema “Maana kwa Malaya mtu hutiwa
katika hali ya kuhitaji kipande cha mkate; na kahaba humwinda mtu anase nafsi
yake iliyo ya thamani”
UZIZI/UASHERATI: Ni tendo la ndoa linalofanywa na mtu mume na mtu mke
kinyume na mapenzi ya Mungu/ kabla ya wakati sahihi wa Mungu (Ndoa takatifu).
Ni watu wengi sana ambao wamerudi nyuma
na kuanguka katika dhambi hii. Hadi sasa bado kuna kundi kubwa la watu
waliokoka ambao bado dhambi hii ina nguvu juu yao na bado wanafanya jambo hili
kinyume na mapenzi ya Mungu katika maisha yao.
Si kana kwamba Mungu anafuga dhambi kwa
kutokuwadhihirisha hao watu na uovu wao, isipokuwa hataki jina lake litukanwe,
kwa kuwa ikijulikana huyo mtu au hao watu wameanguka huenda kutokana na
nafasi zao kiuongozi, kihuduma kiushuhuda nk jina la Mungu litatukanwa sana na
mataifa lakini pia hata na wale waliokwisha kuokoka. Kwa lugha rahisi hao watu au huyo mtu atakuwa ametoa nafasi ya jina la
Mungu kutukanwa.
Kwa bahati mbaya sehemu kubwa ya
watumishi wa Mungu katika makanisa yao hawaoni athari ya hili jambo katika
upana wake kama Biblia inavyosema. Inafika mahali baadhi yao
wanawafariji wale walioanguka kwa kusema jipe moyo, tubu na Mungu ni wa rehema
atakusamehe. Na wengine utasikia wanasema haukuanza wewe, Daudi naye
yalimshinda sembuse wewe!!.
Wengine wanatumia maandiko kabisa
wanasema ‘mwenye haki huanguka mara
saba’ we mara moja tu wala isikusumbue sana tengeneza tu Mungu atakusamehe,
na wengine wanasema mimi mwenyewe
nilishindwa kwahiyo, hata wewe isikusumbue saana kazana tu uoe wa kwako au omba
upate mume/mke. Ni kama vile watu wanatumia rehema/neema ya Mungu kuendelea
kutenda dhambi tena kwa ujasiri.
Sikiliza, si kana kwamba napingana na
neno au na mawzo ya hao watumishi wenzangu La hasha!. Nakubali kwamba Mungu husamehe dhambi na maovu ikiwa ni pamoja na
dhambi hii ya uasherati/uzinzi (Matendo ya Mitume 3:19 ‘Tubuni basi, mrejee, ili dhambi zenu zifutwe, zipate kuja
nyakati za kuburudishwa kwa kuwako kwake Bwana’).
LAKINI
TAMBUA Mungu husamehe kwa sababu 2 kubwa sana:-
Ø Moja
hafurahii kifo cha mwenye dhambi ‘Ina
thamani machoni pa Bwana mauti ya wacha Mungu wake’ Zaburi 116:15.
Ø Na
pili ni ili kukurejesha kwenye nafasi yako ili uweze kulitumikia kusudi lake.
Lakini je, unajua madhara/matokeo ya
dhambi hii kwa mtu aliyeokoka anapoifanya? Hata kama Mungu akikusamehe/amekusamehe,
unajua nini kimetokea/kilitokea kwako pale ulipofanya dhambi hii? Au je unaijua
gharama ya kurejea kwenye nafasi yako aliyoikusudia Mungu?
Biblia inasema aziniye na mwanamke
afanya jambo litakalomwangamiza nafsi yake? Huenda huwa unausoma
tu huo msitari bila kujua uzito wa hayo maneno. Ni vizuri kwanza ukajua kwamba
ndani ya nafsi ya mtu ndiko kwenye hisia, nia (utashi), akili, na maamuzi.
KUBWA Zaidi kwa Mungu nafsi ndiyo ‘operating
system’ kama kwenye computer, kwa maana ndiyo kiwanda kinachotoa tafsiri ya
kila kitu ambacho Mungu anazungumza/sema na mwanadamu
MAMBO 3 YANAYOTOKEA
MTU ALIYEOKOKA ANPOFANYA DHAMBI HII YA UASHERATI/ZINAA:-
1.
Kuharibika kwa mfumo wa mahusiano na
mawasiliano kati yake na Mungu.
Katika mfumo wa ufalme wa Ki –
Mungu ni kawaida kwa mtu aliyeokoka na mwenye mahusiano mazuri na Mungu, kuona
Mungu akiwasiliana/akisema naye kwa njia mbalimbali ili kumshirikisha mawazo na
mipango yake ikiwa ni namna ya kumuongoza mtu huyo katika kusudi lake chini ya
jua. Hii ina maana suala la mawasiliano kati ya mtu na Mungu ni la
kawaida kwa mtu mwenye mahusiano mazuri na Mungu wake.
Sasa mtu anapofanya dhambi hii, athari
yake ni hii, dhambi inaharibu mfumo huu
wa mahusiano kati ya mtu na Mungu. Na
mahusiano kati ya mtu na Mungu yakiharibika mawasilano kati ya Mungu na mtu
yanakatika/kuharibika pia. Ninaposema yanakatika ina maana si rahisi kwa Mungu kusema tena na huyo mtu
au huyo mtu kusema tena na Mungu wake kwa sababu asili/mazingira hayaruhusu
na hili linapelekea mafunuo/sauti ya
Bwana kuwa hadimu kwako, kwa kanisa, kwa jamii, kwa kampuni na hata nchi
tegemeana na nafasi yako katika ufalme wa Mungu.
2.
Kuharibika kwa mfumo wa kufanya
maamuzi/kufikiri ndani yako.
Dhambi hii inaharibu mfumo wa kufanya
maamuzi, shetani anapomuongoza mtu
kufanya dhambi hii, lengo/interest yake ipo kwenye nafsi ya mtu huyo.
Shetani akikamata nafsi ya mtu maana yake amekamata akili/nia ya mtu huyo,
akikamata akili ya mtu huyo maana yake amekamata maamuzi yake pia. Na akikamata
maamuzi yako amekamata matokeo ya maisha yako ya sasa na ya baadae.
Hivyo mtu huyu hataweza tena kufikiri
mambo ya rohoni kama Paulo anavyoagiza kwa Warumi ile sura ya 8:5 “Kwa maana wale waufuatao mwili
huyafikiri mambo ya mwili, bali wale waifuatao roho huyafikiri mambo ya roho”.
Hivyo kufanya dhambi hii ni kuathiri mfumo wako wa kufanya maamuzi, na hii ina
maana hata Mungu akileta wazo lake kwako huwezi kulipokea maana mfumo wa kuamua
umeukabidhi kwa Shetani kwa njia ya zinaa/uasherati.
3.
Kuharibika kwa mfumo wa utiifu ndani
yako.
Warumi 2:13 ‘Kwa sababu sio wale
wasikiao sheria walio wenye kuhesabiwa haki, bali ni wale waitendao
sheria watakaohesabiwa haki”. Baada ya matokeo hayo 2 hapo juu hiki ndicho kinachozaliwa mwishoni.
Ubaya wa dhambi hii inaharibu mifumo hii
ambaayo ndiyo misingi ya mwenye haki. Fuatili maisha ya watu wengi sana
walioanguka kwenye dhambi hii angalia
utiifu wao mbele za Mungu ukoje. Nakuhakikishia utagundua ni ngumu sana kwao
kutii maagizo ya Mungu kwao. Mtu wa aina hii hata Mungu akimpa maagizo ya
kutekeleza hataweza kwa kuwa tayari mahusiano yamevunjika, mamuzi yametekwa .
JE
MUNGU ANATAKA TUJIFUNZE NINI KUPITIA HILI?
Unapokuwa na mahusiano mazuri na
Mungu hii mifumo yote mitatu/Mambo yote 3 yatafanya kazi vizuri na ndiyo
kusudi la Mungu. Dhambi hii inapoingia inasababisha kuharibka kwa mifumo hii
mitatu (MAHUSIANO,KUFIKIRI NA UTII). Kitu kibaya au kinacho muumiza Mungu ni
kwamba hata kama akikusamehe pale utakapotubu, LAKINI itakugharimu sana
kuirejesha mahali pake mifumo hii 3. Na
ndio maana neno linasema afanya jambo litakalomwangamiza nafsi yake,
kwahiyo utakua unakazi ya kurejesha NAFSI yako katika upya wake na ni garama sana
sana tu. Kwasababu kila kilichomo ndani ya nafsi (HISIA, NIA, AKILI, MAAMUZI)
kimeangamizwa. Ili kuirejesha mifumo hii maombi ya muda mrefu ya rehema na
kutengeza mahali palipobomoka ni ya lazima.
PENGINE unaweza kusema la muhimu Mungu
amenisamehe, hayo mengine sijali sana. Unaweza kusema hayo maneno kama hujui/ huelewi muda unathamani kiasi
gani kwa Mungu, na pia mahusiano kati ya muda na Mungu.
NGOJA
NIKUAMBIE SIRI YA MUNGU NA MUDA JAPO KIDOGO; Muda na Mungu ni
marafiki, na tena wote wana mahusiano mzuri sana. Muda anaongoza maamuzi
ya Mungu na Mungu anaongoza matumizi ya muda kwa kuiweka mipango ndani ya mtu
na kumwagiza atekeleze ndani ya muda. Hivyo kwa Mungu muda ni muhimu sana.
Kitu gani namaanisha hapa; Mungu hakutenga/kuweka muda wa mtu
kurejesha mifumo hii kwa sababu umeanguka katika dhambi.
Katika kipindi ambacho wewe unatubu na kutengeneza kwa Mungu wako ili kurejesha
mifumo hii, basi uwe na uhakika upande wa pili umesha athiri kusudi la Mungu
duniani kupitia wewe ambalo limefungwa katika muda. Sasa kama utatumia siku
tano, mwezi mmoja, miezi sita, mwaka mzima nk, kurejesha hii mifumo basi
kwa kipindi hicho chote utakuwa umekwamisha kusudi la Mungu kupitia wewe. Na
ndio maana Biblia inasema Shetani
anawinda nafsi yako iliyo ya thamani, maana anajua akikamata nafsi yako
amekamata akili, nia, hisia na maamuzi yako na hivyo amefanikiwa kuharibu hiyo mifumo na kusababisha mipango ya Mungu
isifanyike kwa muda aliokusudia kupitia wewe.
Kwa Mfano; Fikiria
umepangiwa na Mungu kusafiri umbali wa kilomita 500 ndani ya masaa saba (7).
Mungu amekupa gari ambalo ni kusudi lake
kwako. Hivyo litazame gari ulilopewa kama kusudi la Mungu kwako na wewe
ni dereva. Sasa wewe ukaamua kuliendesha gari bila kuweka maji kwenye
injini. Baada ya kusafiri umbali wa kilomita 300 injini ya gari ikafa kwa
kukosa maji na mbele yako zimebaki kilomita 200. Je unajua utakuwa umeathiri
kwa kiwango gani kusudi la Mungu? Kutokana na mfano huu, unapotenda dhambi hii
je unajua ni kwa kiwango gani utakuwa umeathiri mipango ya Mungu kupitia
wewe duniani kwa kipindi chote ambacho utakuwa unairejesha mifumo iliyopo ndani
ya nafsi yako mahali pake?.
Kinacho muumiza/huzunisha Mungu
kimsingi si kwa sababu umeanguka dhambini, lakini ni kwa sababu kuanguka kwako
dhambini kunamzuia yeye kukutumia wewe mpaka hiyo mifumo yote irejee mahali
pake. Hii ina maana interest ya Mungu ipo
kwenye muda. Maana anajua itakugharimu wewe muda wa kutengeneza na
itamgharimu yeye muda wa kukusubiri wewe utenegeze mifumo hii.
Mpendwa kumbuka hili usije sahau, Mungu
hategemei wewe uanguke katika dhambi hii, maana kadri unavyoanguka ndivyo
unavyokwamisha na kuchelewesha kazi ya Mungu duniani kupittia wewe. Je unajua hasara na matokeo ya kukwamisha
na kuchelewesha kazi ya Mungu?
Je
katika nafasi ambayo Mungu amekupa Kazini, huduma, au kanisa unachunga kwa
kiasi gani nafsi yako isiharibiwe na dhambi hii? Neno linasema Matendo ya Mitume 20:28 “Jitunzeni nafsi zenu, na
lile kundi lote nalo, ambalo Roho Mtakatifu amewaweka ninyi kuwa waangalizi ndani yake, mpate kulilisha
kanisa lake Mungu, alilolinunua kwa damu yake mwenyewe”.
Naamini ujumbe huu utakusaidia
kuhakiksha unafanya maamuzi ya kutofanya tena dhambi hii si kwa sababu
imeandikwa tu usizini bali ni kwa sababu unampenda Mungu na unataka kuhakikisha
kusudi la Mungu linafanikiwa bila kukwamishwa kwa dhambi hii.
Mwisho.
******** MUNGU
ATUSAIDIE. *********