MAOMBI YENYE UWEZO WA KUPASUA ANGA
NA: DR. GODWIN GUNEWE
MAOMBI NA JINSI YANAVYOZUILIWA
NA WAKUU WA ANGA
Moja kati ya silaha kuu, ambayo inamwezesha mtoto wa Mungu kushinda vita dhidi
ya majeshi ya giza, ni maombi. Hofu kubwa kwa shetani na majeshi yake, ni pale
anapokuwapo mtu mwenye nguvu ya kuzalisha maombi yaletayo moto, na hatimaye
kuleta athari kubwa sana katika ufalme wa giza.
Ni ukweli usiopingika kwamba, watoto wa Mungu katika kanisa la leo, wanakosa
ufahamu sahihi wa namna gani wanaweza kuzalisha maombi yanayoweza kutishia
usalama wa shetani na majeshi yake, kama vile ilivyokuwa katika kanisa la
kwanza. Wengi wanaomba, lakini hawapokei majibu ya maombi yao, kwa kuwa
wanaomba vibaya (Yakobo 4:3). Wengi wanaomba, lakini hawaombi kwa imani,
hivyo kusababisha maombi yao kutokuwa na nguvu ya kupenya katika anga.
Ni kwa sababu hii basi, tutachukua muda mrefu, katika kuchimbua siri kuu iliyo
katika maombi, na kufahamu kwa mapana na marefu, sababu inayomfanya shetani kuogopa
sana maombi.
Kabla hatujaingia kwa undani sana, ni vema kwanza tukifahamu kwa nini
tunatakiwa kufanya maombi. Hatuwezi kusababisha maombi yanayoweza kupasua anga
kama hatujui kwa kina, kwa nini tunapaswa kuomba. Zifuatazo ni sababu kuu zinazopelekea
watoto wa Mungu kufanya maombi;
1. Maombi ni uchaguzi wa Mungu wa kuzuia nguvu na kazi za shetani (Mathayo
6:13; Waefeso 6:12, 18).
2. Maombi hutupatia msaada wa Mungu katika kila hali (Zaburi
3:3-4; Zaburi 34:4, 6).
3. Maombi yanaondoa vikwazo au vipingamizi vyote (Marko 11:23-24).
4. Maombi ni njia ya kupata amani tunapokabiliwa na hali ya kutisha
na kukatisha tama (Wafilipi 4:4-7).
5. Maombi hugeuza mioyo na tabia ya watu wengine (Nehemia 2:4-8).
6. Maombi ni njia ya uponyaji wa kimwili na kiroho (Yakobo
5:14-15).
7. Maombi huleta msukumo wa kiroho na kumtia mtu nguvu wakati mtu
fulani anapokabiliwa na hali ya kushindwa (Wakolosai 1:9-11).
Kwa ujumla, maombi ni njia ya kuita nguvu ya Kimungu ili ikatende kazi katika
eneo kusudiwa.
SABABU KUU ZINAZOPELEKEA KUZUILIWA AU KUCHELEWESHWA KWA MAJIBU
YA MAOMBI YETU
Asilimia kubwa ya watoto wa Mungu, katika kanisa la leo, wamekata tamaa kabisa
katika kuomba. Na sababu kuu ni kucheleweshwa au kutopokea kabisa kwa majibu ya
maombi yao. Zipo sababu kuu nne zinazopelekea majibu ya maombi kucheleweshwa au
kuzuiliwa kabisa, ingawa katika kitabu hiki nitaizungumzia kwa undani sana
sababu ya pili, yaani ushindani wa wakuu wa giza katika anga (Danieli
10:12-13).
1. DHAMBI/
UOVU (Isaya 59:2; Mithali 28:9)
Dhambi ni kikwazo kikubwa kinachosababisha muombaji asipokee majibu ya maombi
yake. Katika Isaya 59:2 tunasoma, “Lakini maovu yenu
yamewafarikisha ninyi na Mungu wenu, na dhambi zenu zimeuficha uso wake msiuone,
hata hataki kusikia.” Mtu yeyote asiyekwenda na maagizo yote ya Mungu, huyo
ni mtenda dhambi, na maombi yake hayawezi kumfikia Mungu, maana maombi yake ni
chukizo mbele za Mungu, kama maandiko yanavyotuambia katika Mithali
28:9, “Yeye aligeuzaye sikio lake asiisikie sheria, hata sala yake ni
chukizo.”
2. USHINDANI WA WAKUU WA
GIZA (Danieli 10:12-13)
Wakuu wa giza katika anga, huchukua nafasi kubwa sana katika kuzuia au
kuchelewesha majibu ya maombi yetu. Yapo majeshi ya ufalme wa giza maelfu na
maelfu katika kila anga la eneo fulani, na moja ya kazi yao ni kuzuia maombi ya
watoto wa Mungu. Zama za Danieli mkuu wa anga aliye katika eneo la Uajemi,
aliweza kuchelewesha majibu ya Danieli (Danieli 10:12-13).
3. KUPIMWA JINSI
TUNAVYOMTUMAINIA MUNGU PEKEE (Zaburi 78:7; 26:1-2)
Sababu hii ya kucheleweshwa kwa majibu ya maombi yetu, hutokana na Mungu
mwenyewe na siyo majeshi ya giza. Mungu huchelewesha majibu ya maombi yetu yeye
mwenyewe, ili kupima imani yetu na kuona namna gani tunaweza kumtumainia yeye
kwa asilima zote.
4. KULINDWA KWA MAISHA
YETU YA KIROHO (2 Wakorintho 12:7-9).
Mungu anatujua vema hali zetu za kiroho tulizo nazo, na anajua nani akipewa
hiki anamwacha Mungu, na nani akipata hiki ataendelea kuwa na Mungu. Hivyo
katika kulinda usalama wetu wa kiroho, kuna vitu ambavyo tukimwomba, huwa
hatupi kwa wakati huo au kutotupa kabisa, kwa kuwa anajua tukipata kitu fulani
tutamwacha Mungu. Hufanya hivi, kwa upendo wake mkuu kwetu ili tusije kuingia
jehanamu ya moto. Kuna watu wanakuwa wanyenyekevu mbele za Mungu wakiwa hawana
fedha, na mara wakipata fedha wanachanganyikiwa na kumwacha Mungu na hatimaye
kurudi dhambini.
MUONEKANO WA MAOMBI KATIKA ULIMWENGU
WA ROHO
Watoto wa Mungu wanapoomba duniani, maombi yao, katika ulimwengu wa roho
huonekana kwa mfumo wa moshi. Katika kitabu cha Ufunuo 8:4Biblia
inasema, “Na moshi wa ule uvumba ukapanda mbele za Mungu, pamoja na maombi
ya watakatifu, kutoka mkononi mwa malaika.” Athari za maombi ya Wakristo
dhidi ya ufalme wa shetani, zinatofautiana kati ya muombaji na muombaji,
kulingana na sifa alizonazo muombaji huyo, zinazomwezesha kusababisha maombi
yenye nguvu, ya kutawanya ukungu wa kipepo katika anga.
Sababisho la uharibifu katika ufalme wa anga, linategemea sana na uhusiano wa muombaji
na Roho Mtakatifu, kiwango cha imani alicho nacho, pia utakatifu alio nao,
kadhalika maarifa aliyo nayo katika Neno la Mungu, pamoja na maarifa ya
kupeleka maombi hayo.
Vitu hivyo, ndiyo vinavyofanya muombaji azalishe aina fulani ya maombi katika
anga. Kimsingi, maombi ya Wakristo katika anga, huonekana katika mfumo wa namna
tatu;
A. MAOMBI YALIYO DHAIFU SANA
Maombi haya, huitwa dhaifu sana, kwa sababu hayana uwezo wa kuwafikia au kuleta
Athari kwa majeshi ya giza yanayozuia maombi ya Wakristo katika anga. Maombi
haya huwa katika mfumo wa moshi usio na muelekeo mmoja, huzagaa katika anga na
hatimaye kupotea katika hewa bila kusababisha madhara yoyote katika ukuta wa
kipepo, yanakuwa hayana nguvu ya kupenya utando wa kipepo. Maombi ya namna hii
hutoka kwa watu wanaoomba huku wakiwa na dhambi (Isaya 59:2). Na mara
nyingi, wakuu wa anga, huwa hawashughuliki na maombi ya namna hii, kwa kuwa
hayana madhara yoyote kwao.
B. MAOMBI YALIYO VUGUVUGU.
Maombi ya namna hii, huonekana kama moshi unaopanda juu na hata kufika kwenye
ukungu au utando wa kipepo, lakini moshi huu, unakuwa hauna uwezo wa kuyeyusha
utando huo ili kupenya na kufika mbinguni, kwa kuwa ni moshi usio na moto.
Maombi haya yanakuwa hayazalishi moto wa kuyeyusha utando huo mzito ulio na
mfano wa kama nta. Huu utando ndiyo kizuizi kikubwa.
Hivyo ni wazi kabisa, maombi ya namna hii huwa hayawezi kupasua anga, ingawa
yanaweza kuleta shida kwa majeshi ya wakuu wa anga. Haya ni maombi ya watu
walio watakatifu, lakini mioyoni mwao hawana imani na kile wanachoomba, kwa
kuwa wanakuwa na mashaka fulani. Katika kitabu chaWaebrania 10:38 Biblia
inasema, “Lakini mwenye haki wangu ataishi kwa imani; naye akisita-sita,
roho yangu haina furaha naye.”
C. MAOMBI YALIYO NA MOTO
Aina hii ya tatu ya maombi, huonekana kama moshi ambao umejaa
moto. Na moshi huu unapopanda juu, ni wa moto sana kiasi kwamba, huyeyusha
utando wa kipepo katika anga na kuyeyuka kama nta, na kupasua anga
lililozuiliwa na wakuu wa giza, na hatimaye hupenya na kufika mbinguni.
Mara zote, wakati Wakristo walio wakamilifu na wenye imani, wanapoanza kuomba,
maombi yao huwa kama ya aina ya kwanza, lakini wanapoendelea kuomba, maombi yao
hubadilika na kuwa kama ya aina ya pili. Na mara wakiendelea kuomba, ghafla
huanza kulipuka na kugeuka kuwa moto. Na maombi yao huwa na nguvu sana, na hata
kusababisha kupasua kizuizi kilichowekwa na wakuu wa giza, na hatimaye maombi hayo
kufika kwa Mungu.
JINSI WAKUU WA GIZA WANAVYOZUIA MAOMBI
YA WATOTO WA MUNGU
Watoto wa Mungu
wanapoomba, maombi yao huweza kuzuiliwa kwa namna mbili;
1. Maombi huzuiliwa
wakati yanakwenda mbinguni ili yasimfikie Mungu mbinguni.
Aina hii ya kizuizi hufanywa na majeshi ya giza yaliyo katika anga kwa
ushirikiano wa majeshi ya giza yaliyo katika ardhi. Mtoto wa Mungu anapoomba,
maombi huanza kupaa kwa mfumo wa moshi, na kwenda juu mbinguni, hivyo majeshi
ya wakuu wa giza wanapoyaona maombi hayo, hufanya jitihada kuyazuia ili
yasifike mbingu ya tatu yaani mbinguni alipo Mungu (2 Wakorintho 12:2).
Ni vema ifahamike kwamba, katika anga yaani mbingu ya kwanza na ya pili, kuna
majeshi ya wakuu wa giza, ambayo yamejipanga kikamilifu ili kupambana na watoto
wa Mungu, ikiwemo kuzuia maombi yao yasimfikie Mungu. Katika kitabu cha Waefeso
6:12 Biblia inasema, “Kwa maana kushindana kwetu sisi si juu ya
damu na nyama; bali ni juu ya falme na mamlaka, juu ya wakuu wa giza hili, juu
ya majeshi ya pepo wabaya katika ulimwengu wa roho.” Katika 1 Petro
3:7 tunasoma, “………kusudi kuomba kwenu kusizuiliwe.”
2. Majibu ya maombi
kutoka kwa Mungu mbinguni huzuiliwa ili yasimfikie muombaji duniani.
Aina hii ya kizuizi hufanywa na majeshi ya wakuu wa giza yaliyo
katika anga pia kwa ushirikiano na majeshi yaliyo katika ardhi na maji.
Muombaji anapofanikiwa kufanya maombi ya nguvu na hatimaye maombi yake
yakapasua anga na kumfikia Mungu, majeshi ya wakuu wa giza, huchukua nafasi
tena kuzuia mara ya pili ili majibu yaliyotoka kwa Mungu yasimfikie muombaji
aliye duniani. Katika kitabu cha Danieli 10:12-13 Biblia
inasema, “Ndipo akaniambia, usiogope, Danieli; kwa maana tangu siku ile ya
kwanza ulipotia moyo wako ufahamu, na kujinyenyekeza mbele za Mungu wako,
maneno yako yalisikiwa; name nimekuja kwa ajili ya maneno yako. Lakini mkuu wa
ufalme wa uajemi alinipinga siku ishirini na moja; bali tazama, huyo, Mikaeli,
mmoja wa hao wakuu wa mbele, akaja kunisaidia; nami nikamwacha huko pamoja na
wafalme wa Uajemi.” Kwa kawaida maombi yanapojibiwa na Mungu mbinguni,
maombi hayo huletwa duniani kwa mkono wa malaika kwa mfumo wa kifurushi, maana
malaika ni roho watumikao kwetu (Waebrania 1:14).
Katika aina hii ya pili ya kuzuiliwa kwa maombi ya watoto wa Mungu, vita huwa
kali sana kuliko ile ya kwanza. Majeshi ya wakuu wa giza hupambana na malaika
aliyebeba kifurushi cha majibu ya maombi ya muombaji, kwa lengo la kupora kile
kilichobebwa, ili kisimfikie mlengwa. Katika eneo hili, ushindi wa malaika huyo
katika vita hiyo, hutegemea sana na hali ya kiroho, aliyo nayo muombaji husika.
Kama mtu anayeomba anazo silaha zote za Mungu zinazotajwa katika kitabu
cha Waefeso 6:13-18, ni wazi kabisa malaika yule aliyebeba majibu
ya maombi ya muombaji huyo, atashinda vita katika anga, na kumfikishia muombaji
majibu yake.
Kama muombaji anakuwa hajavaa silaha zote za Mungu, na malaika atakayetumwa
kuleta majibu ya maombi, anakuwa hana hizo silaha, kama alivyo muombaji. Hiyo
humfanya malaika yule, kuporwa majibu ya muombaji husika. Silaha za kiroho
hazitulindi katika ulimwengu wa kimwili, bali zinatulinda katika ulimwengu wa
kiroho.
Malaika anaponyang’anywa majibu ya maombi na majeshi ya giza, siyo kwamba
malaika huyo anakuwa ameshindwa vita, la hasha; anayekuwa ameshindwa vita ni
muombaji na wala siyo malaika wala Mungu.
Kwa
kawaida majeshi ya giza hata yakikusanyika yote, hayana uwezo wa kumshinda
malaika wa Mungu mmoja. Kinachofanyika ni kwamba, uaminifu wa muombaji kwa
Mungu, ndiyo unaomfanya Mungu ahakikishe usalama wa kile anachomletea; lakini
pia, uzembe wa kiroho wa muombaji, ndiyo unaomfanya Mungu kuruhusu majeshi ya
giza yatimize makusudi yao dhidi ya majibu ya muombaji husika.
Ni sawa tu na Mkristo aliyemwamini Bwana Yesu, anapoenda kwenye mateso ya
jehanamu ya moto; siyo kwamba, Bwana Yesu kashindwa, bali aliyeshindwa ni
Mkristo mwenyewe. Mungu ameweka kanuni na miongozo ya kuifuata ili mtu afike
mbinguni, kwa hiyo anaposhindwa kufuata miongozo hiyo ni wazi hataiona mbingu.
Kadhalika, katika maombi, Mungu ameweka kanuni zitakazomwezesha mtoto wa Mungu
kupokea majibu ya maombi yake, hivyo mtu anapokosa kuzifuata kanuni hizo, ni
wazi atakosa kile ambacho amekiomba.
Majeshi ya wakuu wa giza yanafahamu wazi kwamba, muombaji anapokuwa na silaha
zote za Mungu, na malaika atakaye tumwa kuleta majibu ya maombi huwa na silaha
zote za Mungu. Wakishagundua malaika huyo ana silaha zote za Mungu, huogopa
kumshambulia; na hata kama wakimshambulia, hawataweza kushinda, hivyo malaika
huyo hufikisha majibu ya maombi kwa muombaji.
Malaika anapotumwa kutoka mbinguni kuleta majibu ya muombaji, majeshi ya wakuu
wa giza, watamchunguza malaika huyo ni silaha gani ambayo hana, na wanapogundua
hana silaha fulani, humshambulia katika maeneo hayo. Baada ya kumshambulia,
humpora majibu ya maombi aliyobeba. Kimsingi, majeshi ya giza hayana uwezo wa
kumharibu malaika huyo, bali wana uwezo wa kupora kile alichobeba. Na baada ya
hapo yule malaika hurudi mbinguni, hivyo muombaji anakuwa amekosa kupokea kile
alichoomba na pia kuwa chini ya mamlaka ya nguvu za giza.
Unaweza kujiuliza ni kwanini inakuwa hivi? Sababu kuu ni kwamba, Mungu mwenyewe
ameruhusu iwe hivyo; hiyo ni kanuni katika ulimwengu wa roho. Ni lazima watu
wafahamu kwamba, kila kitu katika ulimwengu wa kiroho kinaenda kwa kanuni. Na
Mungu wetu anaheshimu sana kanuni alizoweka.
MUUNDO WA FALME ZA WAKUU WA ANGA
NA UTENDA KAZI WAO
Ufalme wa giza katika anga, ngazi ya kimataifa, umegawanyika sehemu kuu nne;
sehemu ya kwanza ya ufalme wa anga katika falme na mamlaka za wakuu wa giza
inaitwa ufalme wa nyota. Sehemu hii ina kanda 900,000,000 na
pepo linalotawala kila kanda huitwa Deva, na mkuu wao katika
ufalme huu niSagna.
Sehemu ya pili ya ufalme wa anga una miungu 33,000,000. Pepo
linalotawala hapo huitwa Bavara. Sehemu ya tatu ya ufalme wa anga
huitwaUzura, ufalme huu hutawaliwa na Sat Kumara.
Na ufalme wa nne wa anga huitwa Kalami, ufalme huu ndiyo makao
makuu ya falme za giza, maana ndipo alipo mkuu wao, kiongozi mkuu katika eneo
hili ni shetani mwenyewe.
Wakuu
wa anga, wamegawanyika katika ngazi mbalimbali; wapo wakuu wa anga wa
mtaa/kijiji, wakuu wa anga wa wilaya au majimbo, wakuu wa anga wa mikoa, wakuu
wa anga wa nchi, na wakuu wa anga wa kimataifa. Mgawanyo wa wakuu wa anga
unategemeana na nchi na nchi, na kila ngazi kuna mkuu wao na majeshi yao.
Hata hivyo
kwa kawaida, inasemekana kwamba, kila mkuu wa anga wa mtaa/kijiji huwa na
mabodigadi 99, na kila bodigadi huwa na watumishi 1000wa
kumsaidia kazi bodigadi huyo. Na jumla ya idadi ya majeshi ya giza yanayohusika
na ulinzi katika kila anga la mtaa au kijiji ni askari wa kipepo36,270,600.
Uongozi huu wa ufalme wa anga katika mtaa, huakikisha kwamba maombi ya watoto
wa Mungu hayamfikii Mungu. Na wakiona nguvu ya uombaji imepamba moto katika
mtaa, hushirikiana na majeshi ya falme za giza katika ardhi na maji ili
kuwadhoofisha waombaji hao.
Nguvu
ya wakuu wa anga na majeshi yao, hutofautiana kati ya mtaa na mtaa, wilaya na
wilaya, mkoa na mkoa, nchi na nchi. Mkuu wa anga wa eneo fulani na majeshi yake
anaweza kuwa na nguvu kubwa kuzidi eneo lingine. Na mara nyingi hii inatokana
na asili ya eneo husika. Kwa mfano, eneo ambalo kuna asili ya uchawi, matambiko
na mambo ya kitamaduni, katika eneo hili, mkuu wa anga na majeshi yake huwa na
nguvu sana ya kuzuia maombi kuliko eneo lingine. Mtu anapofanya maombi katika
eneo kama hilo, huwa ni ngumu sana kupata mpenyo wa kimaombi.
Pia
maeneo ambayo, kulikuwa au kuna utawala mkubwa wa dini nyingine kama uislamu
n.k. mara nyingi anga la eneo hilo huwa zito sana kimaombi. Na ndiyo maana,
muombaji anaweza kutililika vizuri katika maombi katika eneo fulani, lakini
pindi akihamia eneo lingine nguvu ya kutililika kimaombi hupotea kabisa, na
hii, husababishwa na uhodari wa majeshi ya giza katika eneo mpya aliloamia
muombaji huyo.
Uzito wa anga na upinzani katika maombi, pia hutegemea na unyeti wa eneo hilo
kwa ufalme wa giza. Kwa mfano, kama eneo hilo ndiyo makao ya mkuu wa giza au ni
lango la kuzimu, eneo hilo huwa na ulinzi mkubwa sana wa mapepo, hivyo
kusababisha ugumu usio wa kawaida katika kuomba.
Kadhalika, kiongozi wa ufalme za giza, anaweza akawa anapita katika anga la eneo
fulani kwa kipindi fulani, ni wazi waombaji waliopo chini ya eneo hilo,
watapata shida sana, kutokana na nguvu ya kipepo inayomlinda kiongozi huyo
anayepita, lakini mara akishapita katika anga hilo, hali ya eneo hilo hurudi na
kuwa kawaida.
UTENDA KAZI WA WAKUU WA ANGA DHIDI YA MAOMBI YA WATOTO WA MUNGU
Laiti kama watoto wa Mungu wangefunuliwa na kuona upinzani uliopo katika
ulimwengu wa roho, kamwe wasingeomba kilegevu kama ilivyo sasa. Watu
wanachukulia maombi kama raha fulani.
Maombi ni kazi zaidi hata ya kazi ya zege, maombi ni vita kali sana, kuizidi
vita yoyote iliyowahi kupiganwa kimwili hapa duniani. Na ndiyo maana kiongozi
mkuu wa wokovu wetu, Bwana wetu Yesu Kristo alitumia muda mwingi sana katika
kuomba, aliomba usiku na mchana (Luka 6:12). Kuna wakati aliomba mpaka
jasho la damu likatoka (Luka 22:44).
Upinzani wa maombi ya watoto wa Mungu ni mkubwa sana, tofauti kabisa, na
wanavyofikiria watu. Muombaji anapoomba, maombi yake huanza kupata upinzani
katika ngazi ya mtaa. Na kama nilivyokwisha kufafanua hapo awali kwamba, mkuu
wa anga wa mtaa, huwa na mabodigadi 99 wa kumsaidia kazi, na katika mabodigadi
hao, kila mmoja ana walinzi 1000. Na katika mtaa, majeshi ya giza yanayotenda
kazi ni 36,270,600. Jaribu kuwaza! Je ni muombaji gani legelege
anaweza kufanikiwa katika upinzani wa namna hii? Ni kweli Mungu anatushindia,
lakini, kuna sehemu na sisi ya kuchukua hatua kama watoto wa Mungu. Na ndiyo
maana Bwana Yesu alitupa kielelezo kwa kufanya maombi yasiyo ya kawaida, Bwana
Yesu alitumia muda mwingi sana katika kuomba.
Kwa hiyo, muombaji anapofanikiwa kupenya kimaombi katika anga la mtaa au
kijiji, maombi yake yanaweza kupata upinzani tena na mkuu wa anga wa wilaya na
majeshi yake. Kama maombi hayo yatapata neema ya kupenya tena katika anga la
wilaya, maombi ya muombaji yanaweza kupata upinzani tena kwa mkuu wa anga wa
mkoa na majeshi yake. Na kama yakipata mpenyo katika anga la mkoa, maombi hayo
yanaweza kupata upinzani katika anga la kimataifa.
Katika
anga la kimataifa kuna mapepo yaliyo na nguvu isiyo ya kawaida. Hivyo, ni
maombi yenye moto wa Roho Mtakatifu, ndiyo yanayoweza kupasua anga na kumfikia
Mungu mbinguni.
Si hivyo tu, lakini maombi, yakifika mbinguni, Mungu huyatolea majibu. Baada ya
kutolewa majibu, malaika hupewa majibu hayo, ili kupeleka duniani kwa muombaji
husika. Katika hatua zote za kupeleka majibu, malaika pia hukutana na upinzani
wa wakuu wa anga katika ngazi zote, ili majibu hayo, yasimfikie mtoto wa Mungu.
Muombaji anaweza akawa na silaha zote za Mungu, pindi anapoomba, hivyo
kusababisha maombi yake kufika mbinguni. Lakini, wakati akisubiri majibu,
akiyumba kiroho na kupoteza baadhi ya silaha za Mungu, kama ngao ya imani n.k,
ni wazi kabisa, majibu yake hayatamfikia. Sababu kuu ni kwamba, malaika
atakayetumwa kuleta majibu, naye atakuwa hana ngao; hivyo kupelekea majeshi ya
giza katika anga, kumvamia kirahisi na kupora majibu ya maombi.
Ni kwa sababu hii basi, Bwana Yesu, katika kitabu cha Luka 21:36anasema,
“Basi, kesheni ninyi kila wakati, mkiomba, ili mpate kuokoka katika hayo
yote yatakayotokea, na kusimama mbele za mwana wa Adamu.” Katika Luka
18:1 Bwana Yesu anatuagiza, “Akawaambia mfano, ya kwamba imewapasa
kumwomba Mungu siku zote, wala wasikate tamaa.” Katika Wakolosai 4:2 Biblia
inasema, “Dumuni sana katika kuomba, mkikesha katika kuomba huku na
shukrani.”
JINSI YA KUFANYA ILI MAOMBI YETU
YAPATE KUPASUA ANGA
Ili maombi yaweze kupasua anga na kumfikia Mungu, inategemea sana kiwango cha kiroho
cha muombaji husika na maarifa sahihi katika kuomba. Siyo kila muombaji anaweza
kupata mpenyo katika anga. Ebu jaribu kujiuliza kwamba, ni Wakristo wangapi
katika nyakati za leo ambao wana hali ngumu sana ya kiuchumi, kiroho,
kifamilia, kimahusiano n.k? Na ukichunguza kwa makini, ni dhahiri kabisa
kwamba, Wakristo hao wanaomba kwa bidii sana. Swali lingine ni kwamba, kama
wanaomba kikamilifu, kwa nini hawapokei majibu yao?
SIFA ZA MUOMBAJI MWENYE UWEZO
WA KUPASUA ANGA KIMAOMBI
Zipo
sifa nyingi sana, zitakazomwezesha muombaji kupata kibali cha kufanya maombi
yake yasambaratishe upinzani wa wakuu wa anga, lakini zifuatazo, ni sifa kuu na
za msingi sana, na sifa zote zimebebwa ndani ya sifa hizi;
1. MUOMBAJI NI LAZIMA AWE
MTAKATIFU ALIYEKAMILIKA.
Ukamilifu wa muombaji, unamfanya shetani na majeshi yake kukosa sababu ya
kumshitaki muombaji kwa lolote. Katika kitabu cha 1Petro 5:8 Biblia
inasema, “Mwe na kiasi na kukesha; kwa kuwa mshitaki wenu Ibilisi,
kama simba angurumaye, huzunguka-zunguka, akitafuta mtu ammeze.” Pia Ufunuo
12:10 Maandiko yanasema, “Nikasikia sauti kuu mbinguni, ikisema,
sasa kumekuwa wokovu, na nguvu, na ufalme wa Mungu wetu, na mamlaka ya Kristo
wake; kwa maana ametupwa chini mshitaki wa ndugu zetu, yeye
awashitakiaye mbele za Mungu wetu, mchana na usiku.”
Ni kwa sababu hii basi, Bwana Yesu anatutaka tuwe wakamilifu kama Baba yetu wa
mbinguni alivyo mkamilifu; Mathayo 5:48, “Basi ninyi mtakuwa
wakamilifu, kama Baba yenu wa mbinguni alivyo mkamilifu.” Katika Walawi
19:2 tunasoma, “Nena na mkutano wote wa wana wa Israeli, uwaambie,
mtakuwa watakatifu; kwa kuwa mimi Bwana, Mungu wenu ni mtakatifu.”
Katika 1 Petro 1:16tunasoma, “Kwa maana imeandikwa, mtakuwa
watakatifu kwa kuwa mimi ni mtakatifu.” Waefeso 1:4, “Kama
vile alivyotuchagua katika yeye kabla ya kuwekwa misingi ya ulimwengu, ili tuwe
watakatifu, watu wasio na hatia mbele zake katika pendo.”
Kwa
ujumla, maombi ya mtakatifu, huwa ni manukano mbele za Mungu, hivyo, Baba yetu
wa mbinguni, huakikisha, majibu ya maombi hayo yanamfikia muombaji husika kama
ilivyokuwa kwa Danieli (Danieli 10:12-13). Maombi yanayoweza kupanda
mbele za Mungu ni maombi ya mtu mtakatifu tu kama Neno la Mungu linavyosema
katika kitabu cha Ufunuo 8:4, “Na moshi wa ule uvumba ukapanda
mbele za Mungu, pamoja na maombi ya watakatifu, kutoka mkononi mwa
malaika.”
2. MUOMBAJI NI LAZIMA AVAE
SILAHA ZOTE ZA MUNGU.
Kitabu cha Waefeso 6:11 Biblia inasema, “Vaeni
silaha zote za Mungu, mpate kuweza kuzipinga hila za Shetani.” Kadhalika
katikaWaefeso 6:13, Maandiko yanasema, “Kwa sababu hiyo twaeni silaha
zote za Mungu, mpate kuweza kushindana siku ya uovu, na mkiisha kuyatimiza
yote, kusimama.” Silaha hizo za Mungu ni kama ifuatavyo;
(i) Kujifunga Kweli (Waefeso
6:14)-
Mtoto wa
Mungu ni lazima akae na kujifunza kweli yote, amfuate Mungu katika kweli na
siyo kufuata mapokeo ya wanadamu. Kweli ni maagizo yote ya Mungu (Yohana
17:17). Kweli ya Neno la Mungu, inamfanya muombaji awe mkamilifu mbele za
Mungu. Wakristo katika kanisa la leo hawafundishwi kweli yote na wachungaji
wao, na hii imepelekea kanisa la leo kupoa sana kimaombi.
(ii) Kuvaa Dirii ya haki
(Waefeso 6:14)
Mtoto wa
Mungu ni lazima atembee katika haki, ukamilifu, utaua, unyoofu ili asipate
kushitakiwa na mshitaki na hatimaye maombi yake kuzuiliwa (1Petro 5:8;
Ufunuo 12:10).
(iii) Kuwa na utayari kwa ajili
ya Injili ya amani (Waefeso 6:15)-
Maandiko
katika 1 Wakorintho 9:16 yanasema, “Maana, ijapokuwa
naihubiri Injili, sina la kujisifia; maana nimewekewa sharti; tena ole
wangu nisipohubiri Injili.” Kutokuhubiri Injili, aidha kwa
kualika, kushuhudia, kugawa tracts n.k. ni kufanya dhambi ya kutotimiza wajibu,
hii inatufanya tuwe na hatia, na ni ole wetu tusipofanya hivyo. Nguvu ya Mungu
katika maisha yetu ya kiroho, inadhihirishwa, pale tunapokuwa tayari na
kuchukua hatua ya kuhubiri habari za Yesu, na amani ya Mungu, kwa watu wote.
(iv) Kubeba ngao ya Imani
(Waefeso 6:16).
Imani kwa
mtoto wa Mungu ni ngao ya kuweza kuizima mishare ya moto ya shetani. Ni lazima tufahamu
kwamba pasipo Imani haiwezekani kumpendeza Mungu (Waebrania 11:6). Pia
Mungu wetu anataka mwenye haki wake aishi kwa imani (Waebrania 10:38;
Wagalatia 3:11). Tunalindwa na nguvu ya Mungu kwa imani (1 Petro 1:5).
Imani yetu katika maombi ndiyo inayotufanya tupokee kile tunachokiomba.
(v) Chapeo ya wokovu (Waefeso
6:17).
Kuuishi
wokovu ni jambo la msingi sana kwa watoto wa Mungu. Wokovu wetu ni wa thamani
sana, kwa kuwa Mungu mwenyewe amegharamika kwa mateso kwa ajili ya kuwakomboa
wanadamu (Waebrania 2:3). Nguvu yetu ya maombi, inasababishwa na jinsi
tunavyoweza kuutunza wokovu tulioupokea.
(vi) Upanga wa roho ambao ni
Neno la Mungu (Waefeso 6:17).
Kwa kawaida
Shetani anamuogopa sana muombaji aliyejaa Neno la Mungu. Neno la Mungu ni zaidi
ya upanga wowote ukatao kuwili, na pia ni nyundo, kadhalika Neno la Mungu ni
moto (Waebrania 4:12; Yeremia 23:29).
Muombaji anapoomba, kwa kulitaja Neno la Mungu yaani ahadi za Mungu, shetani na
majeshi yake hutetemeka na kuogopa sana. Mungu analiangalia Neno lake apate
kulitimiza (Yeremia 1:12, hivyo muombaji anapoomba kwa kulitaja Neno la
Mungu yaani ahadi za Mungu, Mungu hushuka kupitia Neno lake na kufanya kile
kilichoombwa.
Muombaji asiyejaa Neno la Mungu, maombi yake ni dhaifu, na ni rahisi maombi
yake kupingwa na wakuu wa anga. Katika kitabu chaYohana 15:7 Biblia
inasema, “Ninyi mkikaa ndani yangu, namaneno yangu yakikaa ndani yenu,
ombeni mtakalo lote nanyi mtatendewa.”
3. MUOMBAJI NI LAZIMA AWE NA
UHUSIANO WA KARIBU SANA NA ROHO MTAKATIFU WAKATI WOTE.
Biblia
inasema kwamba, wanaoongozwa na Roho wa Mungu, hao ndiyo wana wa Mungu (Warumi
8:14). Kadhalika, Roho Mtakatifu hutusaidia udhaifu wetu katika kuomba,
maana sisi hatujui kuomba ipasavyo, na Yeye pia hutuombea (Warumi 8:26).
Tunapokuwa na uhusiano wa karibu sana na Roho Mtakatifu, Yeye hutufunulia
wakati mzuri wa kuomba, si hivyo tu, lakini hutufundisha namna nzuri ya kuomba
ili maombi yetu yasizuiliwe (Yohana 14:26) kwa kuwa Yeye ni msaidizi
ambaye Baba amemleta kwa ajili yetu (Yohana 14:16; 14:26; 15:26; 16:7).
Tukiwa na Roho Mtakatifu atatuwezesha kufanya yafuatayo;
1. Atatufundisha kuomba sawasawa na mapenzi ya Mungu (1Yohana
5:14).
2. Atatufundisha kuomba ipasavyo (Yohana 14:26; Yakobo 4:3).
3. Atakufanya tuzae matunda, hivyo kufanya maombi yetu yasizuiliwe(Yohana
15: 9-17).
4. Atatupa nguvu ya kusamehe wengine, hivyo kufanya maombi yetu
yasizuiliwe (Marko 11:25-26).
5. Atatuwezesha kuomba kwa kutumia Neno la Mungu, hivyo kufanya
maombi yetu yawe na nguvu ya kupasua anga (Yohana 15:7).
6. Atatuwezesha kuwa na mahusiano mazuri na familia zetu, maana
uhusiano mbaya na wake au waume zetu, hufanya maombi yetu kuzuiliwa (I
Petro 3:7).
7. Atatuwezesha tusiombe kwa unafiki, kwa kuwa kuomba kwa unafiki
kunasababisha muombaji asipokee chochote kutoka kwa Mungu (Mathayo
6:5-6)
8. Atatuwezesha kuwajali wahitaji, kwani mtu asiyejali maskini,
maombi yake hayawezi kusikiwa (Mithali 21: 13).
9. Atatuwezesha tuwe na imani katika kuomba (Marko 11:23-24).
10. Atatuwezesha kukaa katika
hali ya utakatifu wakati wote, kwani dhambi hufanya majeshi ya wakuu wa giza
kuzuia maombi yetu (Isaya 59:1-2).
11. Hutufanya tusiwe na
kiburi bali tuwe wanyenyekevu; mtu mwenye kiburi maombi yake huzuiliwa na wakuu
wa anga (Ayubu 35:12-13).
4. MUOMBAJI NI LAZIMA AWE NA
SIFA YA KUWA NA BIDII KATIKA KUOMBA, NA KWA MUDA MREFU NA KILA WAKATI.
Katika
kitabu cha Waefeso 6:18 Maandiko yanasema, “Kwa sala zote
na maombi mkisali kila wakati katika Roho, mkikesha kwa jambo hilo na kudumu
katika kuwaombea watakatifu wote.” KatikaWakolosai 4:2 Biblia
inasema, “Dumuni sana katika kuomba, mkikesha katika kuomba huku na shukrani”
Muombaji mwenye sifa ya kuomba kila wakati, ndiye anayeweza kupasua anga
kimaombi.
JINSI YA KUFANYA MAOMBI YA KUPASUA ANGA
Kuna hatua za msingi ambazo, Mkristo mwenye sifa za hapo juu, akizifuata,
atafanya maombi yake yawe na uwezo wa kupasua anga. Hatua hizi ni kama
ifuatavyo;
HATUA YA KWANZA
Kabla
hatujaanza kuombea jambo lolote lile, ni vema kwanza tukatafakari, na kumuuliza
Roho Mtakatifu, juu ya jambo tunalokwenda kuombea kama ni mapenzi ya yake au
la. Tutajichunguza wenyewe kwamba, hilo jambo tunalokwenda kumuomba Mungu, je!
Tunastahili kuliomba kwa wakati huo au la? au je! Hilo tunalotaka kumwomba
Mungu ni hoja yenye nguvu kwake? (Isaya 41:21; 43:26). Hapa ndipo
Wakristo wengi tunapofanya makosa kwenye uombaji. Kuwa na hoja yenye nguvu, ni
kitu cha msingi sana mbele za Mungu ili tupokee kile tunachoomba.
Maombi
ya Wakristo wengi yanapata upinzani kwa kuwa yanakuwa si hoja zenye nguvu mbele
za Mungu. Kumuuliza Roho Mtakatifu, kunaleta muongozo wa jinsi ya kuliombea
jambo fulani. Lolote tunaloliomba kwa Mungu sawasawa na mapenzi yake, Yeye
atusikia. Katika kitabu cha 1 Yohana 5:14 Biblia inasema, “Na
huu ndiyo ujasiri tulio nao kwake, ya kuwa, tukiomba kitu sawasawa na mapenzi
yake, atusikia.” Kwa hiyo ni wazi kabisa kwamba, tukiomba kinyume na
mapenzi yake Yeye hawezi kusikia.
Makundi mengi ya wanamaombi, huchukua hatua ya kuombea jambo fulani kama
walivyopokea maelekezo ya kuliombea kutoka kwa wahitaji, bila kuuliza kwa Roho
Mtakatifu kama ni sahihi kuliombea kwa namna hiyo au siyo sahihi. Kupata muongozo
wa kuliombea jambo fulani kutoka kwa Roho Mtakatifu, ni jambo la msingi sana,
kuliko kuliombea jambo moja kwa moja kama apendavyo aliyeleta jambo hilo.
Wengine wanaweza wakafunga na kuomba, kumuombea mtu fulani afanikiwe katika
biashara zake, wakati waombaji hao hawajui kama mtu huyu analipa fungu la kumi
na sadaka kwa uaminifu. Kumuombea mtu wa namna hii ni kupoteza muda.
Amani
inapochafuka katika nchi, watumishi wa Mungu wasikimbilie kuwaambia watu
waombee amani tu ya nchi hiyo bila kujua kwanza, chanzo cha uvunjifu wa amani
hiyo nini. Watumishi wa Mungu, ni lazima waanze kwa kumuuliza Mungu chanzo cha
uvunjifu wa amani hiyo. Hatupaswi kuliombea jambo lolote, bila kwanza
kulitafutia usahihi wa jambo lenyewe kutoka kwa Roho Mtakatifu.
Baada
ya kupata majibu kutoka kwa Mungu, ndiyo Wakristo wapewe muongozo wa nini cha
kuombea. Wakristo wanaweza kuombea amani, lakini kumbe, swala si kuombea amani
tu, bali taifa limemkosea Mungu, hivyo linapaswa kufanya maombi ya toba ili
taifa lipone (2 Nyakati 7:14). Taifa la Israeli lilipopigwa na watu wa
mji wa Ai, baada ya kuuliza kwa Bwana, Bwana alimfunulia Joshua kuwa tatizo
lilisababishwa na Akani mwana wa Zera, ambaye alikuwa ameiba hazina ya Mungu (Yoshua
7:1-26). Baada ya kugundua chanzo cha tatizo, wakapata muelekeo wa nini
waombee na kipi wanapaswa kufanya.
Swala
kama hili, lilitokea kule Burudi miaka ya nyuma. Mwaka 1989, mwezi wa kumi, saa
kumi na mbili asubuhi, Mtumishi wa Mungu Emmanueli Lazalo, alipewa ujumbe na
Mungu juu ya kuharibiwa kwa Burundi na Tanzania kwa sababu ya uovu mkubwa.
Ujumbe huo ulisema, “TANZANIA HAITAWEZA KUSIMAMA KATIKA SIKU YA KUPIMWA KWAKE,
WALA BURUNDI NAYO.”
Watu
walipuuza na kuusahau ujumbe huu. Unabii huu ulikuja kutimia kwa Burundi,
vurugu zilipokaribia kuanza katika nchi hiyo, watumishi wa Mungu walianza
kuombea amani, badala ya kutangaza maombi ya toba kwa nchi nzima. Maombi ya
kuombea amani kwa nchi ya Rwanda na Burundi, hayakuleta majibu, kwa kuwa
waliomba kinyume na Mungu alivyotaka. Mungu alimtumia Mtumishi wake Emmanueli
Lazalo ili watu watubu, lakini hao wakafanya kinyume.
Moja ya vitu vya msingi ambavyo muombaji anatakiwa kufanya ni kumuuliza Roho
Mtakatifu kabla ya kuanza kuombea jambo lolote ambalo anaona haliko wazi kwake
au hajui chanzo chake. Lengo la kumuuliza Roho Mtakatifu, ni kuhakiki nini
kimpendezacho Mungu ili aombee jambo hilo kwa usahihi. Katika kitabu cha Waefeso
5:10 Biblia inasema, “Mkihakiki nini impendezayo Bwana”
Kumuuliza Roho Mtakatifu ni maombi ya kutafuta taarifa kamili au muongozo, ili
muombaji aweze kupata ushirikiano mzuri na Roho wa Mungu. Wachungaji wengi
hawakufanikiwa kwa sababu hawakuuliza kwa Bwana kama Biblia inavyosema
katika Yeremia 10:21, “Kwa sababu wachungaji wamekuwa kama
wanyama, wala hawakuuliza kwa Bwana; basi hawakufanikiwa, na makundi yao yote
yametawanyika.” Kama watoto wa Mungu tunapaswa kumwita Mungu ili atuonyeshe
mambo makubwa na magumu tusiyoyajua kama maandiko yanavyosema katika Yeremia
33:3, “Niite, nami nitakuitikia, nami nitakuonyesha mambo makubwa,
magumu usiyoyajua.”
Baada ya
waombaji kuhakikisha kwamba, maombi wanayokwenda kuomba ni mapenzi ya Mungu, na
wana muongozo katika kuliombea jambo hilo, basi hawana budi kufuata hatua ya
pili.
HATUA YA PILI
Kabla
hatujaingia kwenye kipindi cha maombi maalum, aidha ya muda mfupi au muda
mrefu, ni lazima tuchukue hatua ya kufanya maandalizi binafsi ya kiroho siku au
masaa au dakika kadhaa kabla ya kuingia kwenye maombi hayo. Kusudi kuu la maandalizi
haya, ni kututengenezea mazingira ya kutufanya tuwe rohoni sana, maana vita
vyetu ni katika ulimwengu wa roho (Waefeso 6:12).
Mtu
anapoingia kwenye maombi, yawe ya muda mfupi au ya muda mrefu bila maandalizi,
muombaji huyo atachoka na kukata tamaa, atakosa matumaini, na anaweza akaishia
njiani bila kukamilisha maombi hayo, kwani atapata uzito na upinzani mkubwa
sana katika ulimwengu wa roho.
Maandalizi haya yanajumuisha toba ya kumaanisha katika maeneo ambayo tumemkosea
Mungu bila kukusudia, kwa kuwa Mkristo wa kweli hafanyi dhambi kwa kukusudia.
Maandalizi haya, pia yanajumuisha, utengenezaji wa mahusiano yetu na Roho
Mtakatifu, maana bila Yeye, hatuwezi kufanikiwa katika maombi (Warumi 8:26).
Katika kipindi hiki cha maandalizi, tunapaswa kutumia muda wetu wote,
kujinyenyekeza mbele za Roho Mtakatifu, tukijieleza mbele zake kwa unyenyekevu
na upole, tukimbembeleza awe pamoja nasi, huku tukimwomba msamaha kwa machozi
maeneo ambayo tumemuhuzunisha, na kumsihi atusaidie tusimuhuzunishe tena,
tukimwomba atutie nguvu na kutufundisha kuomba ipasavyo. Tutamwambia Roho
Mtakatifu kuwa bila Yeye sisi hatuwezi kufanya chochote. Roho Mtakatifu siyo
nguvu fulani kama wanavyodhani wengi, bali ni nafsi hai ya Mungu (Soma kitabu
changu kinachoitwa ‘Roho Mtakatifu na utenda kazi wake’).
Kutenda kazi
na Roho Mtakatifu kunahitaji ufahamu wa ziada, asilimia 99.9 ya Wakristo bado
hawajajua namna ya kwenda na Roho Mtakatifu. Baada ya Bwana Yesu kuondoka
kwenda mbinguni, akatuachia Mungu Roho Mtakatifu akae pamoja nasi hapa duniani,
bila Yeye kamwe hatutaweza kufanya chochote (Yohana 14:16; 14:26; 15:26;
16:7).
Kadhalika, katika kipindi hiki cha maandalizi, muombaji anapaswa
kutumia muda mwingi peke yake, ili apate kuwa na muda mwingi wa kuzungumza na
Roho Mtakatifu. Muombaji anapaswa kuepuka mazingira yoyote yatakayomfanya
ufahamu wake kurudi mwilini au kumuhuzunisha Roho Mtakatifu.
Kwa maombi ya muda
mfupi, muombaji anapaswa kufanya maandalizi, masaa au dakika kadhaa, kabla ya
kuingia kwenye maombi hayo. Maandalizi hayo yatamfanya muombaji apate utayari
wa kuomba. Maandalizi kwa muombaji, yatamfanya apate muunganiko katika
ulimwengu wa roho.
Baada ya
maandalizi haya, muombaji; kwanza, atajisikia amani ya ajabu moyoni mwake;
pili, atasikia furaha ya namna ya kipekee; tatu, atasikia uwepo wa Mungu usio
wa kawaida; nne, atasikia hamu kubwa ya kuomba; tano, atasikia uamsho wa nguvu
kubwa sana ya maombi.
ANGALIZO
Kwa
kuliombea tatizo la ghafla, hatuna budi kujitakasa wakati huo huo na kuingia
moja kwa moja kwenye maombi, hapa hatuhitaji maandalizi ya siku au masaa
kadhaa. Mara nyingi tatizo lolote la ghafla, kwa asili hutufanya tuende mbele
za Mungu kwa unyenyekevu, hivyo kutufanya tuingie kwenye ulimwengu wa roho kwa
wepesi sana, kulingana na uchungu tunaoupata kutokana na tatizo hilo.
HATUA YA TATU
Baada
ya kufuata hatua ya kwanza na ya pili kwa uaminifu, muombaji hana budi sasa
kuingia kwenye maombi, akiwa na imani timilifu ya kupokea kile anachokwenda
kuomba, huku akifuata vipengele vifuatavyo;
1. KUFANYA TOBA KAMILIFU.
Kabla ya kuanza kipindi cha maombi, muombaji atafanya maombi ya toba. Ni vema
ikumbukwe kwamba, toba inayofanywa hapa ni kwa dhambi ambazo tumezifanya bila
sisi kujua au kukusudia. Sisi kama watoto wa Mungu, hatupaswi kufanya dhambi
kwa makusudi ili tutubu, dhambi za namna hii huwa hazisamehewi. Maandiko
katika Waebrania 10:26 yanasema, “Maana, kama tukifanya
dhambi kusudi baada ya kupokea ujuzi wa ile kweli, haibaki tena dhabihu kwa
ajili ya dhambi; bali kuna kuitazamia hukumu yenye kutisha, na ukali wa moto
ulio tayari kuwala wao wapingao.”
2. KUMSHUKURU MUNGU KWA YOTE
ALIYOTENDA.
Hatuwezi kuwa watu wa kuomba tu, bila kuwa watu wa shukrani kwa yale mambo
kadhaa ambayo Mungu ametenda kwetu. Na ndiyo maana Neno la Mungu katika Wakolosai
3:15 linasema, “.........tena iweni watu wa shukrani.” Ni jambo
linalompendeza Mungu wakati wote, pale tunapoanza kumshukuru, kabla ya kuanza
kuomba mambo mengine mapya. Mtume Paulo katika nyaraka zake zote, kwanza
kabisa, anaanza na kumshukuru Mungu (Filemoni 1:4; 2 Timotheo 1:3; 1
Timotheo 1:12; 2 Wathesalonike 1:2; 1:13; 5:18; Wakolosai 1:3; 1:12 ; 3:17;
Wafilipi 1:3; 4:6; Waefeso 5:4; 5:20; 1 Wakorintho 1:4; 1:14; Warumi 1:8).
Kwa hiyo, kabla hatujaanza kuyaombea yale yaliyokusudiwa kuombewa katika siku
hiyo, ni vema kwanza, tukitumia dakika kadhaa, katika kumshukuru Mungu kwa yale
ambayo amefanya.
Kitendo cha mimi na wewe kuwa wazima na afya njema kwa wakati huo wa maombi,
hiyo ni neema, hatuna budi kumshukuru Mungu. Kitendo cha kupata neema ya
kukusanyika katika maombi kwa wakati huo, hiyo ni neema, hivyo hatuna budi
kumshukuru Mungu. Kitendo cha mimi na wewe kuwapo kwenye nchi ya amani na hata
kupata nafasi ya kuomba kwa amani bila vurugu, hiyo ni neema, ni lazima
tumshukuru Mungu. Kwa ujumla, yapo mambo mengi ambayo tunaweza kumshukuru Mungu
na kumwinua kwa ajili ya hayo aliyotenda. Na baada ya kumshukuru Mungu na
kumwinua kwa yake aliyotutendea, hatuna budi, kwenda kwenye kipengele
kifuatacho.
3. KUOMBA KUMWAGIWA ROHO WA
NEEMA NA KUOMBA.
Baada ya kumshukuru Mungu, kabla hatujaanza kupeleka hoja zetu mbele za Mungu (Isaya
41:21), kwanza, tutamwomba Bwana atumwagie Roho wa Neema na Kuomba kama
maandiko yanavyosema katika Zekaria 12:10, “Nami nitawamwagia
watu wa nyumba ya Daudi, na wenyeji wa Yerusalemu, roho ya neema na kuomba;
nao watamtazama yeye ambaye walimchoma……..” Roho wa Neema na Kuomba ndiye
Roho Mtakatifu anayetusaidia udhaifu wetu katika kuomba, kwa kuwa sisi hatujui
kuomba jinsi ipasavyo (Warumi 8:26).
4. KUANZA KUOMBA HUKU
TUKITUMIA JINA LA YESU NA KUZITAJA AHADI ZA MUNGU (NENO).
Baada
ya kumwalika Roho Mtakatifu, muombaji anaweza kuendelea kuomba yale ambayo
amepanga kuyaomba katika kipindi hicho cha maombi. Muombaji ni lazima aombe kwa
Baba kwa Jina la Yesu. Wengi wanafanya maombi bila kutumia Jina la Yesu. Baba
wa mbinguni hawezi kutufanyia jambo lolote tunapomwomba, kama hatutatumia jina
la Yesu katika maombi yetu. Bwana Yesu katika kitabu cha Yohana 16:23 anasema, “Tena siku
ile hamtaniuliza neno lolote. Amin, amini, nawaambia, mkimwomba Baba neno
lolote atawapa kwa jina langu.” Pia katika Yohana 14:14 Bwana
Yesu anasema, “Nanyi mkiniomba lolote, kwa jina langu, hilo nitalifanya, ili
Baba atukuzwe ndani ya mwana. Mkiniomba neno lolote kwa jina langu, nitalifanya.”
Maombi
yoyote, yasiyoenda na muhuri wa jina la Yesu, ni rahisi kuzuiliwa na majeshi ya
giza, na mara zote maombi haya huwa hayana majibu. Kwa ujumla sala, maombi au
dua yoyote isiyohusisha jina la Yesu, hiyo siyo sala na haina faida yoyote.
Pia wakati wa
maombi, muombaji anapaswa kutumia Neno la Mungu yaani kuzitaja ahadi za Mungu
kulingana na hitaji husika. Kwa kawaida Mungu analiangalia Neno lake ili apate
kulitimiza (Yeremia 1:12), hivyo muombaji anapotaja ahadi alizotoa Mungu
katika Neno lake kulingana na jambo analoombea, jambo hilo hufanyika kwa
haraka, na majeshi ya wakuu wa giza, huwa hawawezi kuzuia, maana Neno la Mungu
ni moto (Waebrania 4:12; Yeremia 23:29).
5. KUSHINDANA NA WAKUU WA
GIZA.
Baada ya
muombaji kumaliza kupeleka hoja zake zote mbele za Mungu, hatua inayo fuata ni
kufanya maombi ya kushindana na wakuu wa giza katika anga. Muombaji anapofanya
maombi ya kushindana na wakuu wa anga, ni lazima awe amesimama. Maombi haya,
yana makusudi ya kupiga majeshi ya wakuu wa giza ili kuwafanya wasizuie maombi
yako (Waefeso 6:12).
Haya ni
maombi ya vita ili kuwatawanya na kuwasambaratisha majeshi ya wakuu wa giza.
Silaha yoyote itakayotamkwa na muombaji ili kupiga majeshi ya wakuu wa anga ni
lazima itumwe kwa jina la Yesu. Kwa mfano, unapotuma moto wa Roho Mtakatifu, ni
lazima utume kwa muhuri wa jina la Yesu. Muombaji anapofanya maombi haya, ni
lazima ufahamu wake utulie katika mapambano hayo. Kumaanisha kwa muombaji
anapotuma makombora, ndiko kunakomfanya ayashinde majeshi hayo. Ni lazima
tukumbuke kwamba, chochote tunachotamka na kufanya wakati huu katika ulimwengu
wa mwili, katika ulimwengu wa roho, hufanyika hivyo hivyo.
Shetani hutumia muda
huu, kuwateka ufahamu waombaji wanaoshindana. Muombaji anaweza kujikuta
anashindana kwa mdomo tu, lakini mawazo yake yakawa kwenye kitu kingine.
Tunapokuwa katika maombi haya, tuhakikishe tunakuwa katika mazingira, yenye
kutufanya, tusihame kiufahamu. Tukizingatia haya, tunashinda na zaidi ya
kushinda (Warumi 8:37).
6. KUJIFUNIKA KWA ULINZI WA
MUNGU.
Muombaji akifanya maombi haya ya kushindana na wakuu wa giza kikamilifu, ufalme
wa shetani unakuwa umeharibiwa sana. Hivyo, shetani mara zote hupanga mipango
ya kuja kulipiza kisasi kwa muombaji husika. Ni lazima ifahamike kwamba kuna
mapepo ya kisasi (Spirits of vengeance), kazi ya mapepo haya, ni kulipiza
kisasi kwa yoyote ambaye ameharibu ufalme wa giza. Mapepo haya, yana silaha
nyingi, na mbinu mbalimbali za kulipiza kisasi kwa maadui zao. Hivyo ni
jukumu la kila muombaji, kujifunika kwa ulinzi wa Mungu baada ya kufanya maombi
haya.
Mapepo
hawa huweza kumvamia muombaji, na kumpiga kwa homa kali, kuwashwa mwili,
kuharisha, kizunguzungu na mengine mengi. Muombaji asipokuwa makini, anaweza
asirudi tena kwenye maombi. Kwa hiyo unaposikia hali yoyote tofauti baada ya
kutoka katika maombi haya, usiogope, endelea kukemea kwa jina la Yesu, huku
ukiamini kwamba unalindwa na nguvu ya Mungu kwa imani (1 Petro 1:5). Pia
unaweza ukashangaa kuona wale waliokuwa wanakudai siku nyingi ambao walitulia
kukusumbua, siku hiyo ndiyo wanakuja kwa kasi au kukupigia simu ili kukudai
pesa. Yanapotokea haya, usiyaogope, ujue wazi kabisa, umeuharibu sana ufalme wa
giza.
Mapepo
hawa wanaposindwa kumpiga muombaji husika, huvamia watoto au mume/mke au ndugu
wa karibu wa muombaji, unaweza ukarudi nyumbani na ukashangaa kuona mafarakano
yasiyo ya kawaida na familia yako au majirani. Pia majeshi haya huweza kuvamia
hata biashara na miradi mbalimbali na kuharibu.
Ni kwa
sababu hii basi, muombaji anapomaliza kufanya maombi ya kushindana, anapaswa
kujifunika yeye mwenyewe, familia yake, miradi yake, huduma yake, mahusiano
yake, vyakula, vinywaji, hewa unayovuta, pamoja na vyote alivyo navyo kwa damu
ya Bwana wetu Yesu Kristo. Mapepo wanaogopa damu ya Yesu Kristo, hivyo
unapojifunika kwa imani, unakuwa salama.
Pia ni
lazima uombe ulinzi kwa jina la Yesu huku ukitaja ahadi za Mungu kuhusu ulinzi;
baadhi ya ahadi hizo ni kama ifuatavyo; Isaya 54:17 Mungu
ameahidi kwamba, “Kila silaha itakayofanyika juu yako haitafanikiwa, na kila
ulimi utakaoinuka juu yako katika hukumu utauhukumu kuwa mkosa. Huu ndiyo
urithi wa watumishi wa Bwana, na haki yao inayotoka kwangu mimi, asema Bwana.” Zaburi
34:7 Neno la Mungu linasema, “Malaika wa Bwana hufanya kituo,
akiwazunguka wamchao na kuwaokoa.” Zekaria 2:8Neno la Mungu
linasema, “Kwa maana Bwana wa majeshi asema hivi, ili nitafute utukufu
amenituma kwa mataifa wale waliowateka ninyi; maana yeye awagusaye ninyi aigusa
mboni ya jicho lake.” Walawi 26:7 Mungu ameahidi kwamba, “Nanyi
mtawafukuza adui zenu, nao wataanguka mbele zenu kwa upanga.”
7. KUMSHUKURU ROHO WA NEEMA
NA KUOMBA (ZEKARAI 12:10).
Roho wa Neema na Kuomba ndiye Mungu Roho Mtakatifu (Zekaria 12:10).
Hivyo kama tulianza naye, hatuna budi kumaliza naye kwa kumshukuru kwa neema ya
kipekee aliyotupa katika kuomba (Zaburi 109:30). Baada ya kumshukuru
Roho Mtakatifu, pia ni vema kumwomba, atupe neema ya kuwepo tena siku
inayofuata kwa ajili ya maombi, na kumsihi awe pamoja nasi katika kila hatua
tunayokwenda kupiga.
Baada
ya kufanya hayo yote kwa ukamilifu na kwa unyenyekevu, ni wazi kabisa maombi
yako yatakuwa na nguvu kubwa ya kusambaratisha majeshi ya wakuu wa giza
na kupasu anga, hatimaye kumfikia Mungu.
MUDA UNAOTAKIWA KATIKA KUFANYA MAOMBI
YA KUPASUA ANGA
Ili maombi yetu yapate kutikisa majeshi ya wakuu wa anga, muda wa kufanya
maombi hayo, ni kitu cha kuangaliwa sana. Biblia haitupi muda maalum wa kuomba,
ingawa tukiwaangalia waombaji mashuhuri katika Biblia, inaonesha wazi kwamba,
walitumia muda mrefu sana katika kuomba. Katika 1 Samweli 15:10-11 tunaona
Samweli aliomba usiku kucha. Katika Luka 6:12tunaona pia Bwana Yesu
aliomba usiku kucha. Danieli aliomba mara tatu kila siku (Danieli 6:10).
Daudi naye vivyo hivyo aliomba kwa machozi asubuhi, mchana na jioni (Zaburi
55:17). Tukimwangalia Nabii mke Ana binti Fanueli, yeye siku zote alikuwa
hekaluni akiomba usiku na mchana (Luka 2:36-37). Yakobo alimng’ang’ania
malaika usiku kucha ili kupata Baraka (Mwanzo 32:24-30). Ili
kurudisha mvua inyeshe, Eliya aliomba mara saba (1 Wafalme
18:41-45). Paulo aliomba mchana na usiku (2 Timotheo 1:3; 1
Wathesalonike 3:10). Kwa hiyo, tukiwaangalia waombaji hawa na wengine
waliotumiwa sana na Mungu katika zama za Biblia, inadhihirisha wazi kwamba kwa
siku, walitumia masaa mengi katika kuomba.
Hata hivyo, tukichunguza kwa makini, juu ya muda wa kuomba,
ambao umesisitizwa katika maandiko, tunagundua kwamba, ni sehemu nyingi katika
Biblia, maandiko yanatuambia juu ya kukesha katika kuomba (Luka 21:36;
Wakolosai 4:2; Waefeso 6:18; 1 Wakorintho 16:13; Marko 13:37; 2 Wakorintho 6:5;
Marko 13:35; Marko 13:33; Mathayo 26:41; Mathayo 26:38; Mathayo 25:13; Mathayo
24:42; Marko 14:38; Marko 14:38; Ufunuo 3:2; Ufunuo 16:15; 1 Petro 5:8; 1
Wathesalonike 5:6). Na neno kukesha katika kuomba maana yake, ni kitendo
cha kukaa macho usiku wote huku mtu akiwa anaomba. Sasa tujiulize, Je! Usiku
una masaa mangapi? Usiku una masaa tisa (9). Muombaji mwenye uwezo wa kuomba
masaa tisa kwa siku, ni wazi kabisa Mkristo huyo atakuwa si wa kawaida katika
ulimwengu wa roho. Maombi ya mtu wa namna hii, majeshi ya giza hayawezi
kuhimili kuyazuia.
Hata hivyo,
Bwana Yesu katika Mathayo 26:40 aliwaambia wanafunzi wake,“…...Je!
Hamkuweza kukesha pamoja nami hata saa moja?” Kwa kusema ‘hata
saa moja’ Bwana Yesu hapa, alimaanisha kuwa, saa moja, ndicho kiwango cha
chini cha muda wa kuomba. Hivyo kwa muombaji mchanga aombe muda usiopungua saa
moja kwa siku. Lakini kwa muombaji mwenye karama ya uombaji, kipimo cha chini
cha uombaji ni karibu wastani wa masaa 4 kwa kila siku.
Huduma ya
Campus Crusade for Christ, yenye makao makuu huko Arrowhead Springs, Califonia
nchini Marekani ina watendakazi wanane (8) ambao maisha yao yote, ni maombi,
hawana kazi nyingine ya kufanya. Watendakazi hawa, hukutanika kila asubuhi
kanisani na kuomba kwa masaa nane (8) mfululizo bila kupumzika kila siku. Pia
kuna muombaji mwingine aitwaye Mrs Bernice Watne wa Eagle Grove, Iowa,
Marekani, muombaji huyu ni kilema anayetembelea wheelchair, lakini huomba masaa
4 kwa siku, na anasema anaifurahia hali hiyo ya ulemavu kwani inampa nafasi
kubwa ya kuomba.
KWA NINI MUOMBAJI ANAPASWA KUOMBA MASAA MENGI KWA SIKU ILI
KUPASUA ANGA?
Tulijifunza
hapo nyuma kwamba, mara zote, wakati Wakristo walio wakamilifu na wenye imani,
wanapoanza kuomba, maombi yao huwa kama moshi na unapanda juu taratibu, lakini
wanapoendelea kuomba, maombi yao hubadilika na kuwa kama moshi unaokwenda kwa
kasi juu na ulionyooka. Na mara wakiendelea kuomba, ghafla huanza kulipuka na
kugeuka kuwa moto. Moto huu, ndiyo unaounguza utando wa kipepo katika anga
unaozuia maombi ya Wakristo yasimfikie Mungu. Na maombi yao huwa na nguvu sana,
na hata kusababisha kupasua kizuizi kilichowekwa na wakuu wa giza, na hatimaye
maombi hayo kufika kwa Mungu.
Sasa hatua zote
hizi, mpaka maombi kugeuka kuwa moto, muombaji anapaswa kutumia masaa mengi
katika kuomba, ili maombi yapate kupasua anga la mtaa, anga la wilaya, anga la
mkoa, anga la Taifa na anga la kimataifa, hatimaye kumfikia Mungu. Maombi ya
muombaji yakigeuka kuwa moto, muombaji anapaswa kuendelea kuomba, ili
kuhakikisha moto huo hauzimiki. Mara akikatiza maombi tu, moto huzimika na
kufanya maombi yake kuzuiliwa na wakuu wa anga.
NI WAKATI UPI MZURI WA KUFANYA MAOMBI?
Wakati wote
ni wakati mzuri wa kuomba, cha msingi ni kwamba, pale unaposikia haja ya kuomba
ni vema ukaanza kuomba. Zaburi 32:6 Maandiko yanasema, “Kwa
hiyo kila mtu mtaua akuombe wakati unapopatikana.” Maandiko katika kitabu
cha Waefeso 6:18 yanasema, “Kwa sala zote na maombi mkisali
kila wakati katika Roho, mkikesha kwa jambo hilo na kudumu katika kuwaombea
watakatifu wote.” Lakini hata hivyo, tutapata ushindi zaidi kama tutakuwa
na utaratibu wa kuomba kila siku, usiku na mchana. Kitabu cha Luka 18:7 Biblia
inasema, “Na Mungu, je! Hatawapatia haki wateule wake wanaomlilia mchana na
usiku naye ni mvumilivu kwao?”
UMUHIMU WA MAOMBI YA USIKU NA ALFAJIRI
Sisi kama watoto wa Mungu, hatuna budi kufahamu kwamba, Shetani ni mfalme wa
GIZA. Wasaidizi wake wanaitwa wakuu wa giza (Waefeso 6:11-12). Nguvu za
Shetani zinaitwa NGUVU ZA GIZA (Wakolosai 1:13). Kwa hiyo, ni muhimu
kufahamu kwamba Shetani hufanya kazi zaidi usiku kuliko mchana.
Dhambi
nzito na uharibufu mkubwa hufanywa zaidi usiku. Uzinzi, uasherati, wizi,
uchawi, ulevi, kucheza dansi, ujambazi, unyang’anyi na mambo mengi machafu
hufanywa usiku.
Mipango yote ya shetani hufanywa USIKU. Kazi za shetani
zinazodhihirika mchana wote, hutokana na mipango ya shetani iliyopangwa usiku
uliotangulia. Ukiona mtu amegongwa na gari mchana, huo mpango ulipangwa usiku
uliotangulia. Mipango ya kumsaliti Bwana Yesu, ilipangwa usiku na kutekelezwa
mapema alfajiri. Mipango ya kumshambulia Daudi ilikuwa usiku pia (2 Samweli
17:1-2).
Wakuu wa
giza hufanya mipango yao ya uharibifu usiku, hivyo nasi kama tutakuwa macho
usiku na kuvunja mipango hiyo, au kuamka alfajiri na mapema na kubomoa mipango
yao yote kwa maombi, ushindi hupatikana siku mzima. Licha ya kuomba kabla ya
kulala, lakini ni muhimu sana kuomba usiku au alfajiri na mapema. Kutokuomba
usiku au alfajiri na mapema ni kuruhusu mipango ya shetani, siku hiyo
itekelezwe kwetu binafsi na kwa kanisa lote.
Shetani anaogopa
sana maombi ya usiku na alfajiri, hivyo hufanya kila jinsi kuyazuia
yasifanyike. Kama Wakristo, hatuna budi kumpinga mpaka akimbie (Yakobo 4:7).
ALFAJIRI ni wakati wowote baada ya saa kumi usiku, mpaka wakati ule ambao bado
kuna giza na haijawa hata asubuhi.
Kumpinga
kwetu shetani ili asituzuie kufanya maombi ya usiku na alfajiri, hakuna budi
kuambatane na jitihada zetu binafsi za kimwili. Tukishiba kupita kiasi, ni wazi
hatutaweza kuamka usiku au alfajiri na mapema kwa ajili ya maombi. Usiku tule
kwa kiasi na tunywe maji mengi sana, hii kwa kiasi inaweza kutusaidia kuamka.
Hata hivyo, yupo Roho Mtakatifu, msaidizi wetu (Yohana 14:16; 14:26; 15:26;
16:7), kama tutakuwa waaminifu kwake, yeye atatusaidia kutuamsha usiku
katika wakati unaofaa zaidi. Kuomba usiku na alfajiri, kunahitaji kujitia
nidhamu na kusema ‘Lazima niamke kwa jina la Yesu’ na kuyakatalia
matakwa ya mwili unaosaidiana na Shetani kuzipinga roho zetu (Wagalatia
5:16-17).
ANGALIZO: ALFAJIRI ni wakati wowote baada ya saa kumi usiku, mpaka
wakati ule ambao bado kuna giza na haijawa hata asubuhi.
MIFANO YA WATAKATIFU WALIOFANYA
MAOMBI YA USIKU NA ALFAJIRI
1. YAKOBO-Yakobo hatimaye aliitwa Israeli kwa sababu alishindana na Mungu
na watu na kuwa mshindi (Mwanzo 32:28). Hata hivyo ushindi wake ulianzia
katika maombi ya alfajiri alipokuwa akiomba na kuweka nadhiri zake (Mwanzo
28:18-22).
2. SAMWELI-Samweli aliomba na kumlilia Mungu usiku kucha yaani usiku na
alfajiri (1 Samweli 15:10-11).
3. BWANA YESU-Bwana Yesu mara nyingi aliomba usiku kucha yaani usiku na
alfajiri (Luka 6:12; Mathayo 4:2; Marko 1:35).
4. WAZAZI WA SAMWELI-Wazazi wa Samweli, waliweza kufanikiwa kumzaa mtoto Samweli
aliyekuwa nabii wa kipekee, kutokana na wao kuzingatia maombi ya alfajiri (1
Samweli 1:19). Sisi nasi tukizingatia maombi ya alfajiri au uziku, tutaona
mambo makuu katika maisha yetu.
5. HEZEKIA-Hezekia naye aliomba maombi ya alfajiri (2 Nyakati 29:20).
Hezekia aliongezewa maisha alipokuwa katika kufa, na Mungu alimjua kama Hezekia
alikuwa mwaminifu kwake kutokana na kujikana na kufanya maombi ya alfajiri.
Maombi yake ya alfajiri yalimpa ushindi dhidi ya mkono wa mfalme wa Ashuru (2
Wafalme 20:1-6).
6. DAUDI-Daudi pia alifanya maombi ya alfajiri (Zaburi 57:8; 119:147).
Ushindi mkubwa wa mfalme Daudi ulitokana na kuzingatia maombi ya alfajiri na
usiku.
7. PAULO-Maombi ya usiku yalimfanya Paulo kutumiwa na Mungu kipekee
kuliko mitume wengine. Siri kuu ni maomba ya usiku (2 Timotheo 1:3; 1
Wathesalonike 3:10).
NGUVU YA MAOMBI YA KUFUNGA
Katika
kitabu cha Mathayo 17:14-21 Maandiko yanasema, “.........Lakini
namna hii haitoki ila kwa kusali na KUFUNGA.” Katika mistari hii, Bwana
Yesu anatufundisha kwamba, yako mambo ambayo hayawezekani kama mtu ataomba tu
bila ya kufunga.
Mkristo anaweza akaomba kwa ajili ya jambo fulani kwa muda mrefu, lakini bado
upo uwezekano wa Mkristo huyo, kutopokea chochote, endapo kama maombi yake
yatakuwa hayaambatani na kufunga. Kwa hiyo, ni jambo la msingi kwa kila mtoto
wa Mungu kujifunza, jinsi ya kufunga ipasavyo.
MAANA YA KUFUNGA
Neno “Kufunga” linatokana na neno la Kiyunani linaloitwa “Nestevo.”
Kadhalika neno ‘Nestevo’ nalo linatokana na maneno mawili ya Kiyunani
ambayo ni “Ne” na “Esthio” Neno “Ne” maana yake ni “Bila”
au “Hapana”, Kwa kiingereza ni “No” au “Without’. Neno “Esthio”
maana yake “Kula chakula au kinywaji”, kwa Kiingereza ni “To eat
solid or liquid food.” Neno “Nestevo” likiunga hayo maneno
mawili ya Kiyunani “Ne” na “Esthio”, inaleta maana ya “Bila
kula chakula au kinyajia chochote.” Kwa hiyo maana ya kufunga ni kutokula
chakula wala kinywaji chochote.
Kufunga siyo kuacha kusoma vitabu, kuacha kuchana nywele au kuacha n.k. Bali
kufunga ni kuacha kula na kunywa kinywaji chochote. Maana hii ya kufunga
inathibitishwa na maandiko yafuatayo; Ezra 10:6; Yona 3:7; 2 Samweli
3:35; Esta 4:16; Kumbukumbu; 9:9; Matendo 9:9.
Kufunga siyo kuacha kula vyakula kama wali, ugali au mihogo halafu tukawa
tunakunywa maji, soda, juisi, maziwa, uji au kula matunda n.k. Kufunga siyo kula
vyakula laini na kuacha vyakula vigumu, bali kufunga ni kuacha kula chakula na
kunywa kabisa.
Wapo
Wakristo ambao wanahalalisha kwamba kufunga unaweza kula vyakula laini au
kunywa tu na ukaacha vyakula vigumu, hiyo siyo sahihi kabisa. Wakristo hao hutumia
andiko la Danieli 10:2-3 linalosema, “Katika siku zile mimi, Danieli,
nalikuwa nikiomboleza muda wa majuma matatu kamili. Sikula chakula
kitamu, wala nyama wala divai haikuingia kinywani mwangu, wala sikujipaka
mafuta kabisa, hata majuma matatu kamili yalipotimia.” Katika andiko hili “Sikula
chakula kitamu” kwa tafsiri ya Biblia ya kiingereza (The living Bible)
chakula kitamu ni “Desserts” au “Pudding”. Neno la Kiingereza “Desserts”
au “Pudding’ lina maana ya chakula kitamu kinacholiwa baada ya mlo (matunda),
chakula hicho ni kama maembe, ndizi, nanasi, papai, machungwa n.k. Katika
mistari hiyo Danieli anasema kwamba, siyo tu kwamba hakula chakula, bali hata
matunda, yaani hakula chakula wala kunywa chochote kwa muda wote wa wiki tatu.
UMUHIMU WA KUFUNGA
Bwana
wetu Yesu Kristo, anamtazamia kila mtu aliyeookoka kuwa na maisha ya kufunga
pale anapotuambia, “Tena mfungapo,” “Bali wewe ufungapo” (Mathayo
6:16-18). Maombi ya kufunga, yanampa nguvu ya kiroho kila aliyeokoka, na
kumfanya imani yake ipande kwa viwango vya juu sana. Wanafunzi wa Yesu,
hawakuweza kumtoa pepo kwa sababu ya upungufu wa imani yao iliyotokana na
kukosa kusali na kufunga. Na ndiyo maana Bwana Yesu akawapa maelekezo kwamba,
hawana budi kusali na kufunga ili wawe na imani hiyo; Mathayo 17:21 Biblia
inasema, “Lakini namna hii haitoki ila kwa kusali na kufunga.” Mtu
anapofunga, mwili huwa na nidhamu kwa sababu ya kutiishwa, hivyo kumfanya mtu
huyo kuwa rohoni sana na hatimaye kumpa nafasi nzuri ya kuzungumza na Mungu.
MIFANO YA KIBIBLIA YA WATAKATIFU
WALIOKUWA WAKIFUNGA
1. Yesu Kristo- Bwana wetu Yesu Kristo baada ya kujaa Roho
Mtakatifu, alifunga siku arobaini na baada ya mfungo huo alirudi kwa Nguvu ya
Roho Mtakatifu (Luka 4:1, 14).
2. Musa (Kutoka 34:28).
3. Ezra (Ezra 10:6).
4. Eliya (1 Wafalme 19:8).
5. Daudi (Zaburi 109:24).
6. Yoshua (Kutoka 24:12-15).
7. Danieli (Danieli 10:1-3).
8. Anna binti Fanueli (Luka 2:36-37).
9. Paulo (Matendo 9:8-9; 2 Wakorintho 11:27).
10. Paulo na Barnaba (Matendo 14:23).
11. Kanisa la kwanza (Matendo 13:1-3).
Ikiwa
watakatifu wengi zama za Biblia walifunga na kupata ushindi mkubwa katika
maisha yao, sisi nasi hatuna budi kuchukua hatua ya kufunga. Tunapopuuza
kufunga, tutakuwa dhaifu sana kiimani na hatimaye kukosa ushindi.
NGUVU YA KUFUNGA
Sehemu
nyingi katika Biblia, tunaona jinsi mambo yalivyobadilika baada ya kufunga na
kuomba. Kufunga kunaweza kutokana na mbiu ya kufunga, yaani kufunga
kunakotokana na kiongozi kutangaza watu wafunge (2 Nyakati 20:3-4; Yona
3:7-8; Ezra 8:21). Pia kufunga kunaweza kutokana na uamuzi wa mtu binafsi (Nehemia
1:4). Mifano ifuatayo, inatufundisha juu ya nguvu ya kufunga;
1. Wana wa Israeli walipigwa mfululizo katika vita na wana wa
Benyamini. Baada ya kushindwa mfululizo, wakaamua kufunga na kuomba (Waamuzi
20:20-26). Baada ya kufunga na kuomba matokeo yakabadilika, Benyamini
wakapigwa sana, na wana wa Israeli wakashinda vita kwa kuiteketeza miji ya
maadui zao kwa moto (Waamuzi 20:34-48).
2. Ezra hakumtegemea mfalme, bali alifunga, na matokeo ya kufunga
yakawa kwamba mkono wa Mungu ulikuwa pamoja naye, yeye na wenzake wakaokolewa
kwa mkono wa adui (Ezra 8:31-32). Ikiwa kanisa linahitaji kuokolewa
kutoka katika mkono wa adui, ni lazima liwe na wafungaji.
3. Yehoshafati alipata taarifa za majeshi kombaini ya maadui
waliotaka kumpiga. Akatangaza kufunga na kuomba (2 Mambo ya Nyakati 20:1-4),
matokeo yake wakashinda vita kirahisi mno kwa sifa tu (2 Mambo ya nyakati
20:22-25).
4. Nehemia alivyopata taarifa za kubomolewa kwa ukuta wa Yerusalemu
na malango yaliyoteketezwa kwa moto, alifunga na kuomba (Nehemia 1:3-4), na
matokeo yake ukuta ulijengwa tena kwa muujiza mkubwa (Nehemia 6:15-16).
5. Hasira ya Bwana kwa kanisa, au Taifa, inayotokana na uovu wa
watu, inaweza utoweshwa endapo watu hao watakuwa tayari kufunga na kuomba (1
Wafalme 21:27-29; Yona 3:7-10; Ezra 10:6).
MUDA WA KUFUNGA
Biblia
haijaweka sheria juu ya muda maalum wa kufunga. Hata hivyo tukichunguza vipindi
ambavyo watakatifu zama za Biblia walifunga, tunaweza kupata mwanga juu ya muda
wa kufunga katika kuombea jambo husika. Hata hivyo mifungo mingi katika
Biblia haitaji idadi ya siku zilizotumika katika mifungo hiyo, lakini katika
jedwali lifuatalo, tutaangalia mifungo ambayo imetaja siku pamoja na sababu za
kufanya mifungo hiyo;
|
MFUNGAJI
|
KIPINDI CHA KUFUNGA
|
SABABU ZA KUFUNGA
|
ANDIKO
|
1.
|
Daudi
|
Asubuhi hadi jioni
|
Kumuombolezea aliyekufa
|
2 Samweli 3:35
|
2.
|
Israeli
|
Asubuhi hadi jioni
|
Kumuuliza Bwana juu ya kushindwa kwao.
|
Waamuzi 20:24-27
|
3.
|
Daudi
|
Asubuhi hadi jioni
|
Kumlilia aliyekufa
|
2 Samweli 1:12
|
4.
|
Yuda
|
Siku moja
|
Kuutafuta uso wa Mungu.
|
Nehemia 9:1-4
|
|
|
|
|
|
5.
|
Yuda
|
Siku moja
|
Kuutafuta uso wa Mungu.
|
Yeremia 36:6
|
6.
|
Mafarisayo
|
Siku moja mara mbili kwa juma.
|
|
Luka 18:9-12
|
7.
|
Wana wa Israeli
|
Siku moja
|
Kumlilia Bwana waokolewe na mkono wa Wafilisti.
|
1 Samweli 7:6-14
|
8.
|
Esta na wana wa Israeli
|
Siku tatu
|
Kumwomba Mungu watoke katika hatari ya kuuawa.
|
Esta 4:13-16
|
9.
|
Kundi la watu
|
Siku tatu
|
Kumsikiliza Bwana Yesu akifundisha
|
Mathayo 15:32
|
10.
|
Paulo
|
Siku tatu
|
Wokovu na wito wa Paulo.
|
Matendo 9:9
|
11.
|
Daudi
|
Siku saba
|
Kumwomba Mungu kwa ajili ya mtoto.
|
2 Samweli 12:16-18
|
12.
|
Wana wa Israeli
|
Siku saba
|
Kuomboleza kifo cha Sauli na wanawe.
|
1 Samweli 31:13
|
13.
|
Paulo na watu 276
|
Siku 14 nzima
|
Safari iliyojaa misukosuko
|
Matendo 27:33-37.
|
14.
|
Danieli
|
Siku 21 nzima
|
Kumwomba Mungu ili kufunuliwa jambo.
|
Danieli 10:1-3
|
15.
|
Musa
|
Siku 40 nzima
|
Kuwaombea wana wa Israeli na kuketi mbele za Bwana.
|
Kumbukumbu 9:9, 18, 25-29; 10:10
|
16.
|
Yoshua
|
Siku 40 nzima
|
Kuketi mlimani mbele za Mungu.
|
Kutoka 24:12-15
|
|
|
|
|
|
17.
|
Eliya
|
Siku 40 nzima
|
Safari ndefu.
|
1 Wafalme 19:5-8
|
18.
|
Bwana Yesu
|
Siku 40 nzima
|
Kujaribiwa nyikani kutokana na kuongozwa na Roho.
|
Mathayo 4:1-2
|
Kutokana na
vipindi hivi vya ufungaji wa watakatifu mbalimbali kama tulivyoona hapo juu,
tunajifunza mambo yafuatayo;
1. Kipindi cha kufunga katika kumtafuta Bwana kwa maombi, kinabidi
kiwe siyo chini ya siku moja (masaa 24).
2. Kipindi cha kawaida cha mfungo kinaweza kufikia siku tatu nzima
yaani masaa 72 yote. Ni katika uzito usio wa kawaida tunazidisha hapo kwa
maongozi ya Roho Mtakatifu, hata hivyo siku hazizidi saba.
3. Kufunga zaidi ya siku saba nzima, lazima kuambatane na
kufunuliwa neno. Mtu hawezi kufunga siku 40 bila kula wala kunywa mpaka kuwe na
maongozi dhahiri ya Mungu, uwepo wake na msaada wake maalum (1 Wafalme
19:8).
Mwanafunzi
halisi wa Kristo, atajipangia muda wa kufunga angalau siku tatu kwa kila mwezi.
Inaweza kuwa siku moja katika wiki mara tatu na siyo mfululizo.
VIZUIZI VYA NGUVU ZA KUFUNGA
1. Nia ya kufunga (Warumi 12:2).
Nia ya kufunga, ikiwa
kinyume na Neno la Mungu, huzuia kupatikana kwa nguvu ya kufunga.
2. Kufunga huku tukiwa na dhambi (Yeremia 14:10-12; Isaya 58:3-5).
3. Kufunga bila kuomba
Kufunga ni lazima
kuambatane kumtafuta Bwana kwa maombi (2 Nyakati 20:3-4; Ezra 8:21; Mathayo
17:21). Kufunga bila kuomba ni kushinda njaa kusiko na faida.
4. Kufunga hakupaswi kuchukua nafasi ya imani.
Hatupaswi kuwaza kila
jambo haliwezekani mpaka tufunge kwanza. Pasipo imani haiwezekani kumpendeza
Mungu (Waebrania 11:6; Yakobo 1:6). Ni lazima ifahamike kwamba kufunga
kunachochea tu imani.
NA: DR. GODWIN
GUNEWE